MRADI WA MAJI WA KUCHOCHEA MAENDELEO KWA MJI WA MANYONI

Wakazi wa Mji wa Manyoni, mkoani Singida wamekuwa na matumaini makubwa baada ya uwekezaji wa zaidi ya Sh. bilioni 26 Wa Serikali kwenye Mradi wa Maji Miji 28 kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama kwa kiwango cha juu zaidi kuwahi kufikiwa katika mji huo.

Kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 10.58, sawa na Shilingi Bilioni 26.46, mradi huu mkubwa unalenga kuwafikia wakazi 64,667 wa Mji wa Manyoni, ukitarajiwa kuleta mapinduzi ya huduma za maji kwa asilimia 100 kutoka kiwango cha sasa cha asilimia 78.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Manyoni (MAUWASSA), Mhandisi Lucas Mwinuka, amesema kuwa utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 45 na shughuli za ujenzi zikiwa katika hatua mbalimbali.

“Tumekamilisha uchimbaji wa visima vitatu vyenye uwezo wa kuzalisha jumla ya lita 270,000 kwa saa na ujenzi wa tenki kubwa lenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni 2 pia umekamilika,” amefafanua Mhandisi Mwinuka.

Akielezea kazi nyingine zilizokamilika ni pamoja na ulazaji wa bomba kuu la maji lenye urefu wa kilomita 14.1 kutoka kituo cha visima, huku ujenzi wa kituo cha kusukuma maji ukiwa umefikia asilimia 70. Pia, kazi ya ulazaji wa mabomba ya usambazaji yenye urefu wa kilomita 30 inatarajiwa kuanza Juni 2025 baada ya usanifu wake kukamilika.

Diwani wa Kata ya Manyoni, Mhe. Samuel Lupembe, amepongeza jitihada hizo na kusema kuwa wakazi wa eneo hilo wamekuwa wakisubiri mradi huu kwa muda mrefu kutokana na changamoto ya majisafi, hasa kwa maeneo yanayozidi kupanuka kutokana na ongezeko la watu.

“Mradi huu utakuwa chachu ya maendeleo kwa wakazi wetu kwani utahakikisha huduma ya maji inawafikia hata maeneo ya pembezoni na kuzidi kuupanua Mji wa Manyoni na kuchochea maendeleo kwa wananchi,” amesema Diwani Lupembe.

Kwa upande wake, Fatuma Shabani, mkazi wa Kitongoji cha Chang’ombe, amesema kuwa mradi huu si tu unawaletea faraja ya kupata maji ya nyumbani, bali pia unafungua fursa mpya za kiuchumi kwa kina mama na vijana kupitia shughuli mbalimbali zitakazotegemea maji.
“Kwa mara ya kwanza, tunaona tumaini jipya kwa maendeleo ya wanawake. Tunaweza kufikiria kuanzisha miradi midogo ya kiuchumi kama bustani, ufugaji wa kuku, na shughuli nyingine zitazoimarisha kipato chetu,” amesema kwa shukrani.

Mhandisi Adam Kweka kutoka Kampuni ya GBS Tanzania Ltd wakishirikiana na Kampuni za Upimark na Mhandisi Consultancy, ambao ni miongoni mwa Wahandisi Washauri wa mradi huo, ameahidi kuhakikisha ubora na ufanisi unazingatiwa katika kila hatua ya ujenzi, huku akiahidi ushirikiano na Serikali na wananchi hadi mradi utakapokamilika kikamilifu.

Mradi huo ni ushahidi wa namna Serikali inavyoendelea kuwekeza kwenye huduma za msingi kwa wananchi kwa lengo la kuimarisha ustawi wa jamii, kuleta maendeleo ya kiuchumi na kuijenga Tanzania yenye majisafi kwa wote.

The post MRADI WA MAJI WA KUCHOCHEA MAENDELEO KWA MJI WA MANYONI appeared first on Mzalendo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *