Msuva anavyoibeba Stars kwa bao mbilimbili Afcon

Dar es Salaam. Mshambuliaji Simon Msuva ameonekana kuisaidia Taifa Stars kwenye mechi muhimu za kufuzu mashindano ya Afcon akiwa amehusika katika mabao mengi yaliyoipeleka Stars Afcon mara tatu.

Mwaka 2019, alifunga mabao mawili, akiifunga Cape Verde bao moja pamoja na Uganda aliyoifunga bao moja kwenye mechi ya mwisho ya Kundi L ambapo Stars ilishinda mabao 3-0, ikifuzu michuano ya Afcon iliyofanyika Misri.

Mwaka 2021, Msuva alifunga mabao mawili kwenye hatua za makundi ya kufuzu Afcon ambapo aliifunga Uganda bao moja lililodumu mpaka dakika 90 kama alivyofanya dhidi ya Niger ambayo ailiifunga bao moja lililoipa Stars pointi tatu kati ya nne ilizokuwa nazo.

Stars ilipata ushindi kwenye michezo miwili ya makundi ambapo Msuva alifunga bao moja kila mechi na kuipa Stars alama sita zilizoisaidia kufuzu michuano ya Afcon iliyofanyika Ivory Coast 2022.

Mwaka huu Msuva ameendeleza rekodi ya kuifungia Stars kwenye mechi muhimu ambapo aliifunga Ethiopia bao moja huku bao lingine akifunga kwenye mechi ya mwisho dhidi ya Guinea, likiwa ni bao pekee lililoipeleka Tanzania kushiriki mashindano ya Afcon yatakayofanyika Morocco 2025.

Kwenye mabao matano staa huyo amefanikiwa kufunga mabao mawili na kuonyesha kuwa ameendeleza moto wake kwenye michuano hiyo.

Msuva alianza kuitumikia Stars Agosti 15, 2012 akifunga mabao 24 akiwa nyuma kwa bao moja kumfikia Mrisho Ngassa ambaye ndiye kinara akiwa na mabao 25.