
Geita. Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Geita imemuachia huru Mahele Petro (19), mkazi wa Nyamilembe wilayani Chato mkoani Geita baada ya kukiri kosa la kumuua baba yake kwa kumchoma mkuki shingoni bila kukusudia.
Hukumu imetolewa leo Septemba 24, 2024 na Jaji Athuman Matuma, aliyesema Mahakama inamuachia huru mshtakiwa kwa sharti la kutotenda kosa la jinai kwa miezi 12.
Akisoma hukumu, Jaji amesema mshtakiwa alimuua baba yake mzazi, Petro Lyamba mkazi wa Kalebezo kwa kumpiga kwa mkuki shingoni kutokana na hasira zilizosababishwa na mgogoro wa kifamilia.
Amesema kutokana na hoja zilizojengwa na wakili wa mshtakiwa, Erick Lutehanga kama shufwaa kwa ajili ya nafuu ya adhabu imetiliwa maanani. Pia, kosa hilo ni la kwanza kutendwa na mshtakiwa kama upande wa mashtaka ulivyoeleza.
“Kwa mazingira hayo mshtakiwa anastahili nafuu ya adhabu. Hata hivyo, tayari amekwishatumikia adhabu kimsingi kwa kukaa rumande kwa miaka mitatu na miezi saba. Maisha yake hayawezi kuwa mazuri kwa kiasi ambacho yangekuwa kama asingetenda kosa hili,” amesema.
“Amemuua baba yake hata kumrudisha nyumbani si jambo jepesi kwake, kwa sababu anahitajika bado kutengeneza maisha yake na familia yake kutengeneza mahusiano yaliyopotea kutokana na tukio hili,” amesema Jaji Matuma.
Kutokana na mazingira hayo Jaji amemuachia huru kwa sharti la kutotenda kosa kwa miezi 12 kuanzia sasa, kwa mujibu wa kifungu cha 38(1) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu sura ya 16 iliyorejelewa mwaka 2022.
Hata hivyo, amesema endapo atafanya kosa la jinai kwa kipindi hicho atakamatwa na kufikishwa mbele ya Mahakama ili kupewa adhabu nyingine kwa mujibu wa sheria.
Ilivyokuwa
Awali shauri hilo lilipoitwa mahakamani kwa ajili ya kusikilizwa, mshtakiwa alisomewa kosa la kuua kwa kukusudia kinyume cha kifungu cha 196 na 198 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.
Ilidaiwa Februari 11, 2021 huko Kayebezo wilayani Chato, mshtakiwa alimuua Petro Lyamba ambaye ni baba yake mzazi. Mshtakiwa alikiri kosa akidai aliua bila kukusudia.
Baada ya kukiri, Jaji Matuma alizihoji pande zote mbili zilizokubaliana na kukiri wa mshtakiwa, hivyo akaagiza asomewe kosa la kuua bila kukusudia.
Wakili wa upande wa Jamhuri, Kabula Benjamin alimsomea maelezo mashtaka akidai alitenda kosa hilo akiwa na umri wa miaka 16 akiwa mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Kalebezo.
Alidai mshtakiwa alitenda kosa la kuua bila kukusudia kinyume cha kifungu cha 195(1) na 198 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.
Alidai siku ya tukio Februari 11, asubuhi mama yake na mdogo wake walikwenda shambani, mshtakiwa akielekea shuleni alirudi nyumbani kukatokea ugomvi kati yake na baba yake.
Amedai mshtakiwa aliingia ndani akachukua mkuki na kumchoma baba yake.
Baada ya tukio alichukua simu ya baba yake na kuwapa ndugu taarifa.
Ripoti ya uchunguzi wa daktari ilieleza sababu za kifo cha marehemu ni kuvuja damu nyingi iliyosababishwa na jeraha alilopata shingoni.
Alidai Februari 15, 2021 mshtakiwa alikamatwa na kukiri kosa akiwa polisi.
Baada ya maelezo hayo, Jaji alimtia hatiani kwa kosa la kuua bila kukusudia.
Upande wa Jamhuri ulieleza hauna kumbukumbu za makosa ya nyuma dhidi ya mshtakiwa, pia uliikumbusha Mahakama kuwa wakati mshtakiwa akitenda kosa hilo alikuwa mtoto, hivyo kuiomba inapotoa adhabu izingatie Sheria ya Mtoto Sura namba 13 iliyorejelewa mwaka 2019.
Wakili wa utetezi, Erick Lutehanga akitoa maungamo amedai kosa la mshtakiwa ni la kwanza na lilitokea kwa bahati mbaya na alikuwa mtoto.
Amedai kwa mujibu wa kumbukumbu zilizopo mshtakiwa hakufanya maandalizi yoyote kwenye tukio, hata baada ya tukio alitoa taarifa kwa ndugu na alikiri polisi na mahakamani hali inayoonyesha ni mwaminifu na muadilifu.
Amedai kitendo cha mshtakiwa kukiri kosa kinaokoa gharama na muda, hivyo ameiomba Mahakama kuzingatia kuwa, mshtakiwa ni mtoto na tayari amekaa mahabusu kwa miaka mitatu na miezi saba.