Mtifuano mpya Ma-RC waongeza joto majimboni

Dar es Salaam.  Unakumbuka Machi 11, 2025, Rais Samia Suluhu Hassan alipoagiza wateule wake, wakiwemo wakuu wa mikoa wenye nia ya kugombea nafasi mbalimbali, kutoa taarifa mapema, ili nafasi zao ziweze kujazwa kwa wakati?

Sasa hali hiyo inajidhihirisha wazi, kwani baadhi ya viongozi hao, hasa wakuu wa mikoa, wanatajwa kuanza harakati za kuwania ubunge katika majimbo mbalimbali Tanzania Bara na Zanzibar.

Hekaheka hizo zinakuja ikiwa imebaki miezi michache kabla ya kuanza kwa michakato ya uteuzi wa wagombea ubunge na udiwani ndani ya vyama vya siasa, kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa baadaye mwaka huu.

Baadhi ya wakuu hao wa mikoa wanaotajwa kujipitisha na kujiandaa kisiasa, pia wameshaanza kuomba kuungwa mkono na mamlaka zenye ushawishi kwenye uteuzi ili waweze kupeperusha bendera ya CCM kwa nafasi hizo za ubunge.

Hili limeelezwa na mmoja wa wajumbe wa sekretarieti ya CCM Taifa (jina lake limehifadhiwa), ambaye amesema wakuu wa mikoa ni miongoni mwa makundi yanayoonyesha nia ya kuutaka ubunge katika uchaguzi huo baadaye mwaka huu.

Kwa mujibu wa mjumbe huyo, tayari kuna wakuu wa mikoa zaidi ya watano wameonyesha nia kisirisiri ya kuutaka ubunge katika majimbo mbalimbali Tanzania Bara na Zanzibar.

“Ninavyokwambia hawa ni walionifuata kuniomba niwaunge mkono, kuna wale ambao hawakunifuata wamewafuata wengine. Hapa nimepokea mialiko mingi kutoka kwao lakini vikao ndivyo vitakavyoamua sina nguvu wala uamuzi wowote kuhusu nia zao,” amesema.

Hata hivyo, Rais Samia alishatoa mwelekeo kuhusu wateule wake wote wenye nia ya kwenda majimboni, akiwasisitiza watoe taarifa mapema ili kwenye nafasi watakazoacha wapatikane warithi.

Akiwa katika mkutano wa 39 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) jijini Dodoma, Machi 11, mwaka huu, mkuu huyo wa nchi alisema, “yeyote mwenye nia ya kugombea atwambie mapema, ili tumpandishe wa chini yake ashike ile nafasi.

“Ukitwambia mapema, umekwenda kujaribu, umeshindwa na wewe ni mzuri, tutakufikiria kurudi; hukutwambia mapema, umekosa yote ndugu yangu, kwa hiyo kajipimeni, sitaki kuwaficha kajipimeni,” alionya.

Makonda na Gambo

Hivi karibuni katika Mkoa wa Arusha, mkuu wa mkoa huo, Paul Makonda alihusishwa na ubunge katika Jimbo la Arusha Mjini, baada ya madiwani kadhaa wa Jiji hilo kutoa matamshi yanayoashiria kumtaka agombee nafasi hiyo.

Hata hivyo, Mbunge wa sasa wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo alitafsiri kitendo hicho cha madiwani kama njama za Makonda mwenyewe kuonyesha nia ya ubunge, huku akimtaka afuate kanuni na taratibu za CCM kuingia kwenye kinyang’anyiro hicho.

Gambo aliweka bayana kwamba, hamwogopi Makonda kuwa mshindani wake katika ubunge wa Arusha Mjini, isipokuwa anakasirishwa na mbinu aliyoitumia na kuwaandaa madiwani waonekane kama wanamuhitaji.

Licha ya maelezo ya Gambo na kauli ya madiwani kumtaka agombee ubunge wa jimbo hilo, Makonda hakuwahi kueleza lolote iwapo ana mpango wa kugombea jimbo hilo au la.

Hali ikiwa hivyo mkoani Arusha, Jimbo la Makambako mkoani Njombe ni patashika nguo kuchanika, akitajwa mmoja wa wakuu wa mikoa, anayetarajiwa kuleta upinzani kwa mbunge wa sasa, Deo Sanga.

Mbali na ukuu wa mkoa, kiongozi huyo anayetajwa kuutaka ubunge wa Makambako, anabebwa na ushawishi alionao ndani ya ya CCM, kwa kuwa amewahi kushika wadhifa mkubwa.

