Mtathimini adai mazao yaliyoharibiwa yalikuwa ya Sh33 milioni

Dar es Salaam. Mtathimini Gregory Mwampule (69) ameieleza mahakama kuwa hasara ilitokana na uharibifu wa mazao yaliyowekezwa katika kiwanja alichopewa, Askofu John Sepeku ilikuwa Sh33 milioni.

Amedai kiwanja hicho chenye ukubwa wa ekari 20 kilichopo Buza Mtoni, kilipimwa mwaka 2010, kilivamiwa na mwekezaji ambaye alikata mazao mbalimbali yaliyokuwepo katika kiwanja hicho na kisha kujenga kiwanda.

Ndani ya kiwanja hicho, imejengwa nyumba yenye thamani ya Sh165 milioni na kwa tathimini ya sasa ya ardhi katika eneo hilo ina thamani ya Sh3.7 bilioni.

Mwampule ametoa maelezo hayo leo, Mahakama Kuu, Divisheni ya Ardhi, wakati akitoa ushahidi wake katika kesi ya ardhi iliyofunguliwa na Bernardo Sepeku, dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Askofu Jackson Sostenes wa kanisa hilo pamoja na Kampuni ya Xinrong Plastic Waste Industry Co Ltd.

Bernado, ambaye ni mtoto wa askofu Sepeku, alifungua kesi hiyo ya ardhi namba 378/2023, akipinga kunyang’anywa zawadi ya kiwanja alichopewa baba yake mwaka 1978 na kanisa hilo.

Askofu Sepeku alipewa zawadi na kanisa hilo ambayo ni nyumba iliyopo Buguruni na kiwanja chenye ukubwa wa ekari 20 kilichopo Buza, wilayani Temeke, kama zawadi kwa kutambua mchango wake katika kanisa hilo.

Katika kesi hiyo, Bernardo anadai alipwe Sh3.72 bilioni ambayo ni fidia ya hasara ya kifedha iliyopatikana kutokana na uvamizi wa mali ya ardhi katika kiwanja hicho.

Pia anaiomba alipwe fidia ya Sh493.65 milioni ambayo ingepatikana baada ya kukomaa na mavuno ya mazao yaliyokuwepo kwenye shamba hilo.

Bernardo ambaye ni msimamizi wa mirathi ya baba yake, anaomba mahakama hiyo iamuru wadaiwa hao kumlipa Sh33 milioni ikiwa ni hasara aliyoipata kutokanana na uharibifu wa mazao yaliyowekezwa katika shamba lililo ndani ya kiwanja hicho.

Akiongozwa kutoa ushahidi wake na wakili, Gwamaka Sekela, mbele ya Jaji Arafa Msafiri, Mwapule alidai kuwa yeye ndio aliyefanya tathimini ya upimaji wa ardhi katika kiwanja G chenye ukubwa wa ekari 20 lililopo Buza, baada ya kutafutwa na Bernardo akitakiwa kupima eneo lilolovamiwa na kuharibiwa mazao.

Mwapule kutoka Kampuni ya GMREC & Developers Ltd, ametoa ushahidi wake wa njia ya mtandao akiwa nyumbani kwake Bunju- Mabwepande amedai kuwa Julai 24, 2023 alifanya tathmini ya eneo lilovamiwa na zoezi hilo lilichukua siku tatu.

Baada ya hapo, Septemba 2023 aliandaa ripoti ambayo imepokelewa na mahakama hiyo.

Mtathimini huyo ameshindwa kufika mahakamani hapo kutokana na kufanyiwa upasuaji wa macho hivi karibuni na kuelekezwa daktari wake, asitoke nje na apate muda wa kupumzika akiwa ndani, hali iliyopelekea mahakama kusikiliza kesi hiyo kwa njia ya mtandao.

Katika maelezo yake ya ushahidi, Mwapule alidai mazao yaliyoharibiwa shambani ni pamoja na miti 200 ya malimao, miti 55 ya mikorosho, hekari mbili za mbaaza, hekari mbili za mihogo na hekari mbili za viazi vitamu.

Mazao mengine yaliyoharibiwa shambani hapo ni miti 30 za mapapai, minazi, miti 60 ya miembe, miti 25 ya michikichi pamoja na miti 45 ya minazi.

“Baada ya kumaliza kufanya tathimini, niliandaa ripoti mbili, moja ikiwa ni ripoti ya tathimini ya uharibifu wa mazao yaliyopo katika ardhi hiyo na nyingine ni ripoti ya thamani ya ardhi, nyumba na mali nyingine zilizopo katika eneo hilo.

Alidai mbali na kufanya tathimini ya eneo hilo, pia alipiga picha mazao yaliyoharibiwa na kuambatanisha picha hizo katika ripoti aliyoiwasilisha mahakamani hapo.

Pia aliwasilisha leseni yake ya kazi ambayo inamtambulisha kuwa yeye ameidhinishwa na bodi na amesajiliwa kisheria kufanya kazi hiyo.

Shahidi huyo mwenye shahada ya uzamili ya masuala ya kutathimini ardhi, aliomba mahakama ipokee ripoti hizo mbili pamoja na leseni yake ya kazi, ziwe sehemu ya ushahidi katika kesi hiyo.

Hata hivyo, wakili wa wadaiwa hakuwa na pingamizi juu ya nyaraka hizo, hivyo mahakama ilizopoke na kuwa kielelezo namba 10, 11 na 12.

Baada ya kumaliza kutoa ushahidi, alihojiwa na wakili wa wadaiwa katika shauri hilo, Dennis Malamba kuhusiana na ushahidi aliyoutoa na sehemu ya mahojiano ilikuwa ni kama ifuatavyo.

Wakili: Shahidi umesoma chuo gani

Shahidi: Chuo Kikuu cha Ardhi

Wakili: umesoma levo gani?

Shahidi: Nimemaliza shahada ya kwanza ya masuala ya tathimini na upimaji wa ardhi mwaka 1990 na shahada yangu ya pili nimemaliza mwaka 2011.

Wakili: Kwa hiyo wewe ni mzoefu katika upimaji wa ardhi?

Shahidi:Sio sana.

Wakili: Kwenye ushahidi wako umetoa leseni yako kazi ya mwaka gani?

Shahidi: Ya mwaka 2024/2025 na kila mwaka tunahuisha leseni.

Wakili: Kabla ya kwenda kufanya tathimini ya ardhi lazima ujue mmiliki wa ardhi?

Shahidi: Ndio

Wakili: Kwenye hiyo ardhi uliyofanya tathimini nani alikuwa mmiliki wake?

Shahidi: Bernardo ambaye ni msimamizi wa mirathi.

Baada ya kumaliza kuhojiwa, upande wa mlalamikaji walifunga ushahidi wao na hivyo upande wa mdaiwa wataanza kutoa ushahidi.

Wakili Malamba amedai atakuwa na mashahidi watatu ambao watatoa utetezi wao kuhusiana na kesi hiyo.

Jaji Msafiri baada ya kusikiliza maelezo hayo, ameahirisha kesi hiyo hadi Juni 4 na Juni 5, 2025 saa tano asubuhi, kesi hiyo itakapoendelea.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *