
MSHAMBULIAJI wa Makadi FC, Oscar Evalisto amesema ameanza kuyazoea mazingira ya soka la Misri na licha ya timu hiyo kushiriki daraja la pili, anakiri ni ligi ngumu na ngeni kwa upande wake.
Evalisto alisajiliwa hivi karibuni na timu hiyo akitokea Mlandege FC ya Zanzibar kwa mkataba wa miezi sita.
Akizungumza na Mwanaspoti, Evalisto alisema licha ya ugeni wa ligi hiyo, tayari ameanza kuizoea akiamini kama ataendelea kupata nafasi ataonyesha kiwango bora.
“Mechi ya kwanza nimefunga bao moja, tukishinda tatu bila na juzi tumetoka sare 1-1, baada ya kuanza kufungwa nikasawazisha, hivyo naamini nikizoea zaidi itanisaidia kuwa bora,” alisema Evalisto.
Aliongeza kocha wa timu hiyo amekuwa na mchango mkubwa kwake kwani kila anapotoka uwanjani anampa maelekezo ya kupunguza na kuongeza baadhi ya vitu.
“Nashukuru jambo kubwa sana unapofanya kocha anakuita na kukuambiwa, anaonyesha anakubali uwezo wangu na mimi kama mchezaji napambana nisimwangushe.”
Hii ni mara ya kwanza mshambuliaji huyo kucheza nje na aliwahi kupita Mlandege, Paje Stars ya Zanzibar, Iringa United na Lipuli ya Vijana U-20.