
Dar es Salaam. Wanasaikolojia wanasema moja kati ya sababu zinazoweza kumfanya mtu kuwa mnene kupindukia, ni kukabiliwa na msongo wa mawazo.
Mwanasaikolojia Charles Kalungu amesema msongo unaweza kumfanya mtu anenepe kwa sababu ya kuvurugwa kwa mfumo mzima wa mwili na akili, ambapo mtu hujaribu kujitafutia furaha kupitia kula vyakula bila kujali kama vina faida au madhara kwa afya yake.
“Mwili kuongezeka au kupungua itategemeana sana na aina ya mapokeo ya tatizo husika yatakayomsababisha kupata hamu ya kula kupita kiasi au kukosa kabisa hamu ya kula kunakoweza kusababisha mwili kuongezeka au kupungua. Hiyo yote ikiwa ni kutafuta amani na utulivu wa moyo ili kusahau machungu,” amesema Kalungu.
Amesema mwili wa binadamu huwa una mifumo ya kujitetea ambayo hufanya kazi kwa kushirikiana na ubongo ambapo huweza kumuathiri mtu kulingana na mapokeo ya kifikra aliyonayo kuhusu tukio au jambo fulani.
“Ubongo huwa una kemikali mbalimbali ambazo huwa zinaufanya mfumo wa akili kuitikia katika matukio fulani. Mwitikio huu ukiwa endelevu, unaweza kumfanya mtu apate mabadiliko fulani ya kimwili au kiakili kama asipotafuta ufumbuzi, “ amesema.
Ameendelea kusema kuwa mabadiliko ya kemikali na vichocheo mbalimbali mwilini yanayosababishwa na msongo wa mawazo, huchangia uzalishaji wa protini ya ‘betatrophin’ ambayo hubadili mafuta yanavyohifadhiwa mwilini.
Ameongezea kuwa moja ya sababu ambazo zinachangia kwa kiasi kikubwa kuzorota kwa afya na kusababisha vifo vingi ni msongo wa mawazo.
“Msongo wa mawazo una athari nyingi kama kusababisha mtu kujiingiza kwenye ulevi uliopindukia, kuvurugika kwa homoni katika mwili, kusababisha macho kupunguza uwezo wa kuona na vilevile kusababisha kifo,”amesema.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) watu takribani milioni 350 duniani wameathiriwa na tatizo la msongo wa mawazo na asilimia 75 ya watu wanaokabiliwa na hali hii katika nchi zinazoendelea, hawapati matibabu.
Vilevile shirika hilo limeonya kuhusu ongezeko la watu wenye unene wa kupitiliza, huku likitaja hiyo kuwa hali hiyo ni mojawapo ya sababu kuu za maradhi ya moyo, kisukari na ini.
Meneja mradi wa afya ya mama na mtoto na mtaalamu wa lishe kutoka Shirika la Word Vision, Dk Daud Gambo amesema katika kipindi ambacho mtu anakuwa na msongo mkubwa wa mawazo, mwili hutumia kiasi kikubwa cha sukari hasa katika ubongo kutokana na nguvu kubwa inayotumika katika kufikiria mambo yanayomsibu.
“Hivyo mtu huhitaji kwa kiwango kikubwa vyakula vyenye ladha nzuri mdomoni na vyenye wingi wa sukari, chumvi pamoja na mafuta kama vile chipsi, soda au bia. Matumizi ya muda mrefu ya vyakula hivyo humsababishia kunenepa kupindukia,” amesema.
Amesema vilevile mtu anaweza kukonda kutokana na kutokula chakula kama inavyohitajika na ikumbukwe katika kipindi hicho mwili huhitaji kwa kiasi kikubwa vyakula vinavyoongeza nguvu pamoja na sukari.
Fanya haya kuondokana na msongo wa mawazo
Mwanasaikolojia Modesta Kamonga amesema msongo wa mawazo, huleta athari katika afya ya mwili na akili hivyo kusababisha hata kupungua kwa ufanisi wa utendaji kazi wake.
Amesema ni muhimu kutumia mbinu zinazoshauriwa kitaalamu ili kukabiliana nazo na kuepuka madhara ambayo yanaweza kujitokeza hapo baadaye.
Amesema miongoni mwa mbinu zinazoelezwa kusaidia kuondokana na msongo wa mawazo, ni pamoja na kutambua sababu ya hali hiyo na kuepuka mambo yote yatakayosababisha hali hiyo.
Amesisitiza kuwa ili kupambana na msongo wa mawazo, ni muhimu kuelewa sababu zinazosababisha hali hiyo.
“Kwa kutambua chanzo, mtu anaweza kupata suluhisho sahihi na kuchukua hatua zinazofaa, ”ameeleza.
Ameshauri kuwa mtu anayesumbuliwa na changamoto hizo ni vyema kuepuka unywaji wa pombe kupita kiasi, matumizi ya dawa za kulevya, na matumizi ya simu kupita kiasi kwani yanaweza kuongeza msongo wa mawazo.
“Kujiepusha na vitu hivi kunaweza kusaidia mtu kuwa na utulivu wa akili, ”amesisitiza.
Amesema badala ya kutumia vitu hivyo ambavyo kimsingi havisaidii kundoa msongo wa mawazo, ni vyema mtu kujikita katika ufanyaji wa mazoezi ya mwili pamoja na kuzingatia lishe bora.
Amesema ufanyaji wa mazoezi husaidia kupunguza msongo wa mawazo kwa kuongeza uzalishaji wa homoni za furaha kama ‘endorphins’.
“Mazoezi kama kutembea, kukimbia, yoga, na kucheza michezo mbalimbali yanaweza kusaidia katika kupunguza msongo wa mawazo,”amesisitiza.
“Pia ni muhimu kuhakikisha unapata angalau saa saba hadi nane za usingizi kila siku ili akili na mwili vipate nafasi ya kupumzika na kurejea katika hali ya kawaida, ”ameeleza.