Baraza la Mawaziri la utawala wa Kizayuni wa Israel linakabiliwa na mgogoro mkubwa usio na mfano wake kufuatia kuendelea vita vya Gaza na Lebanon na kushindwa jeshi la utawala huo kukabiliana na makundi ya muqawama ya Palestina na Lebanon.
Kutokana na kuendelea vita huko Gaza, ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu na utawala katili wa Israel inakabiliwa na mgogoro mkubwa usio na mfano wake, na kushindwa jeshi la Kizayuni kukabiliana na makundi ya muqawama huko Gaza na Lebanon kumezidisha mgogoro huo huko Tel Aviv.
Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni katika matamshi yanayogongana huku akidai kuwa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS, imeshindwa huko Gaza ameibua mshangao mkubwa kwa kutoa pendekezo la kumpa hongo mtu yeyote na hasa Wapalestina watakaosaidia katika kuachiliwa huru mateka wa Kizayuni wanaoshikiliwa na wapiganaji wa Hamas. Kutolewa pendekezo hilo na Netanyahu kunaonyesha kuwa jeshi la Kizayuni na asasi za kiusalama na kijasusi za Wazayuni hazijafanikiwa kukabiliana na Hamas.
Mapema siku ya Jumanne Novemba 19, Netanyahu alisema: ‘Mtu yeyote atakayetuletea mateka wa Israel atapata zawadi ya dola milioni tano.” Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni ameongeza kwa kusema: “Wale watakaotukabidhi mateka Waisraeli, mbali na kupewa zawadi nono, wataweza kupata fursa ya wao na familia zao kuondoka salama Gaza.”

Sambamba na madai hayo ya Netanyahu kuhusu juhudi za kukombolewa mateka wa Kizayuni walioko mikononi mwa HAMAS, vyombo vya habari vya Kizayuni vimeripoti, vikinukuu baadhi ya vyanzo vya habari, kwamba hakuna mazungumzo yoyote ya maana yanayofanyika kuhusu suala hilo. Kwa mujibu wa gazeti la Israel la Yediot Aharnot, likinukuu baadhi ya vyanzo vya habari, hakuna mazungumzo yoyote yanayofanyika kwa ajili ya kuachiliwa mateka na kila kitu kimesambaratika. Hali ya usalama katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na utawala pandikizi wa Israel nayo ini ya kutatanisha na kutokana na kuendelea vita, viongozi wa utawala wa Kizayuni wanakabiliwa na hatari na vitisho mbalimbali.
Aidha polisi na taasisi ya usalama wa ndani ya utawala wa Kizayuni inayojulikana kwa jina la Shabak imewatia mbaroni watu watatu akiwemo brigedia jenerali wa akiba wa jeshi la Israel kwa tuhuma za kurusha moto katika makazi ya Waziri Mkuu Netanyahu. Kwa mujibu wa ripoti hii, watu hao watatu walihamishwa hadi kituo cha mahojiano cha eneo hilo ili kufanyiwa uchunguzi wa pamoja wa polisi na Shabak. Mmoja wa washukiwa waliokamatwa katika kesi hiyo ni afisa wa ngazi ya juu katika Jeshi la Wanamaji la Israel.
Itamar Ben-Gvir, Mzayuni mwenye misimamo ya kufurutu ada na Waziri wa Usalama wa Ndani wa utawala wa Kizayuni amesema: “Leo wanashambulia nyumba ya Waziri Mkuu kwa moto, kesho watashambulia kwa risasi za vita.” Vyombo vya habari vya Israel vimeripoti kwamba Netanyahu siku hizi anafanya kazi akiwa amejificha katika chumba kilichohifadhiwa chini ya ofisi yake kutokana na hofu ya kushambuliwa kwa ndege zisizo na rubani.
Malalamiko katika jeshi na asasi za kiusalama na kijasusi za utawala wa Kizayuni, ni moja ya matokeo ya kuendelea vita vya Gaza na Lebanon na hali ya mgogoro iliyojitokeza katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel). Netanyahu ameendeleza vita kwa ahadi ya kuwatimua Hamas kutoka Ukanda wa Gaza, nalo baraza la mawaziri la utawala ghasibu wa utawala wa Kizayuni kuvuruga mazungumzo ya usitishaji vita ili kutekeleza njama zao hatari dhidi ya Wapalestina, lakini njama hizo zimevunjwa na mapambano makali ya makundi ya muqawama, ambapo leo hii Wazayuni ndio washindwa wakuu wa vita hivyo.

Uungaji mkono na msaada mkubwa wa Marekani na nchi nyingine za Magharibi kwa utawala wa Kizayuni pia haujawasaidia sana Wazayuni ambapo sasa baraza la mawaziri la Netanyahu liko katika hali mbaya sana kisiasa na kijeshi. Upinzani katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu unazidi kuongezeka dhidi ya Netanyahu na baraza lake la mawaziri siku baada ya nyingine kufuatia oparesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa ambapo vyama vya upinzani vinatoa mashinikizo ya kufanyika uchaguzi kwa ajili ya kuliondoa madarakani baraza hilo.