
Dar es Salaam. Serikali imewataka wananchi kutoangalia faida zinazopatikana kwa Shirika la ndege Tanzania (ATCL), kwa watu wanaokata tiketi peke yake, kwani linachangia kukuza sekta nyingine ikiwemo utalii.
Hayo yamesemwa leo Jumamosi na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa, katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika katika Hifadhi ya Mikumi, mkoani Morogoro.
Msigwa amesema watalii wengi hawaji nchini kwa mabasi bali kwa ndege na wachache kwa meli, eneo ambalo pia Serikali imeanza kulifanyia kazi.
Akielezea ufanisi wa sekta ya utalii nchini, Msigwa amesema idadi ya watalii imeongezeka kutoka 822, 232 mwaka 2021/2022 hadi kufika abiria 1,323,696 kwa mwaka 2023/2024.
“Najua kuna mjadala ikija ripoti ya CAG inaonyesha pengine tunapata hasara, shirika letu kumbukeni Watanzania lilikuwa limekufa kabisa, hivyo unapokuja kulifufua huwezi kufufua kupata faida hapohapo, utakuwa polepole na kadiri muda unapokwenda ile hasara itazidi kupunguza na mwisho tutaanza kupata faida .
“Hivyo naomba kusisitiza , tunapozungumza faida za shirika la ndege msiangalie faida za tiketi za abiria, kwani faida nyingine ni pamoja na kuimarisha utalii,” amesema Msigwa.
Ameeleza kuwa ni vizuri Watanzania wakawa na hiyo picha kwamba shirika hilo ndilo linalowawezesha leo kutarajia ujio wa watalii zaidi ya 2500 mwaka huu ambapo huko nyuma mwaka 2020 kulikuwa na watalii 620.
“Pia leo unazungumzia nchi kufikisha watalii milioni mbili, rekodi ambayo haijawahi kufikiwa huwezi kuacha kulitaja shirika hilo,” amesema Msigwa.
Msemaji huyo amesema ni kwa kulitambua hilo, SerIkali imefanya uwekezaji mkubwa katika ununuzi wa ndege na mpaka sasa kuna ndege 16 zinazotoa huduma ndani na nje ya nchi na tayari wameshafikia vituo 25.
“Hivi karibuni tumeanza kwenda Afrika Kusini. Hili ni eneo la kimkakati sababu kuna idadi kubwa ya watalii ambao wanakuja Afrika kupitia Afrika Kusini kwa hiyo tumepeleka ndege zetu za ATCL ambazo zinafanya safari tano kwa wiki, tunaleta watalii,” amesema Msigwa.
Ameongeza kuwa ndege zilizopelekwa huko ni mpya na kueleza kwamba watalii hawa wanapofanya utalii, wanaangalia vitu vingi ikiwemo usalama na hata ukienda kwenye shirika la ndege duniani, wastani wa usalama kwa ndege za ATCL ni asilimia 60 , lakini zipo za asilimia 87.
Msigwa amewataka wananchi kupuuza siasa kuwa ndege hizo hazipo salama, kwani sasa Serikali inachotafuta ni kwenda kutua kila mahali na kununua ndege nyingi zaidi.
“Hao wanaosema tumezuiwa msipate shida, hata China haikuwa rahisi tumetumia karibu miaka sita kupata kibali kwenda huko, Afrika Kusini tumetumia zaidi ya miaka mitatu, kwa hiyo ni michakato ya kawaida, tutaendelea kuomba vibali kwenda nchi mbalimbali.
“Tunakwenda China, tunakwenda India, tutakwenda Ulaya , tutakwenda Marekani, tutakwenda Amerika ya Kusini , kila mahali, tunaendelea kulikuza shirika kila mahali kwa sababu tunapotaka kwenda kufikia idadi kubwa ya watalii lazima shirika letu liwe na safari za moja kwa moja kwenda kwenye maeneo yote ambapo tunawategemea watalii,” amesema Msigwa.