
ALIYEWAHI kuwa Ofisa Habari wa Mlandizi Queens, Sajda Sadick amesaini mkataba wa mwaka mmoja na Trident Queens inayoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake nchini Zambia.
Alisajiliwa kwenye timu hiyo akitokea Mlandizi ambako alihudumu kama msemaji wa timu na hajawahi kucheza timu za Ligi Kuu Tanzania zaidi ya Kinondoni Queens ligi ya mkoa akiwa kama mshambuliaji.
Akizungumza na Mwanaspoti, Sajda alisema hii ni mara ya kwanza kucheza soka nchini Zambia kwani kabla hakuwahi kwenda nje.
Mwanaspoti ilipomuuliza timu hiyo ilimuonaje hadi kumpa mkataba licha ya kwamba hakuwahi kucheza Ligi Kuu, alijibu: “Mimi ni mfano wa Kelvin De Bruyne wakati anaenda Man City hakutafutwa, aliambatanisha vitu vyake na kutumia CV zake kwenye menejimenti ya timu, hiyo ndio inaendana na ishu yangu mimi,” alisema na kuongeza:
“Kwahiyo nilituma CV zangu kwenye klabu mbalimbali sio moja, ikiwamo TP Mazembe, lakini waliniambia mwisho wa msimu huu wangeniita kufanya majaribio, sikusubiria ndio nikapata Zambia.”