
Dar es Salaam. Serikali imesema wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi wameonesha nia ya kuwekeza katika ujenzi wa miradi mbalimbali iliyopo katika programu ya BSEZ na wapo katika hatua mbalimbali za mazungumzo na taasisi mbalimbali husika za Serikali.
Wakati huohuo Serikali imesema mpaka sasa haijaingia makubaliano (commitment) yoyote na mwekezaji yeyote kwa sasa, huku ikisisitiza kuwa kutokana umuhimu na ukubwa wa programu ya BSEZ, umma utajulishwa kikamilifu katika kila hatua ya utekelezaji wake.
Taarifa ya leo Februari 14, 2025 ya Waziri wa Mipango wa Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo imeeleza kuwa Serikali ipo katika hatua mbalimbali za kutekeleza programu ya ujenzi BSEZ, ikiwa ni moja ya miradi 17 ya kielelezo iliyopo katika Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26.
“Pamoja na mambo mengine, programu ya ujenzi wa BSEZ itahusisha ujenzi wa Bandari, Kongani za Viwanda, Kongani za Tehama, ukanda huru wa biashara, na kituo cha reli. Utekelezaji wa programu hii utafanywa na sekta binafsi kwa kushirikiana na serikali kupitia mpango wa ubia kati ya Sekta Binafsi na Sekta ya Umma (PPP),” imeeleza taarifa ya Profesa Mkumbo.
TPA yakana kuingia mkataba mpya
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Plasduce Mbossa amesema hakuna mkataba wa uwekezaji uliosainiwa baina ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Uwekezaji na Maendeleo ya Saudi-Africa (SADC) kwa ajili ya uendeshaji bandari ya Bagamoyo.
Kauli ya Mbossa inakanusha taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii ikieleza Serikali ya Tanzania imeipa Kampuni ya Uwekezaji na Maendeleo ya Saudi-Afrika (SADC) haki ya uendeshaji na usimamizi wa Bandari ya Bagamoyo.
Katika taarifa hiyo inayosambaa kupitia mitandao ya kijamii iliambatana na picha inayomuonyesha Waziri wa Viwanda na Biashara, Selemani Jafo, Waziri wa Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo kwa pamoja wakiwa kwenye picha na wenyeji wao kutoka Saudi Arabia.
Viongozi hao wa Tanzania kwenye picha hiyo wapo nyuma ya wawakilishi wa Tanzania na Saudia ambao kwa mbele wanaonyesha nyaraka zinazodaiwa ni mikataba.
Pia, nyuma ya picha ya pamoja ya wawakilishi hao yapo maandiko yanayosomeka Tanzania- Saudi Round Table Meeting.
”Hatujasaini mkataba, tukisaini tutawajulisha kama ambavyo huwa tunafanya,” ameandika Mbosa kupitia ujumbe mfupi baada ya kuulizwa taarifa hiyo.
Shirika la Habari la Saudi (SPA), kupitia taarifa yake iliyochapishwa jana Februari 13, 2025 ilimnukuu Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyabiashara wa Saudi, Hassan Al-Huwaizi ikisema idhini hiyo ni sehemu ya mradi wa “East Gateway” wa SADC, unaolenga kukuza biashara na uwekezaji katika eneo la Afrika Mashariki.
Kupitia taarifa hiyo kutoka nchini Saudia Arabia, imeeleza uendelezaji wa bandari hiyo utaongeza nafasi ya Saudi Arabia kama mhimili mkuu wa maendeleo ya uchumi wa dunia, kuvutia uwekezaji mkubwa wa kigeni (hasa barani Afrika), na kuimarisha uwezo wake wa kimkakati katika usafirishaji wa bidhaa zake kwenda kwenye masoko ya kimataifa.
Kwa mujibu wa taarifa ya chombo hicho cha habari, Bandari ya Bagamoyo inashikilia thamani kubwa ya kimkakati kwa Saudi Arabia, kwani inatarajiwa kuwa lango kuu la biashara kwa Afrika Mashariki.
Kuhusu BSEZ
Mradi wa Bandari ya Bagamoyo na Eneo Maalumu la Kiuchumi (BSEZ) ulianzishwa kwa lengo la kupunguza msongamano katika Bandari ya Dar es Salaam na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha usafirishaji katika Afrika Mashariki. Mikataba ya kuanza ujenzi ilisainiwa mnamo Oktoba 2015, ikipangwa kukamilisha awamu ya kwanza ya ujenzi ifikapo mwaka 2017.
Hata hivyo, mradi huu umekumbwa na changamoto kadhaa zilizochangia kusuasua kwake. Mnamo Januari 2016, serikali ilisitisha mradi huo kutokana na vipengele vya mkataba vilivyoonekana kuwa na masharti magumu. Rais wa wakati huo, John Magufuli, alieleza kuwa mkataba huo ulikuwa na vipengele visivyofaa, ikiwa ni pamoja na sharti la kutojenga wala kuendeleza bandari yoyote kuanzia eneo la Tanga hadi Mtwara.
Baada ya kusitishwa, kumekuwa na juhudi za kufufua mradi huo. Mnamo mwaka 2021, serikali ilianza tena mazungumzo na wawekezaji wa Kampuni ya China Merchants Holdings (International) Co. Ltd (CMHI) na Mamlaka ya Uwekezaji ya Oman (OIA) kwa ajili ya kuendeleza eneo dogo la hekta 3,000 kati ya hekta 9,800 za mradi mzima wa BSEZ.
Hadi sasa, mradi wa Bandari ya Bagamoyo unaendelea kusuasua kutokana na changamoto za kimkataba na mazungumzo yanayoendelea kati ya serikali na wawekezaji. Serikali inaendelea na juhudi za kuhakikisha mradi huu unatekelezwa kwa manufaa ya taifa.