
Dar es Salaam. Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imetoa muda wa wiki moja kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kiwe kimewasilisha maelezo kuhusu malalamiko ya mjumbe wa Baraza Kuu wa chama hicho, Lembrus Mchome.
Mchome aliwasilisha malalamiko kwa msajili wa vyama akilalamikia kikao cha Baraza Kuu Taifa kilichofanyika Januari 22, 2025 kwamba kilikuwa batili kwa sababu hakikutimiza masharti ya Katiba ili kuwa kikao halali.
Pia, Mchome alidai kikao hicho ndani ya ukumbi walikuwepo wanachama ambao siyo wajumbe na baadhi ya watu hao walipiga kura kinyume na matakwa ya katiba ya chama hicho.
Barua iliyosainiwa na Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Sisty Nyahoza imekitaka Chadema kujibu barua ya Mchome kwa muda usiozidi Machi 31, 2025.
Kwa mujibu wa Nyahoza ili msajili aweze kuchukua hatua stahiki kuhusu malalamiko hayo lazima majibu ya Chadema yawepo.
Leo Jumatatu Machi 24, 2025 akizungumzia hatua iliyofikiwa dhidi ya malalamiko ya Mchome, Nyahoza amesema, “tayari tumeiandikia barua Chadema kuanzia leo walete maelezo, utaratibu ni kwamba ukilalamikiwa ukapewa barua na wewe ujibu, tumewapa wajibu hadi Machi 31 na Mchome tumempatia nakala,” amesema Nyahoza.
Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa Chadema, Brenda Rupia amethibitisha chama hicho kupokea barua hiyo akisema watajibu ndani ya muda. “Tumepokea barua kutoka kwa msajili na ametupatia muda wa kujibu na tutaijibu kwa wakati,”amesema.
Anacholalamika Mchome
Malalamiko ya Mchome kwa Chadema ni kupinga uteuzi wa viongozi wa juu na wajumbe wa Kamati Kuu ulioufanywa na Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Tundu Lissu Januari 22, 2025, akidai umekiuka katiba ya chama hicho.
Mchome katika barua yake amelalamikia uteuzi wa vigogo wa chama hicho Katibu Mkuu, John Mnyika, Aman Golugwa (Naibu Katibu Mkuu – Bara) na Ally Ibrahim Juma (Naibu Katibu Mkuu – Zanzibar) akidai waliidhinishwa bila akidi ya kikao cha Baraza Kuu kutimia.
Katika barua ya malalamiko yake, Mchome aliwataja wajumbe wa Kamati Kuu walioteuliwa na kuidhinishwa na kikao hicho ni Godbless Lema, Rose Mayemba, Salma Kasanzu, Hafidh Ally Saleh na Dk Rugemeleza Nshala, akidai uteuzi wao ni batili.