Mrithi wa Askofu Sendoro kujulikana Machi 10, wachungaji wanamtaka huyu

Mwanga. Dayosisi ya Mwanga ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) inatarajia kufanya mkutano mkuu maalumu wa uchaguzi, Machi 10, 2025, ili kumpata mrithi wa aliyekuwa askofu wa Dayosisi hiyo, Chediel Sendoro.

Dayosisi hiyo inafanya uchaguzi wa Askofu ikiwa ni miezi sita imepita tangu Askofu Sendoro afariki dunia kwa ajali, hivyo nafasi hiyo kubaki wazi.

Askofu Sendoro alifariki dunia Septemba 9, 2024 kwa ajali ya gari iliyotokea katika eneo la Kisangiro, Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro saa 1:30 usiku, baada ya gari alilokuwa akiendesha aina ya Toyota Prado, akitokea Kileo kuelekea nyumbani kwake Mwanga, kugongana uso kwa uso na lori.

Historia inaonyesha, Askofu Sendoro ndiye wa kwanza wa Dayosisi ya Mwanga ambaye  aliingizwa kazini Jumapili ya Novemba 6,2016 baada ya kuzaliwa kwa dayosisi hiyo mpya iliyotokana na kugawanywa kwa iliyokuwapo awali ya mama ya Pare.

Akizungumza na Mwananchi, leo Alhamisi Machi 6,2025, Katibu Mkuu wa Dayosisi ya Mwanga, Mathias Msemo amesema mkutano mkuu maalumu utafanyika Jumatatu Machi 10, 2025, na utakuwa na ajenda moja ya uchaguzi.

“Uchaguzi wa Askofu ni Jumatatu Machi 10, 2025, na usingetokea ule msiba kusingekuwepo na uchaguzi, kwani Askofu Sendoro bado alikuwa hajamaliza kipindi chake, alishahudumu kwa miaka minane,” amesema Katibu Mkuu.

Aidha amesema kwa taratibu zilizopo, Askofu anakaa madarakani kwa kipindi cha miaka 10 na baada ya hapo unafanyika mkutano mkuu ambapo anapigiwa kura ya imani na akishinda anahudumu hadi umri wa kustaafu.

“Kwa taratibu zetu Askofu anakaa miaka 10 na baada ya miaka hiyo anapigiwa kura ya imani akishinda anakaa hadi muda wa kustaafu, na wakati anafariki Askofu Sendoro alikuwa amekaa miaka minane na alikuwa aende mpaka 2026, ndipo ufanyike mkutano mkuu apigiwe kura ya imani,” amesema Msemo.

Amesema kwa mujibu wa katiba umri wa kustaafu Askofu ni miaka 65 kwa hiari na kwa lazima ni miaka 70.

Haya hapa matamanio ya Wachungaji

Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti baadhi ya wachungaji wa Dayosisi hiyo, wameeleza namna miaka minane ya Askofu Sendoro ilivyokuwa ya mafanikio na kusema kuwa, wanatamani kumpata Askofu mpya ambaye ataweza kuvaa viatu vya mtangulizi wake.

Mkuu wa Jimbo la Mision la dayosisi hiyo, Mchungaji Deogratius Msangi amesema wanaendelea kumuomba Mungu, ili awape Askofu ambaye atasimama vyema kwenye nafasi hiyo na kuendeleza huduma ambazo zilianzishwa na Askofu Sendoro enzi za uhai wake.

“Tunaendelea kuweka jambo hili mikononi mwa Mungu kwa sababu ni miezi sita tangu baba askofu apumzike ni muda mfupi sana, na enzi za uhai wake alitenda mambo makubwa na mingine aliyaweka kwenye mipango yake, lakini kikubwa tunamuomba Mungu atusaidie tuweze kumpata Askofu mwingine ambaye atafuata nyayo za baba askofu Sendoro,” amesema Mchungaji Msangi.

“Ingawa bado tupo kwenye changamoto kubwa mawazo mengi kufikiri kwamba labda ni yupi, lakini bado tuna matazamio kuwa Mungu atatupa kiongozi mzuri na mwema,” amesema.

Amesema ipo miradi iliyoanzishwa na Askofu Sendoro ikiwemo ya vitega uchumi vya Dayosisi na maono yake makubwa ilikuwa ni kuendeleza mshikamano wa Wanamwanga waliopo Mwanga na wale walioko nje ya dayosisi hiyo, hivyo wanatamani ajaye aendeleze hayo kwa wivu mkubwa wa maendeleo ya dayosisi.

“Pia alijenga upendo, pamoja na changamoto ambazo wakati mwingine watu wanakutana nazo kama binadamu lakini yeye alihamasisha upendo na tunatamani tumpate askofu wa namna hiyo, mwenye moyo wa upendo kwa wote na watumishi wenzake”amesema Mchungaji Msangi.

Mchungaji wa usharika wa Mgagao, Charles Tenga amesema wanatamani kumpata askofu ambaye ataweza kuvaa viatu vya Sendoro na kuhakikisha anasimama kiroho, kufanya maendeleo ya Dayosisi na kuwa kiunganishi.

“Askofu Sendoro alikuwa wa kiroho, alipenda maombi na aliweka makongamano ya maombi ambayo yalisaidia sana kuwajenga wananchi kiroho, hivyo tunatamani tumpate askofu ambaye ataweza kuliongoza kanisa kimaombi”amesema Mchungaji Tenga.

Amesema:”Pia sisi kama wachungaji tunatamani tumpate Askofu ambaye atasimama kama  mchungaji wa wachungaji,  asiwe mtawala wa wachungaji, awe ambaye atachunga wachungaji wenzake”.

Mchungaji wa Usharika wa Msangeni, Anituja Msuya amesema wanatamani kumpata Askofu mnyenyekevu, mpatanishi na mwenye ushirikiano na watu wote

Mchungaji Msuya ambaye pia ni Mratibu wa kitengo cha jinsia, wanawake na watoto katika Dayosisi hiyo, amesema wanatamani pia kumpata Askofu ambaye atakuwa mfuatiliaji bila ubaguzi kama alivyokuwa mtangulizi wake.

“Tunatamani Askofu atakayekuja aweze kuendeleza ndoto za Sendoro, alitufundisha kusameheana, alijali na kuwathamini wachungaji wenzake, lakini pia alipenda watoto na alianzisha uimbaji wa Askofu na watoto na ulikuwa na mafanikio makubwa, na haya yote tunatamani yaendelezwe,” amesema Mchungaji Msuya.

Ameongeza:”Tukumbuke pia wakati anakuja Askofu Sendoro  ndipo tulitoka kwenye mgogoro lakini aliondoa  makundi na kutuunganisha pamoja na kusonga mbele, alikuwa msema kweli na muwazi na alikuwa mpatanishi tunatamani ajaye aweze kufuata haya na endelezeni huduma zilizoanzishwa  na Sendoro.”