Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran: Gaza imekuwa kaburi la watoto

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amesema kuwa, Ukanda wa Gaza umegeuka kuwa kaburi la watoto kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara ya utawala unaofanya mauaji ya kimbari wa Israel.

Ismail Baqaei ameandika kwenye mtandao wa kijamii wa X sambamba na maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Watoto kwamba Novemba 20, Siku ya Kimataifa ya Watoto, ni ukumbusho wa haki ya watoto wote kuishi katika amani na usalama.

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran ameeleza kuwa, siku hili ni fursa ya kuona machungu na mateso wanayopata watoto wa Gaza na kusema kuwa, tangu tarehe 7 Oktoba 2023, zaidi ya watoto elfu 17 wa Kipalestina wameuawa shahidi, maelfu ya watoto wametoweka, makumi ya maelfu ya watoto wameojeruhiwa, zaidi ya watoto elfu 35 wamekuwa mayatima au wamepoteza wanafamilia wao wote.

Baqaei ameongeza kuwa, karibu watoto 4,000 wa Kipalestina wamefariki dunia kutokana na njaa na wengine wengi wako hatarini kutokana na njaa, maradhi, ukimbizi na ukosefu wa mahitaji muhimu.

Watoto wa Gaza

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amesisitiza kuwa, kama alivyoripoti Francesca Albanese, Ripota Maalumu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Palestina, mamia ya watoto na vijana wa Kipalestina wamekuwa wakitekwa nyara na jeshi la Israel kila mwaka katika miongo kadhaa iliyopita. 

Akieleza ukweli kwamba kuwaua na kuwatesa watoto wasio na hatia wa Kipalestina kumesababisha majeraha makubwa katika dhamiri za binadamu, mwanadiplomasia huyo wa Iran ameongeza kuwa, wakati umefika kwa walimwengu kukomesha jinai za kutisha dhidi ya watoto wa Kipalestina.