
Dar es Salaam. Bernardo Sepeku (63), mtoto wa marehemu John Sepeku, Askofu Mkuu wa kwanza wa Kanisa la Anglikana Tanzania, ameieleza Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi jinsi alivyopigania haki ya umiliki wa kiwanja alichorithi kutoka kwa baba yake kwa zaidi ya miongo minne bila mafanikio.
Akitoa ushahidi wake jana, Machi 28, 2025, katika kesi ya ardhi namba 378/2023 aliyofungua dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Askofu Jackson Sostenes na Kampuni ya Xinrong Plastic Waste Industry Co. Ltd, Bernardo alidai kiwanja hicho kilitolewa kwa baba yake kama zawadi na kanisa hilo mwaka 1978, lakini baadaye akanyang’anywa umiliki wake.
Sepeku alipewa zawadi na kanisa hilo ambayo ni nyumba iliyopo Buguruni na kiwanja chenye ukubwa wa ekari 20 kilichopo Buza, wilayani Temeke, kama zawadi kwa kutambua mchango wake katika kanisa hilo, akiwa kama Askofu wa Mkuu wa kwanza kanisa hilo.
Bernardo katika kesi hiyo, anadai alipwe Sh3.72 bilioni ambayo ni fidia ya hasara ya kifedha iliyopatikana kutokana na uvamizi wa mali ya ardhi katika kiwanja hicho.
Pia, anaiomba mahakama alipwe fidia ya Sh493.65 milioni ambayo ingepatikana baada ya kukomaa mazao yaliyokuwepo kwenye shamba hilo.
Hata hivyo, wakati kesi hiyo ikiendelea na usikilizwaji, mdaiwa wa tatu katika shauri hilo, kampuni ya Xinrong Plastic Waste Industry Co Ltd, haijawahi kufika mahakamani hapo tangu kesi hiyo ilipofunguliwa licha ya kupokea wito wa kuitwa mahakamani.
Akiongozwa kutoa ushahidi wake na wakili Deogratias Butawantemi akishirikiana na Gwamaka Sekela, amedai Oktoba 27, 2020 Mahakama ya Mwanzo Kariakoo ilimteua kuwa msimamizi wa mirathi ya marehemu askofu John Sepeku.
Alimweleza Jaji Arafa Msafiri anayesikilisha shauri hilo kuwa mwaka 1978 na 1980 kulifanyika mkutano mkuu wa Sinodi, ambapo pamoja mambo mengine, ulipendekeza Askofu Sepetu apewe zawadi baada ya kustaafu utumishi wake.
Mtoto huyo ambaye ni shahidi wa nane wa upande wa mlalamikaji, alidai kuwa mkutano huo ulikuwa ni mahususi kwa ajili ya mapendekezo ya kutoa zawadi kwa Askofu Sepetu, ambaye alikuwa askofu wa kwanza mkuu tangu kuanzishwa kwa kanisa hilo mwaka 1970.
Vilevile, kikao hicho kilielekeza Sepeku ajengewe nyumba Buguruni na baada ya mapendekezo hayo kufanyika, kanisa lilitekeleza mapendekezo hayo na Askofu Sepeku alijengewa nyumba Buguruni na kupewa ardhi ekari 20.
“Mpaka sasa ni miaka 44 imepita, kanisa halijaweza kutupatia hatimiliki ya eneo la ekari 20 ambalo mzee wangu (marehemu John Sepeku) alipewa na kanisa hili kama zawadi, baada ya kustaafu utumishi wake wa kulitumikia kanisa,” alidai Bernardo.
Nyaraka zapokewa na mahakama
Bernardo aliwasilisha nyaraka sita kuthibitisha madai yake kuwa baba yake alipewa eneo hilo kihalali, ikiwemo hati ya usimamizi wa mirathi na muhtasari wa vikao vya kuduma vya Sinodi uliofanyika mwaka 1978 na 1980.
Pia, aliwasilisha barua ambazo familia ya Sepeku ilikuwa ikiiandikia Bodi ya Wadhamini ya Kanisa hilo kuhusu ucheleweshaji wa mchakato wa kuhamisha umiliki wa kiwanja alichopewa Askofu Sepeku.
Bernardo ambaye ni mtoto wa 12 kwa Askofu Sepeku, aliwasilisha pia barua kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Temeke kwenda Bodi ya Wadhamini wa kanisa hilo, ikiitaka bodi ikamilishe mchakato wa kuhamisha umiliki kutoka kwake kwenda kwa familia ya Sepeku.
Vilevile aliwasilisha hati ya kutokukubaliana kutoka Baraza la Ardhi la Kata ya Buza, lililopo wilaya ya Temeke.
