
Arusha. Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha linamshikilia Emmanuel Charles Mollel (25) mkazi wa Wilaya ya Arumeru kwa tuhuma za mauaji ya binti mwenye umri wa miaka 17 ambaye jina lake limehifadhiwa.
Akitoa taarifa hiyo leo Machi 6,2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, SACP Justine Masejo amesema mtuhumiwa huyo alitenda tukio hilo Machi 1, mwaka huu.
“Mtuhumiwa huyu tunamshikilia kwa tukio hili la mauaji baada ya kumjeruhi marehemu na kitu chenye ncha kali na kisha kumbaka kabla ya kupoteza maisha wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru Arusha,” amesema.
Awali, bosi wa marehemu, Jenifa Esau amesema kuwa alimleta msichana huyo Februari 18, 2025 kutoka mkoani Singida kwa ajili ya kumsaidia malezi ya mtoto wake mdogo.
“Msichana wangu hana hata wiki mbili tangu nimlete kwa ajili ya kunisaidia kumlea mtoto wakati nikienda kazini.
“Lakini, nashangaa nilipigiwa simu na dada yangu saa moja jioni kuwa amekuja nyumbani kwangu na msichana hayupo wala begi,” amesema.
Amesema kuwa baada ya kupata taarifa hizo aliwahi nyumbani kujua kulikoni, ndipo alipokuta msichana wake wa kazi amejeruhiwa na baadaye kupoteza maisha.
“Baada ya kupigiwa simu kurudi nyumbani nikiwa ndani nikikagua mazingira ndio tukasikia kishindo nyuma ya nyumba mithili ya mtu anayegonga na tulipozunguka ndipo tulimkuta msichana wangu akiwa mtupu tena hoi kwa maumivu makali ya kupigwa, kubakwa na kuchomwa chomwa mwili huku ukivuja damu muda wote akiomba msaada kwa ishara ya mikono,” amesema Jenifa.
“Tulipiga kelele na majirani wakaja kisha kumpakia kwenye pikipiki tukaelekea polisi kutoa taarifa na kisha Hospitali ya Mount Meru kwa matibabu, lakini alifia njiani,” amesema.
Amesema kuwa baada ya kumaliza taratibu za kuhifadhi mwili mochwari walirudi nyumbani na asubuhi wakaanza kupeleleza muhusika wa tukio hilo.
“Katika kuzunguka nyumba tuliona michirizi ya damu kutoka kwenye mlango wa mtoto wa dada yake (Emmanuel) ambaye anaishi naye chumba cha jirani,” amesema.
Amesema kuwa bada ya kuona ishara hizo waliamua kuchukua maamuzi ya kuvunja mlango, ndipo wakakuta damu zimetapakaa kila mahali ikiwemo kwenye godoro, ukutani na kwenye sakafu.
“Inaonekana kabisa huyu mtoto wa dada yangu ndio muhusika wa tukio maana tumekuta damu nyingi ndani ya chumba chake, hivyo inaonekana alimvutia ndani kwake na walikuwa na mapambano kabla ya kufanikiwa kutekeleza tukio hilo na kukimbia,” amesema.
Dada wa Jenifa, Judika Maiko ambaye ni mama wa mtuhumiwa amesema kuwa siku ya tukio alikuja mchana kumuacha mwanaye acheze na wenzake kisha akaenda kusuka, alirudi saa 10 jioni na kuamua kumchukua mtoto wake na wa mdogo wake.
“Niliporudi kusuka nilimkuta mtoto wa mdogo wangu analia sana hivyo niliamua kumsaidia huyu dada wa kazi kumbembeleza, lakini hakunyamaza ikabidi niondoke na mtoto wangu na yule wa mdogo wangu ili dada aendelee na kazi zingine kwanza,” amesema.
Amesema kuwa saa 12 jioni aliporudi alikuta mlango uko wazi, lakini dada wa kazi (marehemu) hayupo.
“Nilimpigia mdogo wangu simu kumwambia kumjulisha jambo hilo na yeye kurudi nyumbani haraka kutoka kazini na kuanza kumtafuta.
“Wakati tukitafakari tukasikia kishindo kwa nyuma ya nyumba tulipozunguka tulimkuta msichana huyo akiwa mtupu na ana majeraha makubwa ya kupigwa na kuchomwa chomwa kisu sehemu mbalimbali za mwili wake ikiwemo koromeo na anaonyesha alinyongwa kutokana na michirizi ya shingoni” amesema.
Amesema kuwa wamemuhisi mwanaye Emmanuel (25) ndio mtekelezaji wa tukio hilo kutokana na viashiria vya damu na yeye pekee ndio jirani wa eneo hilo na pia hakuonekana tangu tukio litokee ,ndio maana wameamua kutoa taarifa polisi.