
Ukiziweka kando Simba na Yanga zilizocheza mechi 22 kila moja, timu zingine zinazoshiriki Ligi Kuu Bara msimu huu zimeshuka dimbani mara 23 na kubakiwa na mechi saba kumaliza msimu. Simba na Yanga zina nane.
Wakati ligi ikielekea ukingoni, kuna vita nyingi zikishindaniwa lakini upande wa kumsaka Mchezaji Bora wa Msimu (MVP), mambo yanaonekana kuwa moto huku ikiwahusisha nyota ambao wamewahi kubeba tuzo hiyo walipotoka.
Jean Charles Ahoua, nyota wa zamani wa Stella Club d’Adjamé, alikuwa MVP wa Ligi Kuu ya Ivory Coast msimu uliopita 2023-2024. Msimu huu anaifukuzia tuzo hiyo akiitumikia Simba na hadi sasa amehusika kwenye mabao 18, akifunga 12 na asisti nane.
Stephane Aziz Ki ndiye alikuwa MVP msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara na nyota huyo pia alikuwa mfungaji bora akifunga mabao 21 na asisti nane, jumla alikuwa na mchango wa mabao 28. Kumbuka Aziz Ki amewahi kuwa MVP wa Ligi Kuu ya Ivory Coast msimu wa 2021-2022 kabla ya kutua Yanga.
Rekodi zinaonyesha katika misimu mitatu nyuma, Tuzo ya MVP Ligi Kuu Bara imebebebwa na nyota wa Yanga, Yannick Bangala (2021-2022), Fiston Mayele (2022-2023) na Stephane Aziz Ki (2023-2024) na wote ni wa kigeni. Safari hii itakuwaje?
Ni nadra kuona mchezaji mwenye mchango mkubwa wa mabao kuikosa Tuzo ya MVP jambo linaloonyesha wazi msimu huu kwa wale nyota waliofunga na kuasisti mara nyingi hadi sasa ndiyo wana vita ya kuwania tuzo hiyo.
Wakati vita hiyo ya MVP ikikolea, hapa kuna uchambuzi wa namna ambavyo wachezaji walivyochangia mabao katika timu zao Ligi Kuu Bara msimu huu, wakiwemo nyota wanaotajwa huenda mmojawapo akawa MVP.
Ikumbukwe, Ligi Kuu Bara imesimama baada ya juzi kupigwa mechi ya kiporo kati ya Simba na Dodoma Jiji, ili kupisha kalenda ya mechi za kimataifa kwa timu za taifa zinazochuana kusaka tiketi ya kufuzu ushiriki wa fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2026.
Watetezi Yanga wapo kileleni wakikusanya pointi 58, nyuma ya watani zao wa jadi Simba mwenye 57, baada ya zote kucheza michezo 22, huku matajiri wa Jiji la Dar es Salaam Azam FC iliyocheza mechi 23, ikishika nafasi ya tatu na pointi 48.
Singida Black Stars iliyocheza pia michezo 23, ni ya nne na pointi 44, KenGold inaburuza mkia na pointi 16, ikifuatiwa na Tanzania Prisons iliyopo ya 15 na pointi 18, wakati Kagera Sugar iko ya 14 na pointi 19 zikipambana kutoshuka daraja.
Wakati Ligi Kuu ikienda mapumziko hadi Aprili Mosi, wapo baadhi ya mastaa wa timu mbalimbali waliotengeneza pacha hatari hadi sasa kutokana na mchango wao wa upatikanaji wa mabao, kama Mwanaspoti linavyowaelezea kwa kina na walichokifanya.
DUBE, MZIZE, PACOME (YANGA)
Hii ni moja ya safu kali hadi sasa katika Ligi Kuu Bara kwani nyota hao wote watatu wamechangia upatikanaji wa mabao 43 kati ya 58, yaliyofungwa na timu hiyo nzima inayoongoza kwenye msimamo na pointi 58, nyuma ya watani zao Simba wenye 57.
Clement Mzize amechangia mabao 13, baada ya kufunga 10 na kuasisti matatu, huku Prince Dube akichangia 17, akifunga pia 10 na kutoa asisti saba, wakati Pacome Zouzoua amefunga mabao saba na kuchangia upatikanaji wa mengine sita ‘Asisti’.
AHOUA, MUKWALA, ATEBA (SIMBA)
Nyota hao kwa pamoja wamechangia upatikanaji wa mabao 42, kati ya 52 yaliyofungwa na kikosi kizima na Ahoua anayeongoza kwa ufungaji hadi sasa, amechangia mabao 18, baada ya kufunga 12 na kuchangia mengine sita ‘Asisti’.
Steven Mukwala amehusika katika upatikanaji wa mabao 13, katika kikosi hicho baada ya kufunga tisa na kuchangia manne ‘Asisti’, huku kwa upande wa nyota mshambuliaji mwenzake, Leonel Ateba akichangia 11, akifunga nane na kuasisti matatu.
FEI TOTO, SILLAH, NADO (AZAM FC)
Feisal Salum ‘Fei Toto’ pekee katika kikosi cha matajiri wa Jiji la Dar es Salaam Azam FC, amechangia mabao 16 ya Ligi Kuu msimu huu, baada ya kufunga manne na kutoa pasi za mabao mengine 12 ‘Asisti’, akiwa ndiye kinara katika eneo hilo.
Gibril Sillah anafuatia akiwa amechangia mabao tisa baada ya kufunga saba na kuasisti mawili, huku Idd Seleman ‘Nado’ akichangia saba akifunga manne na kutoa pasi tatu ‘Asisti’, hivyo kuchangia mabao 32 kati ya 36 ya timu nzima.