Nguvu ndani ya chama ni jambo moja, lakini maandalizi ya anayodaiwa kuyafanya kulinyaka jimbo hilo ni jambo lingine linalotajwa kutishia hatima ya Sanga kutetea nafasi yake kwenye uchaguzi wa baadaye mwaka huu.

Mkuu huyo wa mkoa ni miongoni mwa wanaotajwa wataaga kwenda jimboni mapema mwaka huu, mara tu CCM itakapopuliza kipyenga cha mchakato wa ndani wa kupitia wagombea.

Lakini pia inaelezwa hekaheka kama hizo zimetawala hata katika majimbo ya Kalenga, Mufindi Kaskazini, Mafinga, Wanging’ombe na Kilolo mkoani Iringa.

Jimbo la Namtumbo ni uwanja mwingine utakaotimka vumbi katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, kwa nafasi ya ubunge kwa kuwa, ndiko anakoelekeza nguvu mmoja wa wakuu wa mikoa ya kusini nchini.

Hatima ya mbunge wa sasa wa jimbo hilo, Vita Kawawa iko kwenye hatihati katika kutetea nafasi yake, kutokana na nguvu ya ushawishi aliyonayo mkuu huyo wa mkoa.

Ukiachana na uzoefu wake katika nafasi hiyo, pia mkuu wa mkoa anayetajwa amewahi kuwa mkuu wa wilaya kadhaa na anabebwa na historia ya kuwa sehemu ya maofisa kwenye idara za CCM makao makuu.

Mkuu huyo wa mkoa ameshuhudiwa mara kadhaa akifanya ziara za kimyakimya na kufadhili shughuli na huduma mbalimbali, ikiwemo za chama na michezo kwa vijana.

Pia, kiongozi huyo anatajwa kuwa karibu zaidi na viongozi wa CCM wa Mkoa wa Ruvuma, muda mwingi anapotembelea jimbo hilo.

Stanslaus Mabula anayeliongoza Jimbo la Nyamagana katika nafasi ya ubunge, pia anatajwa kwamba atakabiliwa na upinzani kutoka kwa mmoja wa wajumbe wa sekretarieti ya CCM, mwenye wasifu mrefu ndani ya chama.

Lakini mjumbe huyo, ana uzoefu mkubwa pia, hata katika nafasi mbalimbali alizowahi kushika ikiwamo ya ukuu wa mikoa na wilaya kadhaa nchini.

Vyanzo vya taarifa hizo vimesema hakuna shughuli ya chama itakayofanyika katika eneo hilo mkuu wa mkoa huyo ambaye pia kwa sasa hatutamtaja, akaacha kushiriki.

Si hivyo tu, pia anatajwa kuwa miongoni mwa wachangiaji wakubwa wa ujenzi wa ofisi mbalimbali za CCM ngazi za chini, kadhalika ananunua vitendea kazi kwa ajili ya viongozi wa chama matawi, kata na wilaya.

Kwa nini wakimbilie ubunge?

Akizungumzia hilo, Mchambuzi wa Masuala ya Siasa, Ali Makame amesema wateule wengi wanaukimbilia ubunge kwa kuwa ni nafasi inayowapa hakikisho la kubaki madarakani kwa muda stahiki.

Amesema fursa hiyo ni tofauti na nafasi za uteuzi, ikiwemo mkuu wa mkoa ambayo mamlaka ya uteuzi ndio inayokuwa na uamuzi wa lini wadhifa wako ukome au uendelee.

“Ndio maana unaona wakuu wa mikoa wanatafuta ubunge, wanatafuta nafasi watakazokuwa na uhakika wa kudumu. Ubunge kwa miaka mitano anajua ana uhakika wa kuongoza kwa muda huo,” amesema.

Sababu nyingine, ameeleza ni uwezekano wa kuukwaa uwaziri unapokuwa mbunge, nafasi hito inawashawishi wengi kuitaka na kuacha nyingine walizonazo.

“Mtu anaona akiwa mbunge kuna uwezekano akateuliwa kuwa waziri na hata akiondolewa kwenye uwaziri anabaki kuwa mbunge,” amesema.

“Sidhani kama ni jambo baya, inaonyesha ukomavu wa demokrasia, watu wanapata uhuru wa kuchagua na kuwania nafasi mbalimbali kwa hiari yao bila kubaguliwa,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *