
Arusha. Mahakama Kuu Masijala Ndogo ya Dar es Salaam imewaachia huru Halima Shabani na baba yake wa kambo, Mbalu Sambalu, waliokuwa wameshtakiwa kwa mauaji ya baba yake Halima, Shabani Rashid.
Halima na baba yake wa kambo walishtakiwa kwa kosa la mauaji kinyume na kifungu cha 196 na 197 cha Kanuni ya Adhabu, ambapo ilikuwa inadaiwa na upande wa mashtaka kuwa walimuua Shabani Aprili 8, 2023 katika eneo la Mapatano-Mbwewe, Chalinze mkoani Pwani.
Katika utetezi wake, Halima aliieleza Mahakama kuwa sababu kubwa iliyomfanya amkimbie baba yake (Shabani) ni kutokana na marehemu alikuwa akifanya naye mapenzi kwa nguvu na matokeo yake alipata ujauzito na kujifungua mtoto.
Hukumu hiyo iliyowaachia huru imetolewa Aprili 16, 2025 na Jaji Awamu Mbagwa aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo, ambaye baada ya kusikiliza pande zote mbili alieleza upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha kesi bila kuacha shaka, hivyo inawaona washtakiwa hawana hatia na kuwaachia huru.
Ilivyokuwa
Katika kesi hiyo, upande wa mashitaka ulikuwa na mashahidi watano ambao ni Dk Victor Bamba (PW1), Ramadhan Rashid (PW2), Mussa Zuberi (PW3), Hashimu Daudi (PW4) na F6413 Sajenti John (PW5) pamoja na vielelezo vitatu ikiwemo ripoti ya uchunguzi ya mwili wa marehemu.
Wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo upande wa Jamhuri uliwakilishwa na Mawakili Neema Kwayu na Caroline Kigembe, huku washtakiwa hao wakiwakilishwa na mawakili Ramadhani Makange na Hilda Mushi.
Mshtakiwa wa kwanza (Mbalu), alifunga ndoa na mama yake Halima (mshtakiwa wa pili) baada ya kuachana na Shabani (marehemu), ambapo Halima alilazimika kuhama kutoka nyumbani kwa baba yake na kwenda kukaa na mama yake eneo la Mapatano kutokana na unyanyasaji wa kijinsia aliokuwa akiupata kutoka kwa baba yake.
Ilielezwa kuwa Aprili 8, 2023, Shabani aliondoka nyumbani kwake na kwenda Mapatano akidai anampelekea mtoto wake dawa, hata hivyo katika ushahidi suala hilo halikuwekwa wazi zaidi.
Ilielezwa kuwa Shabani alikodi pikipiki kwa ajili ya kwenda huko na kumweleza mmiliki wa pikipiki hiyo kuwa atairudisha muda si mrefu lakini hakurejesha pikipiki hiyo wala kurudi nyumbani kwake baada ya kwenda Mapatano.
Kufuatia kutoweka kwa marehemu, ndugu zake walianza juhudi za kumtafuta hadi alipokutwa akiwa amefariki katika msitu wa Mapatano ndani ya kijiji cha Kwang’andu.
PW5 aliieleza mahakama kuwa kabla ya kupatikana mwili huo, pikipiki hiyo ilikutwa imetekelezwa katika eneo la Tanesco na kuwa Mwenyekiti wa Kijiji hicho na mgambo waliichukua pikipiki hiyo hadi Kituo cha Polisi Mbwewe.
Kwa mujibu wa hukumu hiyo, mwenyekiti huyo na mgambo hawakufika mahakamani kutoa ushahidi.
PW1 aliyeuchunguza mwili huo aliieleza Mahakama kuwa mwili wa ulikuwa na majeraha kichwani na mkono wa kulia na chanzo cha kifo ni kuvuja damu nje na ndani.
Mashahidi wa upande wa mashtaka walieleza kuwa kulikutwa kipande cha mbao (fimbo) kikiwa na madoa ya damu kando ya mwili wa marehemu.
PW3 ambaye alikuwa polisi jamii alieleza mwishoni mwa Aprili 2023, alipata taarifa kuwa wahusika wa kifo cha marehemu ni Mbalu, Halima Shabani, Tatu na Mkwayu Gosi.
Mei 27, 2023, PW3 alimkamata Mbalu katika vibanda vya mkaa na baadaye kumpeleka kituo cha Polisi Mbwewe, ambapo ushahidi wa upande wa mashtaka ulikuwa kimya juu ya kukamatwa kwa Halima, lakini Halima mwenyewe alisimulia jinsi alivyokamatwa.