RUPIA, SOWAH, TCHAKEI (SINGIDA BS)
Kwa pamoja nyota hao wamechangia mabao 26 kati ya 32 yaliyofungwa na kikosi hicho hadi sasa katika Ligi Kuu Bara na Mkenya Elvis Rupia ndiye anayeongoza kwa kuchangia mabao 11, baada ya kufunga tisa na kusaidia mengine mawili ‘Asisti’.
Mshambuliaji mwenzake, Jonathan Sowah aliyejiunga na timu hiyo katika dirisha dogo la Januari mwaka huu akitokea Al-Nasr Benghazi ya Libya, tayari ameonyesha umwamba wa kucheka na nyavu kwani amefunga mabao saba kwenye mechi saba alizocheza.
Kiungo mshambuliaji nyota wa kikosi hicho raia wa Togo, Marouf Tchakei amehusika katika mabao manane ya timu hiyo baada ya kufunga matano na kuchangia mengine ‘Asisti’ matatu, hivyo kuifanya timu hiyo kushika nafasi ya nne na pointi 44.
CHIKOLA, MAKAMBO, YACOUBA (TABORA UNITED)
Unapotaja miongoni mwa nyota wa Tabora United waliokuwa katika kiwango kizuri hadi sasa, hatoacha kulitaja jina la Offen Chikola ambaye ndiye anayeongoza kwa kupachika mabao mengi kikosini humo, akiwa na saba na kuchangia mawili ‘Asisti’.
Mkongomani Heritier Makambo amechangia mabao tisa ya timu hiyo baada ya kufunga matano na kuchangia pia manne ‘Asisti’, huku kwa upande wa nyota mwenzake, Yacouba Songne waliowahi kucheza wote Yanga akifunga mabao manne na kuasisti matatu.
Kijumla nyota hao wamechangia mabao 25 ya Ligi Kuu Bara kati ya 27, ndani ya kikosi hicho kilichopo nafasi ya tano na pointi zake 37, baada ya kushinda michezo 10, sare saba na kupoteza sita kati ya 23, iliyocheza hadi sasa msimu huu.
EDGAR, MUKONO, KIHIMBWA (FOUNTAIN GATE)
Nyota wote wamechangia upatikanaji wa mabao 19 katika kikosi hicho kati ya 28 yaliyofungwa na timu nzima na Salum Kihimbwa pekee aliyekuwa kwenye kiwango bora akiwa amechangia tisa msimu huu, baada ya kufunga manne na kuasisti matano.
Mshambuliaji Edgar William anayekabiliwa na ukame wa mabao hadi sasa, amefunga matano sawa na kiungo mshambuliaji raia wa Burundi, Elie Mokono aliyefunga pia matano na kuifanya timu hiyo kushika nafasi ya saba kwenye msimamo na pointi 28.
Kabla ya hapo timu hiyo ilikuwa inaongozwa na mshambuliaji nyota, Seleman Mwalimu aliyechangia mabao saba, akifunga sita na kuasisti moja, japo kiwango chake bora kiliwavutia Wydad Casabalanca ya Morocco na kumsajili rasmi Januari mwaka huu.
BWENZI, MISHAMO, LUKINDO (KENGOLD)
Licha ya KenGold kuburuza mkiani mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara na pointi 16, baada ya kucheza michezo yake 23, ila nyota watatu wa kikosi hicho wamechangia upatikanaji wa mabao 17, kati ya 20 yaliyofungwa na timu hiyo msimu huu hadi sasa.
Mishamo Michael ndiye nyota aliyechangia mabao mengi ndani ya timu hiyo katika Ligi Kuu Bara, baada ya kufunga matano na kuasisti mawili, akifuatiwa na Selemani Bwenzi aliyehusika na sita, akifunga matano na kuchangia lingine moja ‘Asisti’.
Bwenzi aliyejiunga na kikosi hicho katika dirisha dogo la Januari mwaka huu akitokea Mbeya Kwanza inayoshiriki Ligi ya Championship, amekuwa muhimili mkubwa wa timu hiyo hadi sasa inayopambania vita ya kubaki na kuepuka kurejea ilipotoka.
Mshambuliaji mwingine ni Herbert Lukindo aliyechangia mabao manne hadi sasa, baada ya kufunga matatu na kuasisti moja, ingawa kabla ya hapo alikuwa nyota mwingine wa timu hiyo, Joshua Ibrahim aliyefunga manne kisha kujiunga na Namungo FC.
LWASA, DATIUS, MKANDALA (KAGERA SUGAR)
Wakati Kagera Sugar ikipambana kutoshuka daraja, ila moja ya kiungo mshambuliaji anayefanya vizuri ni Mganda Peter Lwasa ambaye hadi sasa ndiye kinara wa mabao kikosini humo, baada ya kufunga manane ikiwa ndiyo kwanza msimu wake wa kwanza.
Nyota huyo amejiunga na Kagera Sugar msimu huu akitokea KCCA FC ya kwao Uganda na hadi sasa ameonyesha kiwango kizuri na kutengeneza uelewano mzuri eneo la ushambuliaji na beki, Datius Peter anayecheza zaidi winga ya kulia akitokea pembeni.
Datius msimu huu amechangia mabao manne ya timu hiyo baada ya kufunga moja na kuasisti matatu, akifuatiwa na kiungo wa timu hiyo, Cleophace Mkandala aliyefunga mawili na wote kuhusika na mabao 14, kati ya 18, yaliyofungwa na kikosi chote.