Msaga Sumu afunguka ya moyoni, ataja uhuni kwenye Singeli

Dar es Salaam, Linapokuja suala la nani mfalme wa Singeli nchini, siku zote Seleman Jabir ‘Msaga Sumu’ hudai hakuna zaidi yake.  Akizungumza na Mwananchi msanii huyo amezungumza mengi kuhusiana na muziki huo.

Anasema namna alivyoutambulisha muziki huu wa Singeli katika jamii hadi sasa unatamba haikuwa kazi rahisi na alitokea kwenye ‘Kigodoro’, huku wengi waliona ni muziki wa kihuni hivyo ilikuwa ngumu kueleweka.

“Hii wengi hawajui lakini ukweli, mimi ndiye mwanzilishi wa muziki wa kigodoro, yaani zamani ukitaka Kigodoro basi ukimkosa Msaga Sumu umekosa burudani.

“Baada ya hapo ndipo nikaanzisha muziki wa Singeli japo mwanzo ilikiwa ngumu sana kueleweka kwa sababu tulikuwa hatujawekewa mazingira mazuri, ulikuwa unaonekana wa uswahilini sana, lakini tukapambana ukaeleweka na kuheshimiwa, japo bado baadhi ya watu wana fikra za kusema ni wa kihuni.

MS01
MS01

‘Madogo’ ndio wameleta uhuni kwenye Singeli

“Hili neno ‘Muziki wa kihuni’ limesababishwa na wadogo zangu niliowatangulia. Mimi niliimba na kundi la wahuni wengi sana japo hawakuwa wakifanya fujo, wala kushika silaha kama panga, visu au sime kwenye shoo. Pia hawakuwa unaona wanaume wakivua mashati na wadada kuvua nguo.

“Lakini baada ya kupumzika kidogo ndiyo wakaja wadogo zangu hawa na swaga zao za kusema “Toa pangaaaa… Mwaga majiiii… Toa kisuuuu… Vua shatiiiii… Hapo ndiyo wakawateka wahuni na hayo maneno yakaonekana kuhamasisha uhalifu na kuonekana ni muziki wa kihuni.”

MS02
MS02

Bifu kwenye Singeli zinawapoteza

“Unajua mimi kwanza nashangaa sana hizi bifu za wasanii wa Singeli zinatokea wapi, kwa sababu ukiangalia tupo wachache, badala ya kushirikiana na kupendana tuwe kitu kimoja, kila mmoja anavimba na kujiona ni zaidi ya mwezake.”

“Unajua kwanza walianza kuungana na kunifanyia bifu mimi, waliponishindwa wamekuwa wanafanyiana wenyewe kwa wenyewe, isitoshe mimi naangalia maisha kuliko bifu, tatizo pia hawa watoto waliokuwa wametamba na nyimbo zao mbili mbili nao wakaanza kuwekeana mabifu na mwishowe wamepotea. Wao walidhani wamemaliza. Mimi nishauri tu waache kudharauliana, wapendane na washikamane.

“Mimi kuna kipindi cha nyuma niliacha kutoa nyimbo baada ya kuona kuna kuigana, wasanii wanashindwa kuwa wabunifu badala yake wote tukawa tunaonekana hatuna kitu chochote sababu ya kuigana igana tu kuimba.

MS03
MS03

Ukimya wake una kishindo, subirini

“Mimi sio tu nipo kimya kwenye muziki, ninaangalia alama za nyakati. Naangalia muziki unaelekea wapi na sitaki  kuuharibu ufalme wangu wa Singeli.

“Nina nyimbo nyingi sana nishazitunga na nina kipaji cha kutunga hata mtu atokee hapa sasa hivi aniambie nitunge nyimbo kuhusu kitu natunga na wimbo ukafanya vizuri, hivyo nikikaa kimya hivi ndiyo wanasema nimefulia kabisa, kumbe mwenzao huwa najitungia sheria zangu huku nikiwaangalia wao wanachofanya.”

Wanasingeli sikieni ushauri

“Ushauri wangu mimi kwa wanamuziki wenzangu wa Singeli ni kujali sana heshima kwa watu wanaowazunguka kwenye kazi zetu, kwenye huu muziki ukiwa na heshima unaweza kufika mbali, kwa kuwa heshima ndiyo kila kitu.

“Lakini hawa wasanii wa singeli wengi wanafeli kwa sababu heshima hawana, wanajifanya wanavimba kutokana na nyimbo zao moja moja walizokuwa nazo.”