
Nairobi. Mtifuano wa Rais William Ruto na aliyekuwa Naibu Rais, Rigathi Gachagua, ni kama umeanza upya baada ya kiongozi huyo wa nchi kutoa tuhuma nyingine dhidi ya Gachagua, ikiwamo madai ya malipo ya Sh10 bilioni.
Gachagua, ambaye Oktoba mwaka jana aliondolewa na Bunge la Seneti kwenye nafasi ya Naibu Rais kutokana na tuhuma za ufisadi na matumizi mabaya ya mamlaka, jana, Aprili mosi, 2025 ni kama Rais Ruto ameliamsha tena baada ya kutoa tuhuma nyingine mpya, ikiwamo kutokuelewana na viongozi wenzake serikalini na baadhi ya wabunge wa Mlima Kenya.
Mbali na tuhuma za Rais Ruto, Gachagua amemjibu kiongozi huyo kwa maelezo kwamba amesema uongo na ni hatari kwa kiongozi wa nchi kusema uongo.
Rais Ruto, ambaye alikuwa ziarani kwenye eneo la Mlima Kenya jana, alifanya mahojiano na vyombo vya habari na ameeleza namna alivyomteua Gachagua kuwa mgombea mwenza wa urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.
Pia, amesema Gachagua alidai malipo ya Sh10 bilioni ili kusaidia kushawishi wapigakura katika eneo la Mlima Kenya kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2027 ili kumsaidia Ruto kurejea madarakani.
Vilevile, Rais Ruto amedai kuwa alimuokoa Gachagua mara mbili kutoka katika njama za wabunge waliokuwa wakijaribu kumuondoa kwenye nafasi ya Naibu Rais kutokana na tabia yake ya kuhusika katika mivutano na baadhi ya wabunge. Hata hivyo, katika jaribio la tatu, Ruto aliamua kuwa ni bora Gachagua aondolewe kwenye nafasi hiyo.
Kauli ya Ruto imejibiwa na Gachagua, ambaye amekanusha madai kwamba alikuwa akizozana na wabunge wa eneo hilo na kuwatisha alipokuwa ofisini, akitaja kauli za kiongozi wa nchi kama uongo.
Pia, amemshutumu Ruto kwa kusambaza habari za kupotosha na kuwadanganya Wakenya, akionya kwamba uongo ndani ya uongozi unaharibu imani ya umma na kudhoofisha maendeleo ya taifa.
Kwa mujibu wa Ruto, alimteua Gachagua kuwa mgombea mwenza kwa sababu aliona alikuwa na umri mkubwa na uzoefu wa kisiasa, lakini pia alimtambua kama mtu mwenye nguvu kisiasa ambaye angesaidia kuleta ushawishi kwa jamii ya Mlima Kenya.
Kwenye kura za maoni za kumpata mgombea mwenza wa urais, Gachagua alipata kura tano, huku Profesa Kithure Kindiki akipata kura 27.
Rais Ruto amesema alifanya hivyo kwa lengo la kumsaidia Gachagua, ambaye alikuwa na ushawishi mdogo wa kisiasa katika eneo lake.
Amesema baada ya kushinda uchaguzi na kuingia Ikulu, Gachagua alianza kujionyesha kama mtu msumbufu, akilalamikia mara kwa mara kuhusu masuala ya serikalini na kudai uwa alikuwa akihujumiwa na viongozi fulani serikalini.
Ruto ameeleza kuwa Gachagua alikosa kutulia na badala yake akaanza kutafuta sababu za kumshinikiza yeye mwenyewe ili kujipatia ushawishi zaidi ndani ya Serikali.
Katika mahojiano hayo, Rais Ruto amezungumzia kwa undani suala lililojitokeza katika kipindi cha uongozi wa Serikali yao, ambapo Gachagua alidai Sh10 bilioni kutoka kwa Rais Ruto kama shinikizo la kushawishi wapigakura wa Mlima Kenya ili kumsaidia kupata ushindi katika uchaguzi wa 2027.
Rais Ruto amesema alikataa ombi la fedha hizo kwa kuwa aliona suala hilo lilikuwa vitisho vya kisiasa na njama za kumshinikiza kuingia kwenye mikataba ambayo ilikuwa na madhara kwa Serikali.
Amesema Gachagua alikuwa akilalamikia mara kwa mara baadhi ya wabunge wa Mlima Kenya, akiwemo Ndindi Nyoro na baadhi ya wabunge wa wanawake, na kusema alikosa uwezo wa kuungana na viongozi hao ili kuwa na ushawishi katika eneo hilo.
Rais Ruto amekumbusha kwamba alikubaliana na uamuzi wa kumtimua Gachagua kutoka katika nafasi ya Naibu Rais, lakini alionekana kutokuwa na mamlaka ya kuzuia hatua hiyo kwani ilifanyika kwa mujibu wa katiba ya nchi.
Oktoba mwaka jana, Bunge la Seneti lilipiga kura ya kumuondoa Gachagua kwenye wadhifa wa Naibu Rais baada ya kukutwa na hatia kwenye mashtaka matano kati ya 11 aliyoshtakiwa nayo.
