Mtaalamu wa UN akosoa vyombo vya habari vya magharibi kwa kuficha ghasia za Waisraeli Amsterdam

Mtaalamu wa sheria wa Umoja wa Mataifa ametoa wito kwa vyombo vya habari vya Magharibi kuchunguzwa kwa “kuficha” utangazaji wa habari kuhusu ghasia zilizoibuliwa siku ya Ijumaa na mashabiki wa utawala wa Israel katika mji wa Amsterdam nchini Uholanzi.

Katika chapisho kwenye mtandao wa X, zamani wa Twitter, Francesca Albanese, ripota maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya haki katika eneo la Palestina linalokaliwa kwa mabavu, amesema kuwa vyombo vya habari vya Magharibi mara kwa mara vinasambaza habari za upotoshaji ambazo zimesaidia kuficha ukatili unaofanywa na Waisraeli kote duniani.

Mwanasheria huyo wa kimataifa wa Italia amesema: “Kwa mara nyingine tena, vyombo vya habari vya Magharibi vinapaswa kuchunguzwa kwa kuficha ukatili wa Israel.”

Msomi huyo wa sheria, mtafiti na mwandishi aliyebobea katika masuala ya haki za binadamu amesema wanahabari wanaosambaza habari za uongo wanahusika na uhalifu wa Israel na wanapaswa kuwajibishwa.

Amesema  mahakama za kimataifa zimewahi kuwapata na hatia waandishi habari katika uchochezi na uhalifu mwingine wa kimataifa.

Wito huo wa mtaalamu wa Umoja wa Mataifa umekuja baada ya baadhi ya vyombo vya habari vya nchi za Magharibi kushindwa kuripoti au kudogesha uhalifu wa wahuni Waisraeli waliojifanya kuwa mashabiki wa timu ya mpira wa miguu ya Maccabi Tel Aviv kabla na wakati wa ghasia hizo, siku za Alhamisi na Ijumaa iliyopita.

Wahuni wa Maccabi Tel Aviv, Amsterdam

Walipofika katika mji mkuu wa Uholanzi kabla ya mechi hiyo, video mtandaoni ziliwaonyesha wanaojiita mashabiki wa soka wa Israel wakirarua bendera za Palestina zilizokuwa zimepeperushwa katika nyumba za wakazi.

Timu ya soka ya Maccabi Tel Aviv ilikabiliana na timu ya Ajax Amsterdam siku ya Alhamisi, ambapo ilichapwa 5-0 na timu hiyo ya Uholanzi katika uwanja wa nyumbani wa Ajax.