Mtibwa yaipa mkono Geita Gold ikijisogeza Ligi Kuu

Mtibwa Sugar imejiweka katika mazingira mazuri ya kupanda Ligi Kuu msimu ujao baada ya leo kuibuka na ushindi mnono wa mabao 5-0 dhidi ya Geita Gold kwenye Uwanja wa Manungu, Morogoro.

 Ushindi huo mnono umeifanya Mtibwa Sugar kufikisha pointi 51 ambazo ni sita zaidi ya pointi za Geita Gold iliyo katika nafasi ya pili na nane zaidi ya za Mbeya City iliyo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi hiyo.

Mabao ya Mtibwa Sugar leo yamefungwa na

Fredrick Magata aliyefunga mawili na mengine yamepachikwa na Marungu Omary Juma Nyangi na Twalib Mhenga.

Mbali na kuipatia pointi tatu muhimu, matokeo hayo yameifanya pia Mtibwa Sugar kulipa kisasi cha kipigo cha bao 1-0 ambacho ilikipata katika mzunguko wa kwanza timu hizo zilipokutana huko Geita.

Katika Uwanja wa Ilulu, Lindi, wenyeji Bigman waliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Biashara United wakati huo Transit Camp ikipoteza nyumbani mbele ya Green Warriors.

Mbuni ilipoteza kwa mabao 3-1 mbele ya Mbeya City na Kiluvya United ilipata ushindi wa bao 1-0 ugenini dhidi ya Cosmopolitan.

Kwa mujibu wa kanuni za Ligi ya Championship, timu mbili ambazo zitamaliza zikiwa kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo zitakata tiketi ya kushiriki Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.