
Dar es Salaam. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo imeonesha kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa mtambo mpya wa mabati ya rangi wa Kampuni ya Alaf Limited, ikiitaka Serikali kuboresha mazingira ya uzalishaji na biashara ili kiwanda kizalishe kwa ufanisi na kuleta faida.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Deo Mwanyika ameipongeza Alaf kwa uwekezaji huo wa kiwanda kipya cha mabati ya rangi kinachotarajiwa kuanza uzalishaji mwezi ujao.
Akizungumza walipotembelea kiwanda hicho jana Jumamosi Novemba 2, 2024, Mwanyika amesema: “Tumekuja kutembelea kiwanda na kujionea maendeleo ya mtambo huu mpya wa rangi, tumefarajika kuona kwamba hivi karibuni tu uzalishaji utaanza. Sisi kama kamati tutachukua maoni yao kama vile kodi zenye kero na uwanja usiokuwa sawa wa biashara.” Amesema mtambo mpya wa rangi utahakikisha ubora, ajira zaidi kwa Watanzania na kwamba hakutakuwa na uingizaji wa mabati ya aina hiyo kutoka nje kwani uzalishaji utatosheleza mahitaji ya nchi nzima.
“Tumefurahi pia, kusikia kuwa mtambo huu mpya utaendeshwa na Watanzania, tayari mainjinia 30 vijana wamepokea mafunzo ya kina nje ya nchi,” amesema Mwanyika.
Hata hivyo, amesema kamati imekubaliana na Alaf kuwa watafanya kikao kingine cha pamoja Dodoma ili kampuni hiyo iwasilishe masuala yote na kamati ijadili kwa kina wayawasilishe serikalini kwa usahihi.
“Leo tumekuja kufanya ziara tu hatuwezi kujadiliana na kumaliza kila kitu leo tunahitaji kukaa tena kwa pamoja tuyaangalie haya masuala vizuri,” ameeleza.
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe ameipongeza Alaf kwa uwekezaji huo mkubwa na kusisitiza kuwa Serikali itafanya kila jitihada kuhakikisha inaweka mazingira bora ya biashara na kwamba mtambo mpya wa wa rangi uzalishe kwa faida.
“Alaf inazalisha mabati yenye ubora mkubwa sana na sisi kama Serikali tunataka Watanzania waweze kupata bidhaa zenye ubora kwa maana hiyo hatuna budi kuhakikisha vikwazo vilivyopo kwa sasa vinaondoka ili waweze kufanya biashara kwa ufanisi,” ameeleza na kuongeza kuwa watakaa pamoja na uongozi wa Alaf ili kutatua kero zilizopo.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Alaf Limited, Ashish Mistry ameishukuru kamati hiyo kwa kutenga muda wa kuwatembelea na kuwahakikishia kuwa kiwanda kipya cha mabati ya rangi kitaanza uzalishaji mwezi ujao.
“Tunawahakikishia ubora wa hali ya juu wa mtambo huu ambao utakuwa bora kabisa Afrika na utazalisha zaidi ya mahitaji ya Tanzania,” amesema Mistry.
Meneja Uhusiano na Mawasiliano wa Alaf, Hawa Bayumi ametoa wito kwa Watanzania wapende vya nyumbani na wajiandae kwa ubora wa hali ya juu huku akisisitiza kuwa kwa msaada wa kamati hii ya Bunge, wanaamini Serikali itatatua kero zote zinazoathiri uzalishaji kwa sasa.
“Tunachohitaji kama Alaf ni uwanja sawa wa kufanyia biashara na mazingira bora,” amesema na kuongeza kuwa kiwanda kipya kitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani 75,000 kwa mwaka ambazo ni zaidi ya mahitaji ya Tanzania.