
Dar es Salaam. Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema Serikali itaendelea kutoa nafasi ya ajira kwa wahitimu kila zinapopatikana, kwani siyo walimu pekee wanaokabiliwa na changamoto hiyo, bali hata tasnia nyingine kama waandishi wa habari.
Msigwa amesema hayo leo Machi Mosi, 2025 alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan mkoani Tanga, mkutano wa tatu wa nchi zinazozalisha kahawa na uwasilishaji taarifa juu ya miaka minne ya Samia madarakani.
Msigwa ametoa kauli hiyo siku chache tangu walipoibuka viongozi wa umoja wa walimu wasiokuwa na ajira Tanzania kuanzia mwaka 2015 hadi 2023 (Neto), wakiwamo mwenyekiti, Joseph Kaheza na katibu, Daniel Edgar katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, wakitaka mambo kadha ikiwa ni pamoja na kusitishwa usaili wa kada ya ualimu, utaratibu ambao Serikali imeanzisha hivi karibuni.
Februari 24, viongozi hao walikamatwa na Jeshi la Polisi ikilezwa umoja huo haujasajiliwa.
Akizungumza na wanahabari, Msigwa mbali na kueleza Serikali imekuwa ikitoa ajira za walimu kwa awamu kila mwaka pia amesema anashangazwa kusikia viongozi wa Neto walikamatwa na Jeshi la Polisi baada ya kuzungumza na wanahabari.
“Lakini walimu ambao hawajapata ajira si kwamba Serikali haijui inatambua na itaendelea kuajiri kwa namna ambavyo nafasi inaruhusu, kwa sababu tukisema tukimbilie kuajiri watu wote itabidi tuchukue hela za dawa, za maji, barabara ukalipe mishahara ya walimu,” amesema.
Amesema Tanzania hakuna tasnia ambayo watu wake wengi hawajapata ajira akitoa mfano wa waandishi wa habari wanaozalishwa kila mwaka ni zaidi ya 500 jambo ambalo pia lipo katika tasnia nyingine.
“Wapo maofisa maendeleo ya jamii hawajapata ajira, wako wahandisi, wachumi, wanasheria wengi, hivyo Serikali itaendelea kuajiri kila nafasi inapopatikana. Haitawezekana kila anayehitimu chuo aajiriwe, itakuwa ni Serikali ya kulipa mshahara.
“Maelezo yangu haya hayana maana ya kubeza madai ya walimu, yanafanyiwa kazi itakapokamilika mtajulishwa,” amesema.
Uhaba wa walimu
Mwaka 2023, madarasa ya awali na msingi pekee yalikuwa yanahitaji walimu zaidi ya 116,885 ili kuweka sawa uwiano wa walimu ikilinganishwa na wanafunzi waliokuwa wamedahiliwa.
Kwa mujibu wa Kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa 2023 kilichotolewa na Wizara ya Fedha, Juni 13, 2024 madarasa ya awali yalihitaji walimu 52,884 na shule za msingi zilihitaji walimu 64,001 ili kuwa na uwiano uliopangwa na Serikali.
Takwimu zinaonyesha, madarasa ya awali mwaka 2023 yalikuwa na walimu 9,608 pekee ikilinganishwa na uhitaji wa walimu 62,491 katika mwaka 2023 ambao walipaswa kufundisha wanafunzi 1,562,286.
Kwa mujibu wa uwiano wa Serikali, walimu waliokuwapo walifundisha wanafunzi 163 ndani ya darasa moja ikiwa ni mara sita zaidi ya kiwango kilichowekwa na Serikali cha kufundisha wanafunzi 25.
Hata hivyo, idadi ya walimu wa madarasa ya awali waliokuwapo mwaka 2023 ni pungufu kwa asilimia 4.8 kutoka wanafunzi 10,093 waliokuwapo mwaka 2022. Idadi hiyo ya walimu ilishuka katikati ya ongezeko la wanafunzi kwa asilimia 8.8.
Hiyo ni baada ya wanafunzi katika shule za awali za Serikali waliodahiliwa kufikia 1,562,286 kutoka wanafunzi 1,435,735 mwaka 2022.
Kitabu hicho cha hali ya uchumi kinaeleza idadi ya wanafunzi katika shule za Serikali ilikuwa milioni 10.82 mwaka 2023 ambayo ilikuwa ikihitaji zaidi ya walimu 240,541 ili kuweka uwiano wa mwalimu mmoja kwa wanafunzi 45.
Badala yake shule hizo zilikuwa na walimu 176,540 ambayo ni pungufu ya walimu 64,001 kufikia uwiano halisi.
Idadi ya walimu waliokuwapo mwaka 2023 ilikuwa ni ongezeko la asilimia 1.8 ikilinganishwa na walimu waliokuwapo mwaka 2022.
Wahitimu waliopo
Kuhusu wingi wa wahitimu, Ripoti ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania 2023 (TCU) iliyotolewa Mei, 2024 inaonyesha kozi hiyo imekuwa ikiongoza kwa kutoa wahitimu wengi kuliko nyingine.
Ripoti za miaka tofauti za TCU zinaonyesha mwaka 2023, walimu waliohitimu walikuwa 15,103, mwaka 2022 walikuwa 15,335, huku mwaka 2021 wakiwa 14,050.
Idadi ya wahitimu inaakisiwa na wingi wa wanaodahiliwa na mwaka 2023/2024 kati ya wanafunzi 106,570 waliodahiliwa kuanza mwaka wa kwanza katika kozi 17 zilizoainishwa, waliochagua ualimu walikuwa 27,731.
Ripoti ya mwisho ya Mpango wa hiari wa nchi za Afrika kujitathmini (APRM) iliyotolewa mwaka 2013 ililitaja suala la ukosefu wa ajira miongoni mwa changamoto zinazotakiwa kutafutiwa ufumbuzi, lakini hadi sasa utekelezaji wa pendekezo hilo haujafanyika kwa ufanisi, hali inayosababisha kuongezeka kwa kundi la vijana wasio na ajira.
Julai 11, 2024 wakati wa mkutano wa awali kabla ya kufanyika kwa tathmini nyingine ya APRM, Mkurugenzi wa Kituo cha Taarifa kwa Wananchi (TCIB), Deus Kibamba alilieleza Mwananchi kuwa Tanzania ina cha kujifunza kwa kilichotokea katika nchi nyingine za Afrika, ikiwa ni matokeo ya vijana kukosa ajira.
Alisema nchi inapokuwa na vijana wengi wasio na ajira ni rahisi kushawishika kufanya mambo yasiyofaa, akitoa mfano wa maandamano yaliyofanywa na vijana wa Gen Z nchini Kenya na yanayofanana na hayo katika nchi nyingine za Afrika.
“Ripoti ya APRM 2013 ilieleza suala la ajira hasa kwa vijana ni bomu ambalo lisipotafutiwa ufumbuzi linaweza kutuharibia utulivu na amani ambayo tumekuwa nayo kwa miaka mingi. Sasa tunapoelekea kwenye maandalizi ya kufanya tathmini ya pili ni muhimu suala hili likapewa kipaumbele,” alisema.