Mtibwa Sugar bado 9 tu Championship

Mtibwa Sugar kwa sasa inahitaji pointi tisa tu kurejea Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kuteremka msimu uliopita.

Mtibwa Sugar inaongoza Ligi ya Championship baada ya kucheza mechi 25, ikishinda 19, sare tatu na kupoteza tatu ikifanikiwa kukusanya pointi 60, imebakiza mechi tano ili kuhitimisha msimu huu.

Katika mechi hizo tano zenye pointi 15, endapo Mtibwa itashinda mechi tatu itafikishe pointi 69 ambazo hazitofikiwa na timu iliyopo nafasi ya tatu kwa sasa, hivyo kuwa na uhakika wa kumaliza nafasi mbili za juu zinazowapa tiketi ya kupanda daraja moja kwa moja.

Katika michezo hiyo mitano, Mtibwa itacheza nyumbani miwili na mitatu ugenini.

Kwa sasa Mbeya City inafuatia kwenye msimamo wa Championship ikiwa na pointi 55 ambapo ikishinda mechi zote tano itamaliza ligi na pointi 70 huku Stand United inayoshika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 52 ambazo hata ikishinda mechi zote zilizobaki itaishia na pointi 67.

Mtibwa ilishuka daraja msimu uliopita, tangu hapo imeonekana kupigania nafasi ya kurejea Ligi Kuu ikiwa na rekodi ya kutodondosha pointi kwenye uwanja wake wa nyumbani.

Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar, Awadhi Juma amesema bado hawajamaliza kwani wana mechi tano ambazo wanazibeba kama fainali kwa sababu kuna wanaowafukuza, hivyo ili kuendelea kufukuzana nao lazima wahakikishe wanapata matokeo bora kila mchezo ili kufikia malengo.

“Haijaisha mpaka iishe, siwezi kusema tumemaliza kazi, bado mechi tano ni nyingi na kila timu tunayokutana nayo inahitaji matokeo, hivyo kazi inaendelea, tunajipanga kuhakikisha tunapata matokeo bora ili kuendelea kusukuma gurudumu kurudi Ligi Kuu,” alisema na kuongeza:

“Ushirikiano mzuri tulioanza nao tunatarajia kuendelea nao hadi mwisho wa msimu, ni mapema sana kujikweza kuwa tumesharudi Ligi Kuu au tuna uhakika wakati bado tuna michezo mitano mkononi na wanaotufuata hatujawaacha mbali, kikubwa ni mapambano bado yanaendelea.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *