Mpenja kutoka utangazaji hadi uigizaji, ishu yake na Azam ipo hivi…

Dar es Salaam. Mtangazaji maarufu nchini Baraka Mpenja siku za hivi karibuni amekuwa gumzo katika mitandao ya kijamii na mtaani, baada ya kuibuka katika tamthilia ya Mwaipopo, akijulikana kama ‘Popo Boy’ kutokana na uhusika aliouvaa.

Vituko anavyovifanya Mpenja katika tamthilia  hiyo vinawakosha wengi katika mitandao mbalimbali ya kijamii kama Instagram,Tiktok na Facebook na nyuma ya stori hiyo ni ukweli unaohusu maisha ya rafiki yake.

Mwananchi limefanya mahojiano maalumu na mtangazaji huyo anaelezea vitu vingi ikiwemo kujibu uvumi unaoendelea mitandaoni kama ameachana  na kutangaza mpira wa miguu.

“Kumekuwa na uvumi mwingi kuhusu mimi kuacha kutangaza mpira wa miguu, nitumie fursa kupitia gazeti la Mwananchi  kuwaambia wapenzi wa soka nchini bado ni mtangazaji, ikifika wakati wa kupumzika basi nitawapisha wengine, maana kuna muda watu wanaweza wakakuchoka kukusikiliza,” alisema.

Alianza kitambo kuigiza

Mpenja anasema alianza kuigiza tangu anasoma sekondari mkoani Mbeya, lakini alishindwa kukiendeleza kipaji chake kutokana na kukosa  mtu wa kumshika mkono, hivyo akaamua kuendelea kusoma.

“Watu wanaweza wakadhani wanawafahamu watu wengine au wanawajua kumbe siyo kweli, ukitaja jina la Mpenja moja kwa moja wanajua mtangazaji wa mpira wa miguu, ila kuna vitu vingi ninavyovifanya nyuma ya pazia hawavijui,” anasema Mpenja na kuongeza;

“Nje na kutangaza natayarisha vipindi na ni mzoefu kabisa ila watu hawajui ndiyo maana mtu ukimwambia naenda ofisini atakuulizwa kwani leo kuna mechi hawajui kitu kingine ninachokifanya zaidi ya kuniona kwenye televisheni au kusikia sauti nikitangaza.

“Talanta ya kuigiza nimezaliwa nayo kwenye kukua kwangu watu wengi nilioishi nao walijua nitakuwa msanii wa filamu au vichekesho, nimeigiza sana katika mahafali ya wanafunzi kuhitimu, sherehe za kidini na nilikuwa mtunzi wa hayo maigizo na mhusika mkuu wa kuigiza.”

Anasema kabla ya kuanza kutamba na tamthilia ya Mwaipopo, mwaka 2008 wakati anamaliza kidato cha nne aliigiza hadi watu wakalia kwa uchungu kutokana na  uhusika aliokuwa ameuvaa.

“Nilishauriwa niwekeze katika uigizaji nitafika mbali, nikawa nawaza nitapata wapi koneksheni ya kuwa mwigizaji mkubwa kipindi hicho nilikuwa Mbeya kijiji, baadaye matokeo yakatoka nikafaulu, nikiaendelea na masomo, nikajikuta nimeanza kutamani utangazaji,” anasema Mpenja na kuongeza;

“Mwaka 2002, kipindi cha Kombe la Dunia nilivutiwa na  watangazaji wakubwa kama Ezekiel Malongo, Ahmed Jongo, Juma Nkamia, baadaye niliowasikiliza kwa uzuri zaidi ni Charles Hilary na Salim Kikeke nikajikuta ninahamishia nguvu  kutimiza ndoto za kufanya kazi hiyo.

“Baada ya kumaliza chuo kikuu nikajiunga na Azam kwa kufanya kazi nyingine, 2017 viongozi wakasema ngoja dogo tumjaribu atangaze dabi ingawa wengine wakawa na wasiwasi kutokana na ukubwa wa mchezo. Tangu kipindi hicho miaka 10 hadi sasa naendelea kutangaza, ndio maana najaribu kufanya vitu vingine  kwa ulimwengu wa digitali ambao una fursa nyingi na ndio maana nimerudi kuigiza kitu ambacho nilikifanya 2008.”

Anasema baada ya kuanza kuzirusha kripu ( vipande vya video) zake za kuigiza mtandaoni kuna watu walikuwa wanamtumia ujumbe na kumpigia simu wakimwambia kazi ya kuchekesha anatia aibu na kujishushia thamani ya jina alilolitengeneza mbele ya wadau wa soka kupitia kutangaza mpira wa miguu.

