
Morogoro. Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro limemkamata John Kandole (11), mwanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Lwemba kwa tukio la kujaribu kumuua mama yake mzazi aitwaye Regina Kalinga (44) kwa kuweka sumu kwenye chakula huku chanzo kikidaiwa kuwa ni tabia ya mama yake huyo kupenda kumtuma tuma na kumnyima muda wa kucheza na wenzake.
Akitoa taarifa hiyo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama amedai tukio hilo limetokea Februari 11 mwaka huu mchana katika kitongoji cha Msalabani Juu, Kijiji cha Lwemba, kata ya Kidodi, Wilaya ya Kilosa baada ya kijana huyo kuweka sumu aina ya ‘Lara force’ ambayo hutumika kuua wadudu kwenye mbogamboga.
Kamanda Mkama amedai mtoto ameweka sumu hiyo kwenye chakula aina ya wali maharage uliopikwa na mama yake huyo mzazi.
“Baada ya kula chakula mama huyo na wanafamilia wengine watano walianza kuumwa tumbo na kukimbizwa hospital ya Mtakatifu Kizito ambapo amelazwa akiendelea na matibabu, watu wengine watano wametibiwa na kuruhusiwa kurudi nyumbani,” amedai Kamanda Mkama.
Walioruhusiwa kurudi nyumbani ni pamoja na Eusebia Kamili (53), Zena Salehe (17), Patrick Ndola (11), Alvin Alex (5) na Hidaya Swedi (1),”
Hata hivyo, Kamanda Mkama amedai wanaendelea na uchunguzi zaidi kuhusiana na tukio hilo huku mtoto huyo akiendelea kuhojiwa.
Katika tukio jingine mwanaume mmoja amemuua mke wake kwa kumchoma na kitu chenye ncha kali kifuani kisha naye kujichoma na sindano ya kushonea viatu na kujinyonga kwa kutumia kamba ya katani ambapo chanzo cha tukio hilo kinadaiwa kuwa ni wivu wa kimapenzi.
Katika taarifa yake Kamanda Mkama amedai tukio hilo limetokea Februari 11 jioni katika kitongoji cha Kiembeni Wilaya ya Morogoro na kumtaja mwanamke huyo ni Naria Abdalah (34) mkazi wa Kiembeni Mikese.
“Mwanaume huyo aliyefahamika kwa jina la Hussein Mtawanja (40) baada ya kufanya mauaji hayo naye alichukua sindano ya kushonea viatu na kujichoma tumboni, na bado akaona haitoshi akachukua kamba ya katani na kujinyonga akiwa ndani ya nyumba yao,” amedai Kamanda Mkama.
Amedai miili ya marehemu hao imehifadhiwa katika hospitali ya rufaa Mkoa wa Morogoro kwa ajili ya uchunguzi wa kidaktari na polisi wanaendelea na uchunguzi zaidi.