
Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa amesema wagombea wa uchaguzi wa serikali za mitaa ambao hawakutendewa haki, bado wanayo nafasi ya kukata rufaa.
Mchengerwa amesema rufaa hizo zinazokatwa ngazi ya wilaya zinapaswa kukatwa na wagombea wenyewe na si vyama vya siasa. Muda wa rufaa umeanza Novemba 10 hadi kesho Jumatano, Novemba 13, 2024.
Waziri huyo amesema hayo leo Jumanne, Novemba 12, 2024 jijini Dar es Salaam katika semina ya wahariri kuhusu Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
“Muda wa kukata rufaa bado upo, watu wakate rufaa wasikae majumbani na kuviachia vyama vyao, rufaa inakatwa na mgombea. Kwa hiyo wale ambao wanaona hawajatendewa haki wakate rufaa sasa,” amesema.
Aidha, Mchengerwa amesema uchaguzi huo utakaofanyika Jumatano ya Novemba 27, 2024 umeshirikisha vyama vyote 19.
Ujasiriamali ni kazi halali
Mwanasheria wa Tamisemi, Mihayo Kadete amesema ujasiriamali ni kazi halali inayotambulika kiserikali, si sawa kutumika kuwaengua wagombea kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa.
Kadete amesema si sahihi mgombea kuenguliwa kwa kigezo tu amejaza kazi halali ni mjasiriamali; na mtu aliyeenguliwa akate rufaa kwa kuwa hiyo ni kazi halali.
Kadete amesema mgombea ambaye hajajiandikisha kupiga kura kwenye eneo lake ni moja ya sababu ya kukosa sifa ya kugombea katika uchaguzi huo utakaofanyika Novemba 27, 2024.
“Mtu akatwe kwa kukosa sifa na si kukatwa kwa kudhamiria bali akatwe kwa haki,” amesema Kadete.
Semina hiyo ya siku moja ya masuala ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 imeandaliwa na Ofisi ya Rais -Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).