Mtifuano mabasi ya Ngorika, Jaji ashusha rungu

Moshi. Kwa waliokuwa wakisafiri kwa mabasi ya Ngorika kutoka Moshi hadi Dar es Salaam miaka ya 90, wanaweza kuwa na swali, ni wapi mabasi hayo yapo? Jibu ni kuwa, kulikuwa na mtifuano wa wanafamilia mahakamani.

Miaka ya 1990 hadi 2000 mabasi ya Ngorika yalitoa ushindani kibiashara katika njia hiyo lakini yalipotea barabarani.

Jaji Safina Simfukwe wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Moshi, ametoa hukumu ya kesi ya madai namba 2 ya mwaka 2022 kati ya kampuni ya Ngorika dhidi ya Kapesa Mberesero anayejulikana pia kwa jina la Patrick Mberesero. Amekataa ombi la kampuni kukabidhiwa mabasi 10.

Katika madai yake, kampuni hiyo iliomba mahakama imuamuru mdaiwa Kapesa kukabidhi mabasi 10 ya kampuni hiyo, eneo la maegesho lililopo Moshi, gari aina ya Toyota Land Cruiser, pikipiki na mali nyingine zikiwa katika hali nzuri.

Kama hilo lisingewezekana, kampuni iliomba mahakama imlazimishe Kapesa kulipa Sh1.27 bilioni ambazo ni sawa na thamani ya mali hizo na kuwasilisha faida halisi iliyotokana na biashara ya mabasi kati ya Desemba 2015 hadi Januari 2022.

Mbali na amri hizo, kampuni iliiomba mahakama imuamuru mdaiwa kulipa Sh750 milioni kama mazao yaliyotokana na biashara ya mabasi hayo ambayo haikuwasilishwa kwenye kampuni na fidia ya Sh500 milioni.

Katika hati ya madai, mdai alieleza kampuni ilianzishwa miaka ya 90 na Benedict Mberesero au Alli Mberesero na watoto wake Stanley na Stephen. Benedict aliiendesha hadi alipofariki dunia 1997.

Inadaiwa baada ya kifo cha muasisi wa kampuni hiyo, familia ilikubaliana baadhi ya wanafamilia wangeendesha na kusimamia mali za kampuni, yakiwamo mabasi hayo kupitia mfuko wa wakfu kwa manufaa ya kampuni.

Ilielezwa kortini kuwa mdaiwa (Kapesa) aliteuliwa kuwa meneja wa kampuni akiaminiwa kusimamia mali hizo kwa masharti ya kuwasilisha hesabu za kila mwaka lakini alishindwa kufanya hivyo.

Mali ambazo kampuni iliziorodhesha ni mabasi 10, eneo la maegesho, gari aina ya Toyola Land Cruiser, pikipiki na lori moja.

Msingi wa shauri hilo ni madai ya kuwepo matumizi mabaya ya mali hizo, kusitisha biashara ya mabasi, kuyatelekeza eneo la maegesho lililopo kwenye yadi ya mdaiwa na kushindwa kuwasilisha hesabu za fedha.

Majibu ya mdaiwa

Mdaiwa katika majibu ya shauri hilo alikiri mdai ni kampuni iliyosajiliwa na Alli Mberesero aliyefariki dunia mwaka 1997, akiwa ndiye mwenye hisa nyingi katika kampuni iliyokuwa na mabasi na malori ya mizigo.

Alidai baada ya kifo cha Alli Mberesero, hakuna uhamishaji rasmi wa hisa uliofanyika au kuteuliwa wakurugenzi kulikofanywa hadi mwaka 2020 ambao watu waliotajwa Sabas na Chivawe walipofanya mabadiliko.

Kuhusu umiliki wa mabasi yanayobishaniwa, alidai awali yalikuwa yakimilikiwa na kampuni ya Ngorika lakini iliacha kufanya kazi kutokana na zuio la Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara.

Ni kutokana na zuio hilo, mdaiwa alieleza mabasi hayo yalisitisha biashara na kuegeshwa. Alidai aliondolewa katika safu ya uongozi mwaka 2017 na suala la hisa na kuteuliwa kwa wakurugenzi wapya halikufanyika.

Mdai akaiomba mahakama itamke kusitishwa kwake kuwa mkurugenzi wa kampuni kulikuwa batili na mahakama itamke uteuzi wa wakurugenzi wapya na katibu kulifanyika kwa ulaghai, hivyo ni batili.

