
KIPA wa Pamba Jiji, Yona Amos amesema ni ngumu kwake kutaja anahitaji kumaliza na clean sheet ngapi msimu huu kwenye Ligi Kuu Bara kutokana na presha ya mechi zilizosalia.
Pamba Jiji imebakiwa na michezo minne dhidi ya Simba iliyopo nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Bar, dhidi ya KenGold inayoburuzwa mkiani, JKT Tanzania (nafasi ya saba) na KMC (nafasi ya tisa).
“Mechi zilizosalia zina presha kubwa, hivyo siwezi kusema nataka kumaliza na clean sheet ngapi, zozote zitakazopatikana nitashukuru kwani itakuwa ndiyo riziki yangu kwa msimu huu,” alisema Amos na kuongeza:
“Jambo la msingi kwa sasa ni usalama wa timu, malengo ya mchezaji binafsi yatakuja baadaye kwani tupo nafasi ya 13 ambayo siyo salama sana kwetu, tunahitaji kupambana ili kushinda angalau mechi mbili na nyingine tupate sare tuwe salama.”
Amos ambaye ana clean sheet tisa kwenye ligi, alisema msimu huu umekuwa mgumu, ukiachana na KenGold iliyoonyesha kushuka mapema, timu ambazo hazipo katika nafasi nne za juu hazina uhakika wa kubaki.
“Ligi ilipofikia imegawanyika kwa timu zinazowania ubingwa, nafasi tatu za juu na sisi ambao tunajikwamua kushuka daraja, presha ni kubwa ila kama mchezaji nahitaji kutuliza akili ili kuisaidia timu,” alisema Amos.