Barua nyingine aliyowasilisha mahakamani hapo ni kutoka Dayosisi ya Dar es Salaam ya kanisa hilo kwenda familia ya Sepeku ambayo ilikuwa inahusu mawasiliano baina ya familia na dayosisi hiyo.
Hata hivyo, baada ya kuwasilisha nyaraka hizo na kuomba mahakama izipokea zitumike kama ushahidi katika kesi hiyo, Wakili wa mdaiwa wa kwanza na wa pili katika kesi hiyo, Dennis Malamba alipinga nyaraka hizo kupokelewa na mahakama hiyo, akidai hazijakidhi vigezo vya kisheria, ikiwemo Sheria ya Tangazo la Serikali namba 761 la mwaka 2021.
Pingamizi hilo lilijibiwa na Wakili Deogratias akidai kuwa sheria hiyo inatoa maana ya namna ya kupeleka ushahidi.
Baada kusikiliza hoja na mapingamizi ya pande zote mbili, Jaji Msafiri alitupilia mbali mapingamizi ya Wakili Malamba na mahakama ikapokea nyaraka zote sita ambazo zitatumika kama ushahidi katika kesi hiyo.
Kiini cha kesi hiyo:
Katika ushahidi wake Bernardo alidai kuwa Julai 2023 alipewa taarifa na mlizi wa eneo hilo kuwa kuna uvamizi umetokea katika eneo lao na mali zilizokuwepo ndani ya shamba hilo zimeharibiwa.
“Baada ya kupata taarifa hizo, niliwasiliana na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Kanisa la Anglikana Tanzania, ambaye ni Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, Maimbo Mndolwa ambaye ndiye anatunza mali, kwa kimpigia simu na kumlalamikia kuwa kuna kampuni imeingia katika shamba letu na kuleta uharibifu katika mazao,” alidai Bernardo.
Hata hivyo, amesema Askofu Mndolwa alimweleza Bernardo kuwa hafahamu kama shamba lao lililopo Buza limevamiwa.
“Baada ya kuniambia hajui chochote, mimi nilifanya jitihada za kwenda hadi katika shamba lililovamiwa na kukuta Kampuni ya Xinrong Plastic Waste Industry Co Ltd, ikiendelea na ujenzi na nilipowahoji, walisema eneo hilo wamekabidhiwa na Askofu wa Dayosisi ya Dar es Salaam, ambaye ni mlalamikiwa wa pili katika kesi hii.
Alidai baada ya kupewa taarifa hiyo na kampuni hiyo, alikwenda Baraza la Kata Buza ili aweze kupata usuluhisho wa awali wa suala hilo ambapo Mwenyekiti wa Bodi ya Kanisa la Anglikana Tanzania alipewa wito wa kufika katika shauri hilo pamoja na kampuni ya Xinrong Plastic Waste Industry Co Ltd.
“Siku ya usikilizwaji wa shauri Baraza la Kata, alikuja Mwenyekiti wa Bodi na washauri wa bodi, lakini kampuni ya Xinrong Plastic Waste Industry Co Ltd haikuwa na mwakilishi katika shauri hilo na badala yake alikuja Askofu Jackson wa Dayosisi ya Dar es Salaam” alidai Bernardo.
Alidai katika uendeshaji wa shauri hilo, Mwenyekiti wa Bodi ya Kanisa la Anglikana Tanzania alikiri mbele ya Baraza kuwa Askofu Mkuu wa kwanza wa kanisa hilo, John Sepeku alipewa zawadi ya ardhi eneo la Buza.
“Mwenyekiti wa Bodi, alieleza Baraza kuwa amepewa taarifa na Bernardo kuwa eneo hilo limevamiwa, hivyo aliomba jambo hilo kulitoa katika Baraza la Kata na badala yake, wakajadiliane nje ya baraza kwa kukutana na wajumbe wa bodi hiyo,” alidai Bernardo na kudai na kuongeza kuwa:
“Baada ya Mwenyekiti kueleza hayo, Askofu Jackson alisimama kwa niaba ya Kampuni ya Xinrong Plastic Waste Industry Co Ltd na kusema kuwa yeye ndiyeo aliyewaweka pale na mwisho wa siku tulishindwa kufikia muafaka” amedai Bernado
Akiendelea kutoa ushahidi, alidai kuwa askofu Jackson aliwaeleza kuwa iwapo itadhibitishwa eneo hilo ni mali ya marehemu Sepeku, basi yupo tayari kulipa gharama.
Jaji Msafiri aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 7 na Machi 8, 2025 saa tano asubuhi, ambapo Bernardo ataendelea kutoa ushahidi wake.