Mtanzania aitaka rekodi Misri

BAADA ya kusaini mkataba wa miezi sita wenye kipengele cha kuongeza, mshambuliaji wa Kitanzania, Oscar Evalisto amesema anatamani kuandika historia ya kufunga mabao akiwa na Makadi FC ya Misri.

Evalisto alisajiliwa hivi karibuni na timu hiyo inayoshiriki Ligi Daraja la Pili nchini Misri akitokea Mlandege FC ya Zanzibar.

Mshambuliaji huyo alikuwa kwenye kikosi cha Mlandege kilichoshinda bao 1-0 dhidi ya Simba, kwenye mechi ya fainali ya Kombe la Mapinduzi msimu uliopita.

Akizungumza na Mwanaspoti, Evalisto alisema ikiwa ni mara ya kwanza kwake kucheza soka la kulipwa Misri kama mshambuliaji anatamani kufunga kila anapopata nafasi.

“Matarajio yangu ni kufanya vizuri kwenye raundi ya pili kwa maana huu ni mwanzo tu lakini malengo yangu ni kufika Ligi Kuu ya hapa,” alisema Evalisto.

Aliongeza kuwa hadi sasa changamoto kubwa aliyokutana nayo ni upande wa chakula na lugha ambayo asilimia kubwa ya wachezaji wanaongea Kiarabu.

“Mazingira ni mazuri japo changamoto kubwa ni vyakula na lugha, wamekuwa wavivu sana kujifunza lugha nyingine zaidi ya lugha yao ya Kiarabu ila nashukuru baadhi ya wachezaji wanaongea Kiarabu na Kiingereza wanakuwa wananitafsiria.”

Kabla ya Mlandege alicheza Paje Stars ya Zanzibar, Iringa United na Lipuli ya vijana U-20.