
Katika miaka kumi iliyopita Tuzo ya Mchezaji Bora (MVP) wa Ligi Kuu Bara imekuwa na ushindani mkubwa huku wazawa wakichukua mara tano na wageni idadi kama hiyo.
Hiyo inaonyesha ni namna ambavyo kumekuwa na kazi kubwa ya kuiheshimisha nchi baina ya nyota wazawa na wa kigeni wanaokuja kucheza soka la kulipwa katika ardhi ya Tanzania.
Ujio wa nyota hao wa kigeni unawafanya wazawa kuwa na kazi ya ziada ya kufanya kuhakikisha wanaiwakilisha nchi vizuri, lakini kwa misimu mitatu iliyopita mambo yalikuwa magumu.
Tangu mara ya mwisho mshambuliaji mzawa, John Bocco kubeba tuzo hiyo akiwa anaitumikia Simba, upepo ukahamia kwa wageni ambao wamechukua mara tatu mfululizo huku wakiifukuzia ya nne ili kujibu mapigo kama ilivyokuwa kwa wazawa kuanzia msimu wa 2014/2015 hadi 2017/2018.
Katika kipindi hicho cha misimu minne, wazawa walitawala akianza kuchukua Simon Msuva (2014/2015), Juma Abdul (2015/2016), Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ (2016/2017) na John Bocco (2017/2018).
Utawala wa wazawa ukaja kuvunjwa na Meddie Kagere raia wa Rwanda aliyebeba tuzo hiyo msimu wa 2018/2019, kisha Mzambia Clatous Chama akaibeba msimu wa 2019/2020 kabla ya mzawa John Bocco kurudisha heshima nyumbani msimu wa 2020/2021.
Tangu hapo, wageni wamekuwa wababe wakichukua mara tatu akianza Mkongomani, Yannick Bangala (2021/2022), akafuatia Mkongomani mwingine Fiston Mayele (2022/2023), kisha msimu uliopita 2023/2024 ikienda Burkina Faso kwa Stephane Aziz Ki.
MSIMU HUU ITAKUWAJE?
Kwa sasa zikiwa zimesalia mechi saba hadi nane msimu kumalizika, bado kuna vita ya wazawa na wageni katika kuwania tuzo hiyo.
Kwa wazawa, Feisal Salum ‘Fei Toto’ anayecheza Azam na Clement Mzize wa Yanga, wanaonekana kuwa katika mbio hizo sambamba na Muivory Coast, Jean Charles Ahoua wa Simba, lakini pia Mzimbabwe, Prince Dube (Yanga), Aziz Ki raia wa Burkina Faso (Yanga) na Muivory Coast, Pacome Zouzoua (Yanga).
Namna ambavyo Fei Toto anafanya katika kuibeba Azam, inampa nafasi ya kuingia kuwania tuzo hiyo kwani hivi sasa amehusika kwenye jumla ya mabao 16 akiwa ndiye kinara wa asisti akiwa nazo 12 na kufunga mabao manne. Kwa upande wa Mzize, amefunga mabao 10 na asisti tatu, hivyo amehusika kwenye jumla ya mabao 13. Kwa nyota wazawa, wawili hao ndiyo waliohusika kwenye mabao mengi zaidi wakichuana na wageni.
Ukija kuangalia namba za Ahoua, amehusika kwenye mabao 18 kutokana na kufunga mabao 12 na asisti sita, anafuatia Dube aliyehusika kwenye mabao 17 akifunga 10 na asisti saba, pia ana hat trick moja.
Aziz Ki naye amehusika kwenye mabao 14, akifunga saba na asisti saba wakati Pacome akihusika kwenye mabao 13, amefunga saba na asisti sita.
Mbali na kuhusika kwenye mabao mengi, pia ishu ya kuzipambania timu kubeba ubingwa ni sehemu mojawapo inayomfanya mchezaji kuongeza sifa ya kumfanya kuwa mchezaji bora wa msimu kwani ukiangalia washindi waliopita asilimia kubwa walizipa timu zao ubingwa huku wakiwa na kiwango bora kasoro msimu wa 2016/2017, aliposhinda Tshabalala ubingwa walibeba Yanga.
Kigezo hicho kinaweza kumfanya Fei Toto kuwa na wakati mgumu zaidi kuwa MVP msimu huu endapo Azam ikishindwa kubeba ubingwa kwani hivi sasa timu hiyo inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo, lakini kama akiendelea kuwa bora inaweza kuwa tuzo yake kama ilivyokuwa kwa Tshabalala msimu wa 2016/2017.
WAZAWA WANAKWAMA WAPI?
Kocha Msaidizi wa Simba Queens, Mussa Hassan ‘Mgosi’ amesema Simba na Yanga zinawabeba wachezaji wa kigeni kuchukua Tuzo za Mchezaji Bora wa mwaka na si kwamba wazawa hawana uwezo.
“Wachezaji wazawa wanajua sio kwamba hawajitumi kinachotokea ni kwamba wageni wengi wanacheza timu zinazojiweza kuanzia kifedha na miundombinu, Simba, Yanga na Azam.
“Wachezaji wa timu nyingine mbali na Simba na Yanga wanapaswa kuonyesha ushindani na sio kukata tamaa, hata hivyo ligi bado inaendelea lolote linaweza kutokea na mzawa anaweza kuchukua tuzo hiyo.
Ukiangalia kila wakati mchezaji anayechukua tuzo hii ni yule ambaye anakuwa ameonyesha ubora wa juu kwa msimu husika na hivyo ili hata hawa wazawa watwae tuzo hiyo wanatakiwa kuwa bora kuanzia mwanzo hadi mwisho wa msimu,” amesema Mgosi.
Mshambuliaji wa zamani wa Yanga na Simba, Mohamed Hussein ‘Mmachinga’ amesema kinachowakwamisha wazawa ni bidii na muendelezo tu lakini wanajua.
“Sio kwamba wanakwama, hapana, lakini wanakosa muendelezo wa kile walichokifanya msimu uliopita, naweza kusema wanapaswa kuwa washindani ili kutetea nafasi zao.
“Ligi bado mbichi, kwa kile alichokifanya Feisal msimu uliopita kuleta ushindani na Aziz KI, naiona bato hiyo tena msimu huu, kikubwa awe na muendelezo tu kama atakuwa hivi hadi mwisho wa msimu atakuwa mshindani sahihi wa tuzo hiyo,” amesema Mmachinga aliyeweke rekodi ya kuwa mchezaji aliyefunga idadi kubwa ya mabao ndani ya msimu mmoja katika Ligi Kuu Tanzania Bara alipofanya hivyo mwaka 1999 alipofunga mabao 26. Rekodi hiyo hadi sasa haijafikiwa pamoja na kuwa na washambuliaji wengi kwenye ligi yetu kutoka kwenye mataifa mbalimbali yenye maendeleo ya hali ya juu kwenye soka.