Dar es Salaam. Kufukuzwa uanachama wa Chadema kwa John Mrema ni utekelezaji wa mkakati wa ndani wa chama hicho, unaodaiwa kufanywa na ngazi ya chini, ukilenga kuwashughulikia makada wote wanaounda kundi la G55.
Taarifa ambazo Mwananchi inazo zinadai mkakati uliopo ni kuwashughulikia G55 kupitia matawi yao. Katika kuhakikisha hilo, kuna timu ya watu wasiopungua watatu wanaoratibu na kusimamia mchakato huo kwa Kanda ya Pwani kwa kupita kila tawi kufuatilia mienendo ya G55.
G55 linaundwa na makada waandamizi waliokuwa na nia ya kuwania ubunge na udiwani katika uchaguzi mkuu utakaofanyika baadaye Oktoba. Hata hivyo, G55 ilingia katika mvutano na uongozi wa Chadema, unaoshikilia msimamo wa ‘No reforms, no election’, wakati kundi hilo likitaka chama hicho kishiriki uchaguzi.
Jana Jumatano, Aprili 30, 2025, Chadema tawi la Bonyokwa, jijini Dar es Salaam, lilitangaza kumvua uanachama Mrema kwa tuhuma za ukaidi, dharau, na kutoheshimu miiko, tamaduni na misingi ya chama, huku mwenyewe akikana kufukuzwa uanachama.

Msemaji wa kikundi cha G55, John Mrema akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Jumanne Aprili 22, 2025. Picha na Sunday George
Katika utetezi wake, Mrema, aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje, amesema bado ni mwanachama wa Chadema, mwenye kadi ya uanachama namba 0111 na anatambulika kwa mujibu wa Kanuni ya 5.1 na 5.2.
“Barua inayosambaa hainihusu mimi kwa sababu haikutaja namba ya uanachama wangu, labda kuna mtu tunafanana majina,” amesema Mrema.
Duru za siasa zinabainisha kuwa kinachoendelea Chadema kinatokana na mpasuko uliotokana na uchaguzi wa ndani wa chama hicho wa Januari 21, 2025, uliomweka madarakani Tundu Lissu kama mwenyekiti, huku Freeman Mbowe aliyekuwa akitetea nafasi hiyo akishindwa.
Wadau wengine wa masuala ya siasa, akiwemo Mbowe, walipendekeza kuundwa kwa tume ya upatanishi ili kutibu majeraha yaliyotokana na uchaguzi huo. Hii ni baada ya kushuhudiwa minyukano ya kambi mbili za Lissu na Mbowe.
Golugwa apigilia msumari
Leo Alhamisi, Mei Mosi, 2025, Mwananchi limemtafuta Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), Aman Golugwa, aliyeanza kwa kusema “case closed” (kesi imefungwa) kuhusu uanachama wa Mrema, akisisitiza kuwa si mwanachama tena na suala lake limeshughulikiwa ngazi ya chini na si makao makuu.
“Kwanza nikiri kuwa barua ya kufukuzwa uanachama niliipokea mimi katika ofisi ya katibu mkuu. Kabla ya uamuzi huo, Mrema alipewa siku 14 kujieleza lakini hakufanya hivyo. Kwa mujibu wa katiba ya Chadema, sisi si mamlaka yake ya nidhamu, bali ni tawi, na Mrema anatoka tawi hilo (Bonyokwa),” amesema.
“Hayo anayoandika sijui anakaa Makongo, ooh mara si tawi langu, anaweweseka. Ni hali ya kawaida tu kwa watu waliochukuliwa hatua, na baada ya muda Mrema atazoea tu… kwamba ameshafukuzwa Chadema,” amesema Golugwa.
Golugwa amedai kuwa anachokisema Mrema kama utetezi ni hali ya kawaida kwa sababu yupo katika kipindi cha mshituko, lakini itafika muda atakubaliana na kilichotokea.
Alipoulizwa kuhusu iwapo fukuza fukuza inalenga G55, Golugwa amejibu: “Mrema ana mrundikano wa mengi na uongozi wa tawi. Kama mtakumbuka Januari mwaka huu, niliingilia kati kusuluhisha kwa kuhimiza mashauriano zaidi. Hili G55 huenda limeongeza zaidi.
“Mrema alikuwa mwanachama wa kawaida na mamlaka yake ni tawi. Ndiyo maana habari zake nyingi zipo huko. Ngazi ya taifa hatuna habari naye, hata mwenendo na tabia zake ulifuatiliwa na tawi lake,” amesisitiza.
Mkakati wa fukuza fukuza
Baadhi ya vigogo wa chama waliozungumza na Mwananchi kwa sharti la kutoandikwa majina yao wamesema kuwa Dar es Salaam kuna viongozi wawili waliokabidhiwa jukumu la kupita kila tawi kutafuta makada wanaounga mkono G55 wanapoishi, kuanzia nyumba hadi mtaa, ili wachukuliwe hatua.
“Hawa jamaa (majina tumehifadhi) wameanza muda mrefu. Wanatembelea matawi yote ya Dar es Salaam. Wakijua kada fulani ni G55, basi wanauliza anakaa wapi, kisha uongozi wa tawi husika waandike barua ya kuwachukulia hatua.
“Kuna matawi mengine hayakufanya uchaguzi. Wakikumbana na hali hiyo wanaghushi ili kuhakikisha wanaounga mkono G55 wanachukuliwa hatua,” amesema kigogo huyo.
Kigogo mwingine amesema watu hao wamekuwa na mkakati maalumu wa kutafuta makada wa G55 wanaoishi mitaa mbalimbali ya mkoa wa Dar es Salaam, ili kuelekeza matawi husika kuwafukuza uanachama.
“Wanachokifanya wanakwenda kila tawi na kutafuta kada anayeunga mkono G55 anakaa wapi, ili kuelekeza viongozi wa matawi kuanza mchakato wa kumfukuza kama ilivyokuwa kwa Mrema,” amesema mtoa taarifa huyo.
…ilishwahi kusemwa na Mrema
Uwepo wa mkakati wa fukuza fukuza kwa kutumia matawi ulidokezwa Aprili 22, 2025, na msemaji wa G55, Mrema, aliyesema makada wanaounda kundi hilo wapo mbioni kushughulikiwa kimya kimya katika ngazi ya matawi.
“Wako watu wa G55 wanaandikiwa barua na matawi yao kwa maelekezo ya chama. Wapo viongozi walioitwa kwenye vikao na kuna wengine wamepewa barua za kujieleza ndani ya siku 14, kwa nini wasivuliwe uanachama. Utamaduni huu si wa nje, ni ndani ya chama, tunashughulikiwa,” alisema Mrema.
Taarifa zilizopo zinadai kuwa wapo makada wengi waandamizi wanaounda G55 waliopo kwenye orodha ya kufukuzwa uanachama kutokana na kupingana na msimamo wa chama hicho, wakionekana kama wasaliti.
Mwita alimwa barua, atakiwa kujieleza
Wakati sakata la Mrema halijapoa, aliyekuwa Katibu wa Sekretarieti ya Kamati Kuu ya Chadema, Julius Mwita, amelimwa barua na uongozi wa Chadema tawi la Nyabisare, wilayani Musoma mkoani Mara, akitakiwa kujieleza mbele ya Kamati ya Utendaji ya tawi, kwa nini anakwenda kinyume na msimamo wa chama.
Katika barua hiyo, iliyoandikwa leo Mei Mosi, ambayo Mwananchi imefanikiwa kuiona, imeeleza kupokea taarifa mbalimbali ambazo Mwita amekuwa akizitoa katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, zikionyesha kuwa anakwenda kinyume na msimamo wa Chadema, hasa ajenda ya “bila mabadiliko hakuna uchaguzi”.
Kutokana na hali hiyo, Katibu wa Chadema tawi la Nyabisare, Jimbo la Musoma Mjini, Samwel Zephania, amemtaka Mwita ajieleze kwa maandishi au afike mbele ya Kamati ya Utendaji Mei 14, kwa kuzingatia siku zilizotajwa.
“Unatakiwa kuwasilisha maelezo yako ya maandishi kwa Katibu wa chama tawi la Nyabisare na kufika mbele ya Kamati ya Utendaji Mei 14, kwa kuzingatia siku zilizotajwa. Uamuzi unaanza leo Mei Mosi,” amesema Zephania.
Mwananchi limemtafuta Mwita ambaye amekiri kuipata barua hiyo leo, akisema: “Nimeipata barua niliyoandikiwa na tawi husika. Kwa hatua ya sasa, naisoma huku nikitafakari.”
Mtazamo wa wachambuzi wa siasa
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Mohamed Bakari, amesema hatua ya fukuza fukuza inaashiria kuwa mpasuko wa uchaguzi mkuu wa chama hicho uliofanyika Januari 21, 2025, bado unaendelea, ingawa si afya kwa watu waliokijenga chama kuvuliwa uanachama.
“Nadhani kuna kitu kinakosekana. Moja ni kazi inayotakiwa kufanywa na uongozi ulioingia madarakani kuziba mpasuko uliojitokeza, lakini bado halifanyiki na ufa unaonekana,” amesema.
“Moja ya wanachotakiwa kufanya ni kuleta utengamano ndani ya chama hicho kwa kuyaita makundi mbalimbali na kufanya maridhiano ili kufikia uamuzi wa pamoja. Jambo jingine ni kuchukua hatua kwa wale wanaoonekana kusaliti chama,” amesema Profesa Bakari.
Hata hivyo, Profesa Bakari amesema uongozi wa Chadema ulipaswa kuanza na maridhiano kabla ya kufikia hatua ya kufukuza uanachama baadhi ya makada wanaounda G55.
“Vyovyote itakavyokuwa, hawa watu wameshiriki kujenga chama kwa muda mrefu. Sio jambo la kujivunia kwa ajili ya uhai wa Chadema kuwafukuza uanachama, hata kama unatafautiana nao. Kama kuna uwezekano, basi wafanye maridhiano kwa hatua ya sasa,” amesema Profesa Bakari.
Mchambuzi wa siasa, Rainery Songea, amesema hatua ya Chadema kuwafukuza uanachama ipo sahihi kama watazingatia hatua zote, ikiwamo kupewa nafasi ya kuwasikiliza.
“Ilivyo G55 wanaenda kinyume na msimamo wa chama unaopitishwa na mikutano mikuu, ikiwemo Kamati Kuu, na hao G55 walikuwa sehemu ya uamuzi.
“Kama unapingana na msimamo, unapaswa kutafuta chama kingine kinachoendana na chenye sera mnazolingana. Hatua ya kushughulika nao inaweza kusaidia ili wasiwakatishe tamaa wenye nia ya kusukuma ajenda hiyo.”
Songea amesema faida ya watu kuja na mawazo mbadala, kiuhalisia, inaonyesha demokrasia inakua, lakini hasara yake, G55 walio wengi misimamo yao inafanana na kiongozi aliyemaliza muda wake, Freeman Mbowe.
“Ukiangalia kwa mbali bado unagundua wanasumbuliwa na makovu ya uchaguzi. Yanawasumbua. Hata ukiwasikiliza baadhi ya G55 katika mikutano yao, wanakuambia,” amesema.