Zaidi ya hayo, upande wa mashtaka ulidai kuwa baada ya kukamatwa, mshtakiwa wa kwanza alionyesha nia yake ya kukiri kosa, hivyo Mei 31, 2023 alipelekwa kwa Hakimu wa Amani (PW4).
P4 alieleza kuwa Mbalu alikiri kumuua marehemu kwa madai kuwa alikuwa na tabia mbaya ya kufanya mapenzi na bintiye (Halima) ambapo alitoa maelezo hayo ya ziada yaliyopokelewa mahakamani kama kielelezo cha pili.
Katika ushahidi wake, Mbalu alikana kuhusika na mauaji ya marehemu na kuwa alikamatwa Mei 25, 2023.
Alieleza alipokamatwa, aliteswa na kulazimishwa kukiri kosa lakini alikataa kufanya hivyo na kuwa alipofika mbele ya PW4, hakutoa maelezo bali alipewa karatasi asaini na kuwa alitii na kuweka alama ya kidole gumba.
Kwa upande wake Halima, alieleza kuwa alikamatwa pamoja na mama yake (Tatu) ambaye aliachiliwa baadaye na kuwa mama yake aliolewa na Sambu baada ya kuachana na baba yake mzazi (marehemu).
Halima aliieleza Mahakama kuwa sababu kubwa iliyomfanya amkimbie baba yake (marehemu) ni kwamba marehemu alikuwa akifanya naye mapenzi kwa nguvu na matokeo yake alipata ujauzito na kujifungua mtoto (ambaye baba yake ni Shabani).
Washitakiwa wote wawili waliiomba Mahakama kuwaachia huru.
Uamuzi wa Jaji
Baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili Jaji Mbagwa amesema uamuzi wa Mahakama ni kama upande wa mashtaka umethibitisha pasipo kuacha shaka kuwa marehemu aliuawa na washtakiwa.
Jaji huyo amesema ametathmini ushahidi huo kwa ujumla na kuwa hakuna shahidi wa upande wa mashtaka hata mmoja aliyeshuhudia watuhumiwa wakila njama ya kumuua marehemu.
Amesema ushahidi pekee ambao angalau unawahusisha washtakiwa ni maelezo ya ziada ya Mbalu ambapo katika maelezo hayo, inadaiwa washitakiwa hao walipanga njama za kumuua marehemu kwa madai kuwa Shabani aliwahi kufanya mapenzi na Halima (mshitakiwa wa pili).
Jaji amesema katika maelezo hayo, Mbalu alikula njama na Halima ili kuweka mtego, hivyo marehemu alivyoenda kufanya mapenzi na binti yake, Mbalu ambaye alikuwa amejificha na wenzake, walimshambulia Shabani.
“Kinyume chake, mshtakiwa wa kwanza katika utetezi wake, alikanusha taarifa hiyo ya ziada ya mahakama akisema kwamba hakuwahi kuitoa bali aliambiwa tu na PW4 aitie saini,” amesema.
Jaji amesema swali la kutafakari ni kama maelezo ya ziada ya ungamo kutoka kwa mshtakiwa wa kwanza yanaweza kuwatia hatiani washtakiwa hao.
“Kwa kweli yaliyomo ni duni sana ili kuwatia hatiani, haijafafanuliwa vya kutosha juu ya jinsi shambulio hilo lilitekelezwa, zadi ya hayo, ushahidi wa mashtaka ulikuwa kwamba marehemu alikuwa amekodi pikipiki lakini hakuna pikipiki hiyo iliyotajwa katika maelezo ya ziada ya mahakama,” amesema Jaji.
Jaji Mbagwa amesema shaka yake inachangiwa zaidi na kuwa PW3 alipata taarifa kuwa washtakiwa na wengine ambao bado wapo nje walihusika na kifo cha marehemu.
“Hata hivyo, mbali na maneno yake tu, hakuna chochote kilichofikishwa Mahakamani ili kuthibitisha tuhuma dhidi ya washtakiwa hao, pia ilidaiwa kulikuwa na mbao zilizotapakaa damu kukutwa kando ya mwili wa marehemu ila haikuletwa kama kielelezo,” amesema.
Jaji huyo alieleza ukosefu wa ushahidi wa mwenendo ambao ungeweza kuthibitisha maelezo hayo ya ungamo ya mshtakiwa huyo wa kwanza na ingawa maelezo hayo yalikubaliwa, ukosefu wa ushahidi ulipunguza uzito wake hivyo haustahili sifa yoyote.
Baada ya kupitia hoja za pande zote mbili Jaji alieleza kuwa upande wa mashataka umeshidnwa kuthibitisha kesi bila kuacha shaka yoyote, hivyo mahakama inawaona washtakiwa hawana hatia na kuwaachia huru.