
Dar es Salaam. Madereva taksi wamekuwa na mitazamo tofauti kufuatia kauli ya Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Ardhini (Latra) kutangaza kuanza mchakato wa kuweka mita katika taksi (taxmeters) ili kuweka uhalisia wa nauli kwa watumiaji.
Wengine wamedai kitendo hicho kitaua biashara yao ambayo tayari imeshasinzia, mwingine akidai ni ngumu kupanga nauli wakati mafuta bei yake hauwezi kuidhibiti na wengine wakisema ni maumivu pande zote kwa abiria na dereva.
Maoni yao yanakuja ikiwa ni siku nne tangu Machi 25, 2025, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo (WMA), Alban Kihulla kusai kuwa wanatarajia kuanza uhakiki wa mita za vyombo vya usafiri (taxmeters) kwa lengo la kuendelea kuwalinda wananchi kupitia usimamizi wa matumizi sahihi ya vipimo.
Kuhusu mpango huo Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano cha Latra, Salum Pazzy anasema tayari mamlaka wamenunua vifaa vichache kwa ajili ya majaribio ya kuunganisha na mifumo ya Latra ili kuwezesha mita zitakazokuja zote zikidhi haja ya kuzungumza na mifumo yao yote na vigezo vya WMA.
“Lakini watakaoziuza mita hizo ni wananchi haohao watakaotaka kuingia katika hiyo biashara hiyo na kuwa na miongozo itakayowataka vifaa vyao (mita) viwe vimekidhi vigezo na vinatuma taarifa kwa mamlaka yetu,” anasema Pazzy.
Ametaja sababu za mita hizo kutuma taarifa kwa mamlaka ni kuhakikisha nauli iliyopangwa inafuatwa kwa kufanya hivyo kutawezesha biashara hiyo ambayo inaonekana kama haina uratibu kuratibiwa (regulate).
“Sasa hivi hawa ambao hawatumii mitandao, wanakoenda, wanakotoka haijulikani, wameenda kushusha watu wapi haijulikani. Kwa hiyo itasaidia kwa upande wa usalama pia,” amesema.
Pazzy amesema mita hizo pia zitasaidia katika kujua mahitaji ya aina mbalimbali ya usafiri yako sehemu gani kwa maana wanaotumia bodaboda, teksi ama bajaji.
Amesema ufungaji wa mita hizo utaisaidia Serikali katika mipango ya usafiri na wale ambao hawako katika huduma ya teksi mtandao wataweza kufanya biashara zao kisasa zaidi kwa kutumia teknolojia.
Pazzy amesema kwa kufanya hivyo watakuwa wamelinda maslahi ya watoa huduma na wanaohudumiwa.
“Kwa kuwa bei zitapangwa na Serikali hakutakuwa na ulazima wa kumshawishi mteja kumlipa kiasi fulani cha fedha, bali atalipa kile kilichopangwa na Serikali.
Akizungumzia suala hili, Mwenyekiti wa kituo cha teksi Kivukoni Feri, Mustapha Mbawala amesema suala hilo litaumiza pande zote yaani abiria na dereva.
“Hili lingefanyika wakati ambao miundombinu imekamilika lakini kama haipo ni changamoto maana sasa hivi njia ambayo mtu anaweza kwenda kwa dakika 20 anatumia saa mbili,” amesema.
Amesema hii ni sawa na kuiga kitu kutoka nchi za watu ambazo zimeshaweka miundombinu rafiki na kuleta sehemu ambayo mambo mengi yanahitaji kufanyiwa kazi bado.
“Sasa hivi tu unaweza kukaa siku mbili hujapata abiria, halafu abiria aje uniambie nauli yake isomwe kwenye mita badala ya makubaliano mwisho wa siku ije Sh5,000 si kweli,” amesema.
Ikiwa hili litafanyika wakati njia bado zina msongamo hawatapata matokeo wanayohitaji kwani watu wengi sasa wanakimbilia usafiri rahisi ikiwemo pikipiki.
“Mapatano ni mazuri zaidi, maana hii kuweka mita ni kama unaua zaidi biashara yenyewe, miundombinu mibovu haikidhi haja,” amesema.
Dereva Nassor Simba anayepaki Posta ya zamani anasema ufungaji mita hauna faida kwa sababu utamuumiza dereva hasa katika kipindi hiki ambacho haiwezi bei ya mafuta haiwezi kudhibitiwa na imekuwa ikipanda na kushuka.
“Halafu si kitu kipya, zamani kilikuwepo unafungiwa lakini ilishindikana kwa sababu hatuwezi kudhibiti bei za mafuta, ilileta mvurugano tukarudi katika hali tuliyoizoea, ukifanya kitu kama hicho kesho bei inapanda je utakuwa unapandisha bei uliyoweka ili usimuumize dereva,” alihoji.
Amesema ikiwa wanataka hilo lifanikiwe serikali iongeze uwekezaji kwenye gesi ili kupunguza gharama za uendeshaji pamoja na kupitia upya bei za ufungaji mifumo ya gesi.
“Pia bei kwa kilomita iangaliwe ili usimuumize abiria kwani ukikaa kwenye foleni muda ukizidi hela inaongezeka unamuumiza abiria,” amesema Simba.
Mansoor Aboubakar ambaye pia ni dereva Upanga amesema ni vyema maoni yakusanywe kwa madereva kabla ya jambo hilo kuanza kutekelezwa ili kuhakikisha kinachofanyika hakimuumizi mtu yoyote.
“Hii itasaidia kuondoa malalamiko, si unaona hata hao Bolt na Uber wanavyogoma kila siku sasa ile ni kwa sababu ni programu inakuwa ngumu mtu kuichezea sasa hii ya kufunga inakuwa rahisi sana mteja kuumizwa na wajanja,” amesema Aboubakar.