Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Kinga wa Wizara ya Afya wa Tanzania, Dk Ntuli Kapologwe ameibuka mshindi wa nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa Jumuiya ya Afya ya Nchi za Afrika Mashariki, Kati na Kusini (ECSA – HC) na kuwashinda wagombea wengine sita waliokuwa wakiwania nafasi hiyo.
Uchaguzi wa nafasi hiyo umehitimishwa leo Jumatano, Februari 12, 2025 nchini Malawi.
Dk Kapologwe anachukua nafasi hiyo kutoka kwa Profesa Yoswa Dambisya wa Uganda ambaye amehudumu kwenye nafasi hiyo kwa mihula miwili ndani ya miaka 10.
Dk Kapologwe kwa kuzingatia vigezo maalumu vilivyowekwa katika makubaliano ya jumuiya hiyo, ataongoza kwa miaka mitano.

Akizungumza baada ya kuhitimisha uchaguzi huo, Waziri wa Afya wa Tanzania, Jenista Mhagama amesema nafasi hiyo ilipotangazwa mara ya kwanza jumla ya waombaji 47 waliwasilisha wasifu wao na kati yao, saba walichaguliwa kuendelea baada ya mchujo wa awali.
Waziri Mhagama amesema baada ya usaili uliofanywa na kamati ya mkutano wa makatibu wakuu wa nchi wanachama, Dk Kapologwe alipata alama za juu zaidi na kuingia katika hatua ya mwisho pamoja na wagombea wengine wawili kutoka Kenya na Malawi.
Amesema majina ya wagombea hao watatu yaliwasilishwa kwenye Mkutano wa Jumuiya ya Afya ya Nchi za Afrika Mashariki, Kati na Kusini (ECSA – HC) ndipo Dk Kapologwe akaibuka mshindi.

Amesema kwa ushindi huo ni dhahiri ya kwamba, Tanzania inaendelea kuuthibitishia ulimwengu kuwa ina watalaamu wenye sifa stahiki za kushika nafasi za uongozi kwenye jumuiya au mashirika ya kimataifa na kutoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya wengi katika uboreshaji wa huduma za afya.

“Hii ni mara ya pili kwa Tanzania kushika nafasi hii katika kipindi cha miaka 51 cha jumuiya hiyo, kwa mara ya kwanza, Mtanzania Dk Winnie Mpanju alihudumu kama mkurugenzi mkuu kati ya mwaka 1993 na 2000. Ni mafanikio makubwa kuona Tanzania inapata nafasi hii tena baada ya miaka 27,” amesema Waziri Mhagama.
Jumuiya ya ECSA-HC ilianzishwa mwaka 1974 na inajumuisha nchi za Tanzania, Malawi, Kenya, Lesotho, Zambia, Zimbabwe, Mauritius, Uganda na Eswatini.
Pia, inashirikiana na nchi 13 zisizo wanachama ambazo ni Botswana, Burundi, Cameroon, Eritrea, Gabon, Liberia, Msumbiji, Namibia, Rwanda, Seychelles, Sudan ya Kusini, Sudan na Somalia.

Kufuatia ushindi huo, wajumbe wa Tanzania wameshangilia huku wakimpongeza mgombea wake aliyependekezwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwania nafasi hiyo.
Jumuiya ina jukumu la kukuza na kuimarisha ushirikiano wa kikanda wa kushughulikia masuala ya afya baina ya nchi ya wanachama ikiwamo kutatua changamoto za sekta ya afya na kupeana uzoefu wa kuboresha huduma za afya.