Mrithi wa Askofu Sendoro kuingizwa kazini Julai 13

Moshi. Mchungaji Daniel Mono ambaye alichaguliwa kuwa Askofu mteule wa Dayosisi ya Mwanga ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) kumrithi hayati Askofu Chediel Sendoro, anatarajiwa kuingizwa kazini Julai 13, 2025.

Mchungaji Mono ambaye ni Msaidizi wa Askofu wa Dayosisi ya kusini Mashariki ya Ziwa Victoria (DKMZV) alichaguliwa Machi 10, 2025 katika mkutano mkuu maalumu ambapo alipata kura 127 za ndio sawa na asilimia 96.2, kati ya kura 132 zilizopigwa, huku kura za hapana zikiwa ni tano.

Msemo amesema Jumamosi ya Julai 12, saa 10 jioni itafanyika ibada ya kubariki vifaa vya kiaskofu.

“Askofu mteule ataingizwa kazini Julai 13, 2025 katika Kanisa Kuu Mwanga, lakini ibada hiyo itatanguliwa na ibada ya kubariki vifaa vya uaskofu Jumamosi ya Julai 12 saa 10 jioni” amesema Msemo.

Ameongeza kuwa, “Machi 24, mwaka huu, tunatarajia Askofu mteule atakuja Mwanga, lakini Machi 12 ni ibada ya kubariki vifaa na Machi 13 ni ibada ya Wakfu. Kiutaratibu pamoja na kwamba watakuwepo maaskofu wengi siku hiyo ya kuingizwa kazini Askofu, lakini wataongozwa na Mkuu wa Kanisa”.

Akizungumza na Mwananchi, Dk Mono amesema anamshukuru Mungu kwa nafasi hiyo mpya na kueleza kuwa ni neema ya Mungu yeye kupewa wito huo.

“Nashukuru Mungu kwa kila jambo. Askofu Sendoro alifanya kazi kubwa sana ndani ya muda mfupi. Mimi sikustahili kabisa kupewa wito huu, bali ni neema ya Mungu,” amesema Dk Mono.

Ameongeza kuwa, “naamini Mungu ana kusudi lake hivyo wana Mwanga waendelee kumwamini Mungu, kumwomba, kumtegemea, kushirikiana na kujitoa kwa kila hali. Tunaendelea kupiga hatua”.

Mkutano wa uchaguzi ambao uliongozwa na Mkuu wa KKKT, Dk Alex Malasusa, ulihudhuriwa pia na viongozi mbalimbali akiwepo waziri mkuu mstaafu, Cleopa Msuya na Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Mwanahamisi Munkunda.

Dayosisi ya Mwanga imefanya uchaguzi wa Askofu ikiwa ni miezi sita imepita tangu Askofu Chediel Sendoro afariki kwa ajali, hivyo nafasi hiyo kubaki wazi.

Askofu Sendoro ambaye alihudumu kama Askofu wa Mwanga kwa miaka minane, alifariki dunia Septemba 9,2024 kwa ajali ya gari iliyotokea katika eneo la Kisangiro, Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro saa 1:30 usiku, baada ya gari alilokuwa akiendesha aina ya Toyota Prado, akitokea Kileo kuelekea nyumbani Mwanga, kugongana uso kwa uso na Lori.

Historia inaonyesha kuwa, Askofu Sendoro ndiye Askofu  wa kwanza wa Dayosisi ya Mwanga ambaye  aliingizwa kazini Jumapili ya Novemba 6,2016 baada ya kuzaliwa kwa Dayosisi hiyo mpya iliyotokana na kugawanywa kwa Dayosisi ya Pare.

Dk Mono ni nani

Mchungaji Daniel Mono, alizaliwa Julai 15,1975, akiwa ni mtoto wa sita kuzaliwa katika familia ya watoto saba.

Dk Mono baada ya elimu ya sekondari alipata elimu ya juu katika vyuo mbalimbali ambapo 2013 hadi 2018 alitunukiwa shahada ya uzamivu katika theologia (DMn) Chuo Kikuu cha Theologia cha Concordia cha Marekani.

Mwaka 2010 hadi 2012 alipata shahada ya Uzamili katika Theologia (MTh) katika Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira na  mwaka 2004 hadi 2009 alipata shahada ya kwanza katika Theologia (BD) katika Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira.

Mwaka 2000 hadi 2001 alipata Stashahada katika usimamizi na uongozi katika Chuo Kikuu cha kimataifa cha Cambridge, huku mwaka 2019 hadi 2022 akipata mafunzo ya uongozi wa Kilutheri Chuo Kikuu cha Theologia cha Concordia Marekani.

Alibarikiwa kuwa Mchungaji  Desemba 6, 2009 Kanisa Kuu Imani Mwanza Dayosisi Mashariki ya Ziwa Victoria ambapo amefanya kazi katika nyanja mbalimbali, ambapo  mwaka 2013 hadi 2017 alikuwa Katibu Mkuu KKKT Dayosisi ya Kusini Mashariki ya Ziwa Victoria.

Mwaka 2012 hadi 2022 alikuwa Mkuu wa Jimbo la Magharibi Kahama na mchungaji kiongozi usharika wa Agape Kahama na Mkurugenzi Shule ya Msingi ya mchepuo wa Kiingereza ya Agape Kahama.

Desemba 2022 hadi anateuliwa katika wadhifa huo, alikuwa anahudumu kwenye nafasi ya msaidizi wa Askofu na mkurugenzi wa misioni, uinjilisti na uwakili Dayosisi ya kusini Mashariki ya ziwa Victoria (DKMZV).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *