Mtihani mgumu wa Lissu Chadema

Dar es Salaam. Uongozi mpya wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) chini ya mwenyekiti Tundu Lissu unakabiliwa na mtihani mzito wa kuwaunganisha wanachama wake wanaoendeleza minyukano ya chini kwa chini.

Lissu aliingia madarakani Januari 22, 2025 baada ya kumshinda Freeman Mbowe kwenye boksi la kura ambaye amekiongoza chama hicho kwa miaka 21 na kukiwezesha kuwa chama kikuu cha upinzani nchini.

Katika utawala wa Mbowe, amekifanya kuwa na mtandao nchi nzima wa viongozi. Ameihitimisha safari ya uongozi akiwaachia wito wa kutibu makovu yaliyotokana na uchaguzi huo. Hoja hiyo iliungwa mkono na Lissu ambaye naye alisema atalifanyia kazi.

Mkutano mkuu uliofanyikia ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam ulishuhudiwa mvutano mkubwa baina ya Mbowe na Lissu waliokuwa wakiwania nafasi moja ya uenyekiti. Mwisho, wajumbe wa mkutano huo wakaamua Mbowe akapumzike.

Licha ya Mbowe kukubali matokeo na kuahidi kutoa ushirikiano, lakini Lissu ana kazi kubwa ya kufanya ya kukirejesha chama hicho kwenye umoja tofauti na sasa ambapo maneno yanayoendelea ya kejeli na kutishiana kwa walioshindwa.

Katika makundi songozi ya WhatsApp, bado kuna minyukano ya hapa na pale. Upande uliokuwa ukimuunga mkono Mbowe unaonekana kutofurahia kuona uongozi mpya unaendelea kumbagaza Mbowe.

Kauli za viongozi na wanachama wanaomuunga mkono Lissu ambaye awali alikuwa makamu mwenyekiti Bara, zinazonekana kuwaumiza na maneno wanayoyaeleza, watakuwa si wanachama ama viongozi watakaopambana kama mwanzo.

Wanadai sasa watakuwa wakishiriki tu lakini unapofika wakati wa utekelezaji mathalani operesheni hawatajitoa kama awali. Lissu anahitaji kuunganisha makundi haya, ukizingatia tofauti ya kura baina yake na Mbowe zilikuwa 31.

Lissu alipata kura 513 sawa na asilimia 51.5, Mbowe akapata kura 482 sawa na asilimia 48.3 na Charles Odero kura moja sawa na asilimia 0.1. Jumla ya kura zilikuwa 999, kura tatu ziliharibika.

Hoja nyingine imetolewa na mmoja wa wanaomuunga mkono Lissu aliyesema kuna haja ya kutibu majeraha. Bila hivyo huku nje watu wanafikiri tuko salama lakini ukweli ni kwamba hali si nzuri. Bado upande wa mwenyekiti wanaonekana kama si kitu.

“Mimi namuunga mkono Lissu, lakini kwa matokeo yalivyo, ili aongoze vizuri anahitaji hata waliokuwa upande wa Mbowe washirikishwe, ukisema uwatenge kabisa, wanaweza kukususia chama, wakawa wanakuja kwenye vikao bora liende,” amesema na kuongeza:

“Yaani timu Mbowe imevunjika moyo, sasa kweli sisi timu Lissu tunaweza kutoboa? Haya sekretarieti inapaswa kuwa mchanganyiko, lakini akiweka wote wa upande wake si sawa. Atakuwa na kazi na hatutatoboa na kwambia mimi.”

Ametolea mfano Zanzibar ambapo CCM na CUF na sasa ACT Wazalendo wamekuwa wanaachana kura kidogo na ndio maana kuna serikali ya umoja wa kitaifa.  Kenya kipindi cha Uhuru Kenyatta na Raila Odinga. Kwa hiyo Lissu akubali akatae akitaka atawale vizuri timu Mbowe kwenye uongozi wake hauepukiki.

Sekretarieti ya Chadema inaundwa na kamati na mabaraza ngazi ya taifa la vijana (Bavicha), wazee (Bazecha) na wanawake (Bawacha) pamoja na kurugenzi tano ya fedha, uwekezaji na utawala, sheria na haki za binadamu na ya mawasiliano, itifaki na mambo ya Nje.

Kurugenzi zingine ni ya uchaguzi pamoja na ya mwisho ni tathmini na ufuatiliaji.

“Ukitaka tusonge mbele kiukweli tunahitajiana wote. Timu Lissu na Mbowe wanapaswa kufanya kazi kwa pamoja. Tukisema timu Lissu pekee ndiyo ishike kila kitu je, hili kundi la Mbowe likiamua kukaa pembeni Chadema itasogea kweli? Inahitajika tathimini kubwa,” anasema mzee mwandamizi wa Chadema.

‘Lissu, Mbowe wanategemeana’

Hoja hiyo ilizungumzwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Wazee Wastaafu wa chama hicho, Profesa Raymond Mosha mara baada ya kutangaza matokeo hayo akisema miamba hiyo ya siasa inapaswa kushirikiana.

“Katika uchaguzi huu, tumeshuhudia jambo moja ambalo kutokana na uzoefu wangu katika nchi kadhaa duniani, ambako alikaa miaka 20 na zaidi Marekani kama mhadhiri wa maadili na falsafa, ameshuhudia chaguzi za nchi ambazo demokrasia zao zimekomaa na kila wakati aliona katika chaguzi za demokrasia safi matokeo ya wanaogombea mara nyingi hayatofautiana sana.

“Kwa sababu utakuta wagombea ni watu wenye nguvu kubwa hivyo utakuta tofauti ni ndogo mfano katika matokeo ya leo (Januari 22), kati ya hao wawili (Mbowe na Lissu) tofauti ni kura 31 tu. Hiyo inaonyesha hawa ni viongozi mahiri, viongozi wenye nguvu.

Kwa sababu wote wana nguvu ndio pale kaulimbiu yetu inaposema Stronger Together. Kwa sababu kama watu wawili wana nguvu kubwa kila mmoja anamhitaji mwingine, mmoja hawezi kusimama peke yake,” alisema Profesa Mosha.

Wajumbe wengine wa kamati hiyo walikuwa, Ahmed Rashid, Alfred Kinyondo, Wakili Edson Mbogoro, Francis Mushi, Lumuli Kasyupa, Ruth Mollel na Dk Azaveli Lwaitama aliyekuwa katibu.

Hoja nyingine ambayo utawala wa Lissu unapaswa kuiangalia ni iwapo utaiweka kando kabisa kambi ya Mbowe, jambo litakalouyumbisha utawala wake wakati wa kufanya uamuzi.

Mathalan, kamati kuu kwa sasa ina wajumbe 24 kwa maana ya viongozi wakuu wa kitaifa, wenyeviti tisa wa kanda, wenyeviti watatu wa mabaraza, wateule wa mwenyekiti watano na Mbowe mwenyewe ambaye ni mjumbe wa kudumu wa kamati kuu wale wa kambi ya Mbowe wasipokwenda kwa sababu mbalimbali, akidi haitotimia.

Vivyo hivyo kwenda Baraza kuu na au mkutano mkuu. Hivyo Lissu na viongozi wenzake wanapaswa kufuata au kuzingatia ushauri wa Profesa Mosha ambaye alisema amekuwa Chadema kwa miaka 32 tangu inaanzishwa.

Alichokisema Devotha, Wenje

Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kati, Devotha Minja ambaye kwenye uchaguzi huo alikuwa akimuunga mkono Mbowe amesema katika kipindi ambacho uchaguzi wa chama hicho umekwisha, ni muhimu chama kirejee jukumu lake la mapambano dhidi ya CCM.

Ameeleza atashangaa na halitakuwa jambo jema, iwapo uongozi mpya utajikita katika fikra za kuwabagua baadhi ya wanachama kwa sababu tu walikuwa wanamuunga mkono kiongozi aliyestaafu.

“Sitarajii kama kuna makundi yanayolenga kubagua watu, utakuwa uongozi wa ajabu kwa sabahu mapambano yetu siku zote ni dhidi ya CCM na sio ndani ya chama,” alisema Devotha.

Hata hivyo, alieleza amesikiliza hotuba za Mbowe na mwenyekiti mpya, Lissu zote zimejikita kwenye mtazamo wa kujenga umoja na kuvunja makundi yaliyosababishwa na uchaguzi.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa chama hicho Kanda ya Victoria, Ezekia Wenje ambaye alikuwa akigombea umakamu mwenyekiti bara akimuunga mkono Mbowe na kabla ya uchaguzi kulikuwa na shtuma baina yake na Lissu za rushwa amesema baada ya uchaguzi aliahidi kutoa ushirikiano kwa uongozi uliopo madarakani.

Kwa sababu mambo ya uchaguzi yamepita, amesema ni muhimu kwa pande zote kati ya walioshinda na walioshindwa, waendeleze umoja, kwa maslahi ya Chadema.

Hata hivyo, Wenje amesema katika utaratibu wa uchaguzi walioshinda ndio huwa na jukumu la kuwafikia walioshindana nao ili wazungumze kama kuna shida yoyote yaishe na wasonge mbele.

“Mara nyingi katika ushindani wa kistaarabu walioshinda huwa na jukumu la kuwafikia walioshindwa ili kumaliza mambo yote ya ushindani na kutengeneza umoja na ndilo jukumu ambalo uongozi mpya unalo sasa,” amesema.