

- Author, Cherylann Mollan
- Nafasi, BBC News, Mumbai
Maisha mfanyakazi wa inia yamebadilika ghafla baada ya kupata almasi kubwa katika mgodi wa Madhya Pradesh uliopo jimbo la kati la nchi hiyo.
Almasi hiyo ya karati 19.22 inatajiwa kuuzwa kwa dola 95,570 za kimarekani katika mnada wa serikali.
Raju Gound alisema amekuwa akikodisha migodi katika jiji la Panna kwa zaidi ya miaka 10 kwa matumaini ya kupata almasi.
Panna inasifika kwa hifadhi zake za almasi na mara nyingi watu hukodisha migodi ya bei nafuu,kutoka kwa serikali ili kutafuta mawe hayo ya thamani.

Mamlaka ya Kitaifa la Maendeleo ya Madini (NMDC) huendesha mradi wa uchimbaji wa almasi hukoPanna.
Pia hukodisha migodi ya kina kifupi kwa watu binafsi, familia na makundi ya ushirika ambao hutafuta almasi, kwa kutumia zana na vifaa vya kimsingi.
Ugunduzi wowote hukabidhiwa kwa ofisi ya almasi ya serikali, ambayo hutathmini jiwe.
“Migodi hii inaweza kukodishwa kwa takriban rupee 200-250 [kwa muda maalum],” Anupam Singh, afisa katika ofisi ya almasi ya serikali ya jimbo, aliiambia BBC.
Mnamo mwaka wa 2018, mfanyakazi kutoka Bundelkhand alipata almasi yenye thamani ya rupee milioni 15m kwenye mgodi wa Panna. Hata hivyo, uvumbuzi huo ni nadra.
Bw Singh alisema kuwa ingawa watu wengi wamepata mawe madogo, mawe aliyopata Bw Gound ilijulikana kwa sababu ya ukubwa wake.
Bw Gound aliambia BBC kwamba babake alikodisha mgodi huo katika kijiji cha Krishna Kalyanpur Patti karibu na Panna takriban miezi miwili iliyopita.
Alisema familia yake hukodisha migodi zaidi wakati wa msimu wa masika wakati kazi ya kilimo na uashi inapoisha.
“Sisi ni maskini sana na hatuna chanzo kingine cha mapato. Kwa hiyo tunafanya hivi kwa matumaini ya kupata pesa,” alisema.

Amewahi kusikia hadithi za watu kupata almasi na alitumaini kwamba yeye pia angebahatika siku moja.
Siku ya Jumatano asubuhi, alienda kwenye mgodi huo kufanya kazi yake ya kila siku ya kutafuta jiwe hilo la thamani.
“Ni kazi ya kuchosha. Tunachimba shimo, tunatoa udongo na vipande vya mawe, kuvichakata kwenye ungo na kisha kuchuja kwa uangalifu maelfu ya vipande vya mawe viliyoshikana na madogo kutafuta almasi,” alisema.
Na alasiri hiyo, kazi hiyo ngumu ilizaa matunda iyakayobadilisha maisha yake .
“Nilikuwa nikipekua mawe nikaona kitu mithili ya kipande cha glasi, niliinua macho yangu na kuona mwanga hafifu, ndipo nilipojua nimepata almasi,” alisema.

Baada ya ugunduzi huo Bw Gound alipeleka bidhaa aliyoipata kwenye ofisi ya serikali ya almasi, ambako ilitathminiwa na kupimwa.
Bw Singh alisema almasi hiyo itauzwa katika mnada ujao wa serikali na kwamba Bw Gound atapokea fidia yake baada ya mrahaba na ushuru wa serikali kukatwa.
Bw Gound anatumai kujengea familia yake nyumba nzuri na kulipia masomo ya watoto wake. Lakini kwanza, anataka kulipa deni lake la rupee 500,000.
Anasema haogopi watu kujua kuhusu almasi hiyo kwani anapanga kugawana pesa hizo na jamaa 19 wanaoishi naye.
Kwa sasa, ameridhika tu kujua kwamba pesa zitamjia.
“Kesho nitaenda tena mgodini kutafuta almasi,” alisema.
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi