
Jumatano ya Februari 12 mwaka huu, Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo ilitoa mchoro rasmi wa uwanja wa michezo utakaojengwa jijini Dodoma. Siku iliyofuata Februari 13, wizara hiyo ikasaini mkataba wa ujenzi wa uwanja huo.
Kwa mujibu wa mchoro na hata maelezo ya viongozi wa serikali kama katibu mkuu wa wizara hiyo, Gerson Msigwa na Waziri Palamagamba Kabudi, wameutaja uwanja huo kwa jina la Uwanja wa Dodoma.
Uwanja huu utaongeza hadhi ya Dodoma kama mji mkuu na makao makuu ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ama kwa hakika Dodoma inazidi kung’ara kwa miradi mikubwa inayopelekwa kimkakati na serikali katika kuupa hadhi mji huo.
Japo Dodoma ilichaguliwa kuwa mji mkuu tangu mwaka 1973, lakini moto huu wa sasa ulianza mwaka 2016 pale Rais wa Awamu ya Tano, John Pombe Magufuli alipotangaza kwamba serikali yake itahamia Dodoma mara moja.
Baada ya tangazo hilo, upepo ukabadilika na ukaanza kuvumia Dodoma.
Kila kitu sasa pakawa Dodoma na harufu ya makao mkuu ya nchi ikaanza kunukia barabara.
Hapo ndipo mwanasiasa mkongwe, Pius Msekwa alipoibuka na kutoa historia nzima ya safari ya Dodoma kuwa makao makuu ya nchi.
Msekwa alisema historia ya Dodoma kuwa makao mkuu inarudi nyuma zaidi ya mwaka 1974, pale Waziri Mkuu Rashid Kawawa alipohamishia ofisi yake mjini hapo kutoka Dar es Salaam baada ya Chama cha TANU na serikali kuuchagua mji huo kuwa makao mkuu mwaka mmoja nyuma yake.
Katika mahojiano maalumu na Gazeti la Jamboleo mwaka 2016, Msekwa alisema anakumbuka mwaka 1966 alipokuwa katibu wa bunge, ndipo kwa mara ya kwanza hoja ya Dodoma kuwa mji mkuu ililetwa bungeni.
Msekwa alisema kwamba wazo la Dodoma kuwa mji mkuu lililetwa kama hoja binafsi na Mbunge Joseph Nyerere.
“Mbunge huyo alisimama bungeni na kutoa hoja binafsi kutaka Serikali ihamie Dodoma,” alisema Msekwa na kuendelea.
“Msingi wa hoja yake ni kwamba kama serikali itafanyia shughuli zake Dodoma itakuwa rahisi kuiangalia nchi kwa kuwa mkoa huo upo katikati. Ni rahisi wakandarasi wakatokea Dodoma kwenda Mwanza kuliko kutoka Dar es Salaam.”
Maneno haya yalirudiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Mei 20, 2023, wakati wa hafla ya uzinduzi wa Ikulu ya Chamwino.
Kwa hiyo wazo la Dodoma kuwa makao makuu ya nchi lilitoka kwa Joseph Nyerere, lakini je, ni nani huyu Joseph Nyerere?
Ni ndugu wa kuzaliwa wa baba wa taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Baba mzazi wa Mwalimu Nyerere, Chifu Burito Nyerere, alikuwa na wake 22.
Mama mzazi wa Mwalimu Julius Nyerere aliyeitwa Mgaya wa Nyang’ombe.
Baada ya kuupokea Ukristo na kubatizwa, akaitwa Christina.
Alikuwa mke wa tano na alizaa watoto sita akiwemo Kambarage Nyerere ambaye baada ya kubatizwa akaitwa Julius na Kizurira Nyerere ambaye baada ya kubatizwa akaitwa Joseph.
Lakini hawa wote majina yao ya kabla ya ubatizo hawakuyaacha,
wakaendelea kuyatumia, ndipo Kambarage akaitwa Julius Kambarage Nyerere, na Kizurira akawa Joseph Kizurira Nyerere.