Gachagua ampinga Rais Ruto
Jana, Aprili mosi, 2025 Gachagua amejibu kwa kupinga kauli ya Rais Ruto kuwa alidai Sh10 bilioni kama ilivyodaiwa na Rais. Kupitia mtandao wa kijamii wa X, Gachagua amejibu kwa kusema tuhuma hizo hazikuwa za kweli.
Gachagua amedai tabia ya Rais Ruto kusema uongo kwa makusudi ni tishio kwa taifa, akionya kuwa viongozi wanaosema uongo waziwazi wanadhihirisha udhaifu wa uongozi wao na wanaharibu imani ya wananchi kwa serikali zao.
Kwa mujibu wa Gachagua, uongo unaharibu mustakabali wa taifa na kwamba viongozi wanapaswa kuwa na ujasiri wa kusema ukweli ili kujenga imani na ushawishi kwa wananchi.
Amesema kuwa inashangaza kuona Rais Ruto akifanya mashambulizi ya kisiasa kwa kusema uongo bila kujutia, na kwamba tabia hiyo ni tishio kubwa kwa maendeleo ya nchi.
Gachagua amekosoa jinsi Rais Ruto alivyokosa kuungana na viongozi wenzake, badala yake akajikita katika kuzungumza uongo ili kuwachafua watu na kujinufaisha kisiasa.
Katika maoni yake, Gachagua amesema kuwa wakati mwingine ni bora kuwa kimya kuliko kusema uongo.
Amesema kuwa uongo uliojaa katika siasa za Kenya unadhihirisha udhaifu wa viongozi wanaoishi katika muktadha wa kukosa kusema ukweli kwa umma.
Gachagua amesema kuwa kama viongozi wangeweza kutoa ukweli, taifa lingekuwa na matumaini na maendeleo endelevu.
Amesisitiza, “Nalilia nchi yangu, Kenya,” akionyesha jinsi alivyohuzunishwa na hali ya siasa inayochochea mgawanyiko na kutokuaminiana kati ya viongozi wa Serikali.
Sababu zilizomuondoa Gachagua
Oktoba 2024, maseneta wa Kenya walipiga kura ya kumuondoa Gachagua ofisini, licha ya yeye kutokuwepo katika bunge hilo.
Gachagua aliugua ghafla na kulazwa hospitalini jijini Nairobi, lakini licha ya hali yake, Bunge liliendelea na mchakato wa kumuondoa ofisini.
Kiongozi huyo alikuwa akikabiliwa na mashtaka 11, lakini mashtaka matano ndiyo yalithibitika na kutiwa hatiani.
Miongoni mwa mashtaka yaliyomtia hatiani ni kukiuka Katiba ya nchi, ikiwamo kutishia majaji na kufanya siasa za migawanyiko ya kikabila, lakini akafutiwa mashtaka mengine, yakiwemo ufisadi na utakatishaji fedha.
Pia, alituhumiwa kuitisha mkutano na waandishi wa habari mjini Mombasa na kumshutumu Mkurugenzi Mkuu wa Huduma ya Kitaifa ya Ujasusi (NIS), Noordin Haji, kwa kushindwa kumshauri ipasavyo Rais Ruto kuhusu Mswada wa Fedha wa 2024, ambao ulisababisha machafuko na upotevu wa maisha jijini Nairobi na maeneo mengine ya nchi.
Pia, alituhumiwa kumshambulia Jaji wa Mahakama ya Juu, Esther Maina, kuhusiana na kesi ya ufisadi wa Sh200 milioni iliyokuwa ikimkabili Gachagua kabla ya kampeni za uchaguzi mkuu wa 2022.
Katika uamuzi wake, Jaji aliamua kwamba Gachagua alipaswa kuziachia serikali fedha hizo, ambazo alidaiwa kuzipata kwa njia ya ufisadi.
Gachagua, kwa kutoridhika na hukumu hiyo, alinukuliwa akitamka hadharani kwamba atawasilisha ombi lake binafsi mbele ya Jaji Mkuu, Martha Koome, kumpinga Jaji huyo ili aondolewe katika idara hiyo ya mahakama kwa madai ya utovu wa nidhamu na ufisadi.
Pia, Gachagua alituhumiwa kukiuka sheria ya uwiano na uadilifu wa kitaifa, ambayo inasema ni kinyume cha sheria kwa mtu yeyote kutumia matamshi ya vitisho na unyanyasaji, kuonesha tabia kama hiyo, kutamka maneno yanayoweza kuzua hofu miongoni mwa makabila, au kusababisha uadui na ubaguzi.
Sheria hiyo ilionekana kumbana Gachagua, ambaye matamshi yake ya mara kwa mara yenye chuki hadharani katika kipindi cha miaka miwili aliyokaa madarakani yalimfanya aonekane kama mkosaji chini ya sheria hiyo.
Imeandikwa na Noor Shija kwa msaada wa mtandao.