“Niliwahi kuwajibu baadhi yao kwamba je, katika kazi ya kutangaza imewahi kutokea siku moja ukanitumia mia tano angalau ninywe maji, kama hujawahi kufanya hivyo kipi cha kunifanya nione aibu wakati natafuta pesa kwa ajili ya kuitunza familia yangu na watu wanaonizunguka,” anasema na kuongeza;

“Waigizaji na wachekeshaji wana heshima kubwa, nani anaweza akapuuza mchango King Majuto (marehemu), Rashid Mwinshehe ‘Kingwendu’ tukiwa watoto tulikuwa tunaigiza kuongea kama yeye, kwa uigizaji wa Jacob Stephen ‘JB Bonge la Bwana’ nani atashindwa kuheshimu mchango wake, ndiyo maana nilishangaa kuambiwa nafanya kazi ya aibu, kwa thamani yao ndio maana unakuta wanaonekana katika matukio mbalimbali.”

Anafanya kila kitu

Katika tamthilia ya Mwaipopo kwa asilimia kubwa kila kitu anakifanya mwenyewe isipokuwa kuchukua video na ana uwezo wa kuandaa stori ya filamu, tamthilia na vichekesho.

“Natumia saa tatu kuitengeneza video ya kripu moja kwa maana ya kuweka sauti vizuri, kuchanganya rangi, matukio na nyimbo zinazoendana kitu kinachozungumzwa.

“Miaka saba iliyopita rafiki yangu alipendwa na binti mmoja sasa akawa  anamdharau na kumuona siyo mrembo, akawa anaanzisha mahusiano na wanawake wengine jambo lililofanya wakaachana, bahati nzuri yule dada alimpata tajiri mkubwa aliyemfungulia kampuni na mshikaji wangu akawa amefilisika na wanawake ambao aliwaona warembo wakamkimbia, akawa na maumivu ya mapenzi na kukosa pesa.

“Kaka wa rafiki kumbe alikuwa anafahamiana na binti aliyetendwa na mdogo wake, akamuombea kazi katika kampuni hiyo aliyofunguliwa na mume wake tajiri, jamaa yangu kwenda ofisini alikoelekezwa akakutana na bosi ambaye ni x wake aliyekuwa anamdharau, akajisikia vibaya ila hakuwa na la kufanya zaidi ya kufanya kazi, mashabiki wangu waendelee kuifuatilia tamthilia hiyo wajue kilichoendelea baada ya hapo.”
 

Mwaipopo yamfungulia  njia

Anasema baada ya tamthilia hiyo kurushwa amepigiwa simu na watunzi, waandishi na waongozaji nguli wa filamu mbalimbali nchini wakimpongeza kwa kazi nzuri, huku baadhi ya wasanii wakiahidi kufanya naye kazi.

“Nilipigiwa simu na kaka yangu Jimmy Mafufu aliniambia nitengeneze kipande atakachoigiza katika tamthilia hiyo, nimezungumza mambo mengi na Lamata mtunzi muongozaji wa tamthilia ya Jua Kali, kwa hiyo mazuri mengi yanakuja mbele,” anasema.

Anasema angechagua wachezaji wa kuwashirikisha katika tamthilia hiyo basi wangekuwa ni Clatous  Chama, Dickson Job, Maxi Nzengeli, Kibwana Shomari kutoka Yanga, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ na  Joshua Mutale wa Simba.

“Chama na Nzengeli wangekuwa washauri wangu  kwa sababu ni wacha Mungu, Job angekuwa sharobaro maana anapenda fasheni, Mutale, Kibwana wangekuwa wachekeshaji na Tshabalala katika timu yangu angecheza beki ili tukienda uwanjani tukashangiliwe na wanawake wale ambao wanasema usiniumizie bebi.”

Anajigawaje na majukumu

Anasema anatumia muda mchache kulala usingizi hasa nyakati za mchana, kuhakikisha anawajibikia ajira yake Azam, anasimamia Mpenja Tv, kufanya matangazo na makampuni mbalimbali na kuigiza tamthilia ya Mwaipopo.

“Vijana ili tutoboe kimaisha lazima kujitoa na kupenda kufanya kazi, nje na hapo kesho yetu inaweza ikawa mbaya na kukumbwa na msongo wa mawazo pia nalinda afya, nafanya mazoezi ya kukimbia kila asubuhi ili kupata pumzi ya kutangaza,” anasema.
Mechi za Simba, Yanga

Anasema amekuwa akiona katika mitandao mbalimbali ya kijamii akihusishwa na kushabikia timu mojawapo ya hizo klabu kongwe ila anachokifanya ni kutekeleza majukumu yake kwa usahihi.

“Kwa namna ninavyowapamba wachezaji wakifunga, upande ambao umepoteza mechi hauwezi kufurahishwa na hilo, ndio maana nakuwa nahusishwa huku na kule, ila jambo la msingi nazingatia maadili yangu ya  kazi.” 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *