Kikao cha dharura cha viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kwa ajili ya kuunga mkono kadhia ya Palestina kilifanyika siku ya Jumatatu mjini Riyadh Saudi Arabia, ambapo msimamo wa pamoja unaolaani jinai za kinyama za utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Palestina Lebanon ulipitishwa katika taarifa ya mwisho ya kikao hicho.
Utawala wa Kizayuni ungali unaendelea kufanya mauaji ya halaiki na jinai za kutisha dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza na Lebanon. Moja ya sababu kuu za kuendelezwa jinai zisizo na mfano wake za utawala wa Kizayuni dhidi ya Gaza na Lebanon, ni uzembe na kutochukua nchi za Kiislamu na Kiarabu hatua madhubuti za kukabiliana na jinai hizi za kinyama zinazofanywa na utawala pandikizi wa Israel.
Katika kipindi cha miezi 14 iliyopita, nchi za Kiislamu na Kiarabu hazikuchukua hatua yoyote ya maana ya kuwaunga mkono watu wa Gaza wala kufanya lolote kwa ajili ya kuwatetea watu wa Lebanon katika siku 45 zilizopita. Uzembe huo pamoja na jamii ya kimataifa, na hasa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kushindwa kutekeleza majukumu yake dhidi ya utawala wa Kizayuni kumeufanya utawala huo umee pembe na kuendeleza jinai zake dhidi ya Gaza na Lebanon bila kujali lolote wala kuhofia kuadhibiwa kuhusiana na jinai hizo za kinyama dhidi ya Palestina na Lebanon.
Mkutano huo wa dharura wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu uliofanyika Jumatatu nchini Saudi Arabia, unaweza kuzingatiwa kuwa moja ya hatua chanya zenye taathira za kidiplomasia kwa ajili ya kuziunga mkono Gaza na Lebanon. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilipendekeza kufanyika mkutano wa dharura wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu, ambapo hatimaye iliamuliwa uwe mkutano wa pamoja wa jumuiya hiyo na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kwa pendekezo la Saudi Arabia.

Madhumuni ya kufanyika mkutano huo yalikuwa ni kujadili njia za kuchukuliwa msimamo mmoja wa kusimamisha uchokozi wa utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza na Lebanon. Kuhusiana na suala hilo, nchi zilizohudhuria mkutano huo zilitilia mkazo ulazima wa kulindwa haki za taifa la Palestina ikiwemo ya wakimbizi wa Kipalestina kurejea katika ardhi zao zinazokaliwa kwa mabavu na utawala bandia wa Israel. Zimesisitiza kwamba suala la Palestina ni sawa na la mataifa mengine yote yanayopigania uhuru na ukombozi wa ardhi zao.
Taarifa ya mwisho ya mkutano huo, imepinga hatua zozote za utawala wa Kizayuni za kutaka kuyahudisha Quds Mashariki (Jerusalem Mashariki), na kusema Quds ni mstari mwekundu kwa mataifa ya Kiislamu na Kiarabu.
Nukta nyingine ni kwamba Washiriki wa mkutano huo pia wamelaani vikali hatua za kiuadui za utawala wa Kizayuni dhidi ya Shirika la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA). Mohammed bin Salman, Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia, amesisitiza kuhusu suala hilo kwa kusema: “Tunalaani vikali hatua ya kupigwa marufuku shughuli za Shirika la Misaada kwa Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) katika maeneo ya Palestina na kuvurugwa shughuli za taasisi za misaada ya kibinadamu.” Msimamo huo unaonyesha kuwa nchi za Kiislamu na Kiarabu zinatilia maanani nyanja zote za jinai za utawala wa Kizayuni huko Gaza.
Jambo jingine ni kuwa, nchi zilizoshiriki kikao cha Saudia zimelaani kitendo cha jamii ya kimataifa cha kutochukua hatua yoyote dhidi ya jinai za utawala wa Kizayuni na kukitaja kuwa ni moja ya sababu za kuendelea jinai hizo za kinyama dhidi ya Wapalestina na Walebanon.

Kuhusiana na suala hilo, Rais Abdel Fattah al-Sisi wa Misri amesema: “Uchokozi wa Israel dhidi ya Gaza, Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Lebanon umekuwa ukiendelea kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa katika kivuli cha kimya cha jamii ya kimataifa. Sisi tunalaani vikali mauaji ya kikatili ya raia huko Gaza.”
Iwapo misimamo inayofaa ya kisiasa ya nchi za Kiislamu na Kiarabu kuhusu itatekelezwa kivitendo kwa ajili ya kukabiliana na jinai za utawala wa Kizayuni ni wazi kuwa utawala huo utalazimika kupunguza jinai zake dhidi ya Wapalestina na Lebanon. Hii ni kwa sababu matokeo muhimu ya utekelezwaji wa siasa hizo yatapelekea kutengwa kisiasa utawala huo wa Kizayuni Asia Magharibi na hivyo kuhatarisha uwepo wake katika eneo.