Pia akaiomba mahakama itamke uhamishaji wowote wa hisa ni batili, kuondolewa kwake kama mmoja wa watia saini wa kampuni kulikuwa batili na kulifanyika kwa ulaghai, alipwe fidia ambayo mahakama itaamua na gharama za kesi.

Hukumu ya jaji

Katika hukumu aliyoitoa Machi 24, 2025 Jaji Simfukwe amesema mahakama inawajibika kujibu swali, kama kampuni iliendelea kufanya biashara baada ya kifo cha muasisi wake, Alli Mberesero na mkurugenzi, Stephen Mberesero.

Jaji amesema katika ushahidi, shahidi wa kwanza wa kampuni, Shaban Mberesero alieleza baada ya kifo cha Stephen mwaka 2016, kampuni iliendelea kufanya biashara chini ya uangalizi wa mdaiwa.

Hata hivyo, mdaiwa katika majibu alieleza kampuni ilikoma kufanya biashara baada ya kifo cha Stephen mwaka 2016 na kwamba, kuna kesi ilifunguliwa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Biashara kuhusu mgogoro huo.

Jaji amesema kwa mujibu wa mdaiwa (Kapesa), alisimamia shughuli za mabasi ya Ngorika kipindi cha nyuma, lakini baada ya amri ya Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara jijini Dar es Salaam, mabasi hayo yaliachwa bila msimamizi.

Kwa mujibu wa jaji, hukumu ya Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara iliibua hoja za msingi kuwa ni pamoja na kampuni kukosa uelekeo baada ya kifo cha mkurugenzi wa mwisho wa kampuni hiyo, Stephen Mberesero mwaka 2016.

Simfukwe amesema Jaji Amir Mruma aliyeamua kesi hiyo, alieleza katika hukumu kuwa tangu kifo cha Alli mwaka 1997 na Stephen mwaka 2016, kampuni hiyo ilikuwa inafanya shughuli zake kinyume cha matakwa ya sheria.

Alibainisha ukiukwaji huo wa kisheria ni katika kuongeza kiwango cha hisa za kampuni, kutozingatia masharti kulingana na Sheria ya Kampuni ya mwaka 1997 na kampuni kuwa na mkurugenzi mmoja kinyume cha sheria.

Jaji Simfukwe amesema kwa kuwa mahakama hiyo ambayo ndiyo yenye mamlaka ya kusikiliza migogoro ya kibiashara ilishaamua kuwa kampuni hiyo ilikuwa kinyume cha sheria baada ya vifo vya wakurugenzi, hawezi kuitolea uamuzi tena.

Amesema wadai wanaweza kusema walalamikaji ni tofauti na kesi iliyokuwa katika Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara, ni ushahidi ulio wazi kuwa kampuni iliyojieleza katika mahakama hiyo ni hiyohiyo mbele ya Jaji Simfukwe.

Amesema hoja kuwa wakurugenzi wapya ambao wametajwa kuwa Mariam Simbano, Lilian Mberesero, Charles Mberesero na Chavawe Mberesero waliteuliwa kusimamia kampuni hiyo ya mabasi ya Ngorika ni upotoshaji.

Kwa mujibu wa Jaji Simfukwe, wakurugenzi wapya waliteuliwa mwaka 2020 baada ya hukumu ya Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara kutolewa mwaka 2019 na ni baada ya mdaiwa kuwa ameshaondolewa mwaka 2017.

Amesema inaonekana kesi ya sasa ilifunguliwa na kampuni baada ya hukumu ya Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara iliyosema kampuni ilikuwa ikijiendesha kinyume cha sheria na kutaka kuhamishia mzigo huo kwa mdaiwa.

Kuhusu hoja ya kama mdaiwa alikuwa ni mwajiriwa wa mdai, jaji amesema kulingana na ushahidi uliopo, hoja hiyo haibishaniwi kwa kuwa pande mbili zilikuwa katika makubaliano ya kufanya kazi kama kondakta na meneja.

Kuhusu hoja iwapo mdai anashikilia mali zozote za kampuni, jaji amesema mahakama haiwezi kuiamua kwa kuwa tayari ilishaamuliwa na Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara katika hukumu ya mwaka 2019.

“Hata malalamiko kuwa mdaiwa alikusanya mtaji ili kuanzia kampuni ya mabasi ya Kaprikon ni kama imepotea njia kwa sababu mdai alishindwa kuthibitisha kama mdaiwa anashikilia mali za mdai wa shauri hili,” amesema.

Kutokana na sababu hizo, Jaji Simfukwe ameitupilia mbali kesi hiyo iliyofunguliwa na kampuni ya Ngorika Bus Transport Company Limited.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *