
Dar es Salaam. Wakati mkutano wa 29 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCC – COP-29) ukianza leo Jumatatu, Novemba 11, 2024, Tanzania ambayo ni miongoni mwa washiriki imeazimia kuwa na mikakati ya pamoja na nchi wanachama, ikiwa ni hatua za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi yanayoipasua kichwa dunia.
Pia, katika mkutano huo unaofanyika hadi Novemba 22, 2024 jijini Baku nchini Azerbaijan, Tanzania inayowakilishwa na Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango anayemwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan, utajadili fursa za nishati safi ya kupikia pamoja na biashara ya kaboni.
Aidha, mkutano huo utajadili namna ya kuongeza uwekezaji kwenye uchumi wa buluu katika maeneo ya bahari na maziwa makuu, kama hatua ya kukabiliana na athari za mabadiliko hayo.
Vilevile, Dk Mpango anatarajiwa kuhutubia katika mkutano huo na ataeleza msimamo na jitihada zinazochukuliwa na Serikali ya Tanzania katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Mwaka 2023 katika mkutano wa COP-28 uliofanyika Dubai, Tanzania kupitia Rais Samia ilijadili nishati safi ya kupikia, kilimo endelevu, na uchumi wa buluu huku ikizindua programu ya kuwakomboa wanawake wa Afrika kupitia matumizi ya nishati safi ya kupikia (AWCCSP).
Programu hiyo inalenga kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, ili kukabiliana na changamoto za afya, mazingira, uchumi na kijamii ambazo huathiri zaidi wanawake na watoto. Kutokana na kwamba wanawake hutumia muda mrefu kutafuta kuni, programu hiyo itawasaidia kupata muda wa kutosha kushiriki kwenye shughuli za maendeleo.
Wadau wachambua
Mwanaharakati wa mazingira na mwanasayansi ya jamii, Shamim Wasii Nyanda amesema anatarajia katika mkutano unaoanza leo njia za kukabiliana na athari za hali ya mabadiliko ya tabianchi kwa nchi zinazoendelea itapewa kipaumbele.
Amesema ni mkutano unaolenga kukusanya fedha kwa ajili ya mfuko wa kukabiliana na mabadiliko hayo kwa nchi wanachama. Amesema duru zinasema mkutano huo unaweza kuathiri mkutano ujao wa 30 endapo fedha zisipopatikana kwa nchi ambazo hazijaendelea.
Aidha, amesema kwa upande Tanzania katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi inajitahidi ikishirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali.
“Tanzania inashirikiana na wadau wa mazingira, inajitahidi kwa kuanzisha miradi mbalimbali ya uhamasishaji. Kitu cha kuwekeza zaidi ni elimu ya hali hiyo kuanzia madhara yake kwa jamii,” amesema na kuongeza kwamba lazima nguvu iongezwe kwa vyombo vya habari katika kukabiliana na hali hiyo.
Mdau wa mazingira, Petro Damian kwa upande wake anasema ameona tatizo la kukosekana kwa taarifa kwa yanayoendelea kwenye mikutano hiyo, akisema inachangia watu kutopata uelewa wa nini kinafanyika kwa kina.
Ameshauri iundwe taasisi maalumu ya utoaji taarifa kamili za kila siku, ili Watanzania wafahamu nini kinaendelea hatua kwa hatua.
Mshauri wa nishati mpito Afrika kutoka Shirika la Kufuatilia Usimamizi wa Rasilimali za Asili (NRGI), Silas Olang’ amesema mkutano huo utajadili wale wanaochangia kwa kiasi kikubwa kuzalisha hewa ya ukaa wanachangiaje katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
“Wote tunahusika na tunajali mabadiliko ya tabianchi, lakini tuna wajibu tofauti, kwani mchango wa nchi zinazoendelea katika kuzalisha hewa ya ukaa ni mdogo ukilinganisha na zile zilizoendelea, hivyo wanaochangia kwa kiasi kikubwa wanachangiaje kwa wanaoathirika,” amesema.
Amesema changamoto iliyopo ni fedha kwa nchi zilizotoa ahadi ya kukabiliana na athari za mabadiliko hayo na kwamba nchi zinazoathirika zimekuwa zikikumbushia fedha hizo muhimu.
Mwanzilishi wa Khanyi Foundation, Anabahati Mlay amesema mkutano umejikita zaidi kwenye namna ya kuhakikisha tunafikia malengo ya mkutano wa Paris ya kuhakikisha tunapunguza ongezeko la joto duniani na hewa ukaa kuwa chini ya 1.5C, lakini zaidi ni namna ya kuongeza na kukusanya fedha zilizoahidiwa kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
“Tanzania ni vyema ikaungana na nchi mbalimbali kupaza sauti juu ya kuhakikisha kila nchi inaheshimu na kutimiza ahadi zake juu ya kupunguza joto la dunia na kutoa fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi pamoja na athari zake, hususani madhara yanayojitokeza kwa nchi zinazoendelea ambazo bado viwango vyake vya uchafuzi ni mdogo sana,” amesema Mlay.
Amesema zaidi ni kuendelea kuhakikisha kama nchi inaendelea kuwa mstari wa mbele kuhakikisha rasilimali fedha zinazotolewa kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi zinawanufaisha watu wote, hususani wale ambao wako katika hatari kubwa ya athari za mabadiliko hayo.
Ikumbukwe, Tanzania iliwahi kuunga mkono hoja ya kuongezwa fedha za ufadhili kwa kuzingatia athari zinazozidi kuongezeka kwa sasa na kuhakikisha ahadi ya nchi zilizoendelea kutoa Dola bilioni 100 (Sh250 trilioni) kila mwaka kwa nchi zinazoendelea kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi zinatimizwa.
Jambo jingine Tanzania ilitaka kuhakikishwa uanzishwaji wa mfuko wa kupambana na majanga na maafa, kuhakikisha juhudi za kuelekea matumizi ya nishati safi zinakuwa jumuishi na mjadala wa masuala ya jinsia unazingatia maadili ya kitaifa na kijamii na wanawake wanapewa kipaumbele.