Sasa huyu Joseph Kizuzira Nyerere ndiye aliyetoa wazo la kuhamishia
Dodoma makao makuu ya chama na serikali, mwaka 1966.
Na kuonesha kwamba alijua anafanya nini, ngoja nikupe mkasa ufuatao.
Katika yale mahojiano yake, Pius Msekwa alisema kwa taratibu za wakati huo, hoja ikitolewa bungeni, serikali inapewa muda wa kuijadili na kuiridhia.
“Katika kuijibu hoja hiyo, aliyekuwa Waziri wa Elimu, Paul Bomani aliliambia bunge kuwa pamoja na kwamba hoja ina tija, serikali haina pesa kwa sababu hesabu zilionyesha kuwa zilihitajika shilingi 3 bilioni kukamilisha mradi huo,” alisema Msekwa.
Majibu hayo yalimfanya Joseph Nyerere aiondoe hoja yake mezani, kwa kufanya hivyo akawa amelilinda wazo łake na kuliacha hai hadi wakati mwingine serikali itakapopata pesa.
Msekwa anasema huu ulikuwa uamuzi wa kijanja sana, kwani Joseph Nyerere alitaka hoja yake isitishwe mpaka wakati ambao serikali ingepata pesa.
Angelazimisha wapige kura wakati ule hoja hiyo ingetupwa, basi ingekuwa imekufa kabisa.
Msekwa akasema hoja hiyo ilifufuliwa tena mwaka 1972 katika mkutano wa Kamati ya Siasa ya Chama cha TANU Mkoa wa Mwanza.
“Kamati hiyo ilijadili hoja hiyo na kutoa mapendekezo yake kwenye chama ngazi ya taifa na uamuzi ukafanyika mwaka 1973,” alisema Msekwa.
Ilikubaliwa iitishwe kura ya maoni ya wanachama wote na kura hizo
zilipigwa kwenye matawi yote ya TANU wakati huo.
Kwa mujibu wa Msekwa matawi yaliyopiga kura hiyo yalikuwa 1,800 na kati yake matawi 800 yalikataa hoja hiyo na matawi mengine yaliyobaki 1,000 yakaridhia.
Kwa wakati ule wa chama kimoja, kama wazo litaamuliwa kwenye chama serikali lazima ilitekeleze.
Hivyo serikali sasa ikachukua wazo la kuhamia Dodoma na ikajipa miaka 10 kuanzia 1973 hadi 1983.
Kwa kuanzia, Rais Julius Nyerere akaunda Wizara ya Ustawishaji Makao Makuu na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA). Hilo lilifanyika mwezi Oktoba.
Mwaka 1974, Waziri Mkuu Rashid Kawawa akahamishia ofisi yake Dodoma, kilichofuata baada ya hapo ni historia.
Kwa hiyo leo hii unapojengwa mradi mkubwa kama uwanja huu, ni busara watu kama hawa wakatambuliwa michango yao kwa kutoa majina yao.
Zaidi juu ya Joseph Nyerere
Mwaka 1958, viongozi wa TANU, Mwl. Julius Nyerere na Rashid Kawawa, walienda Ghana kwenye sherehe za maadhimisho ya mwaka mmoja wa uhuru.
Wakiwa huko, Kawawa akakutana na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Israel, Bi. Golda Meir, ambaye baadaye alikuwa waziri mkuu.
Katika mazungumzo yao, Bi Meir akamdokeza Kawawa namna Israel inavyoandaa vijana wao kuwa wazalando.
Mpango huo ukamvutia Kawawa na aliporudi nchini akamwambia Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa TANU, Joseph Nyerere.
Naye akalipeleka kwenye mkutano mkuu wa Umoja wa Vijana wa TANU, baada ya uhuru wazo lile likageuzwa na kuwa JKT ambayo tunatamba nayo sasa kama taifa.
Kwa kifupi inawezekana kama siyo Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa TANU, Joseph Nyerere, kulivalia njuga wazo lile, labda tusingekuwa na JKT.
Siyo lazima uwanja huu tu, tumkumbuke kwa mengine hapo Dodoma.