
Jana Simba ilikuwa ikicheza mchezo wake wa 21, huku Yanga ikiwa imekwishacheza mechi 22 za Ligi Kuu Bara kuelekea mchezo wa Kariakoo Dabi unaotarajiwa kupigwa Jumamosi, wiki ijayo.
Tayari vaibu lipo juu baada ya Simba kuirarua Coastal Union kwa mabao 3-0 mjini Arusha jana, idadi sawa na mabao ambayo Yanga iliifunga Pamba Jiji juzi katika mchezo wa mashindano hayo jijini Mwanza, suala ambalo limeibua tambo kwa pande zote mbili za mashabiki wa timu hizo.
Hata hivyo, wakati hali ikiwa hivyo, miongoni mwa wachezaji wa Simba ambao watakaocheza kwa mara ya kwanza Dabi ya Kariakoo dhidi ya Yanga, Machi 8 ni Elie Mpanzu ambaye ameeleza ni kwanini anausubiri kwa hamu mchezo huo wa Ligi Kuu Bara ambao umekuwa ukigusa hisia za mashabiki wa soka katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Mpanzu mwenye mabao mawili katika ligi tangu alipojiunga na timu hiyo kutoka AS Vita ya DR Congo anafahamu umuhimu wa dabi kwa mashabiki wa timu hizo na jinsi inavyohusisha hisia na shauku kwa wapenzi wa soka.
Licha ya kwamba alishuhudia Simba ikipoteza kwa bao 1-0 kwenye mchezo wa raundi ya kwanza dhidi ya Yanga, anasema kuwa mara hii itakuwa ni fursa nyingine ya kutengeneza historia na kuleta furaha kwa mashabiki wa Wekundu wa Msimbazi.
Katika mahojiano maalumu na Mwananachi, Mpanzu anasema kwamba hii ni aina ya michezo ambayo amekuwa akitamani kuicheza kila siku tangu akiwa nyumbani kwao DR Congo, hivyo hana presha ya mchezo huo na amepania kutengeneza matukio mazuri kwa Simba.
“Mchezo huu ni fursa kwangu kuonyesha kile ninachoweza. Najiandaa kikamilifu na sina shaka kwamba tutafanya vyema. Yanga wana timu nzuri, lakini sisi tuko tayari na tutapambana kwa kila kitu ili kuhakikisha Simba inapata ushindi. Hii ni ligi ya ushindani, lakini tuna timu bora,” anasema Mpanzu ambaye kwasasa ni kipenzi cha mashabiki wa Simba.
Mpanzu ameongelea kiwango chake akisema hakijafikia asilimia 100 na bado anajitahidi kupambana ili kufikia kilele cha uwezo wake akijua kuwa Ligi Kuu Bara Bara inazidi kuwa na ushindani na kila mchezaji anahitaji kuonyesha makali yake.
“Bado sijafika kiwango changu bora, lakini naendelea kujitahidi kila siku. Hii ni changamoto kwangu na kwa timu yangu pia. Mashabiki wa Simba wanatarajia makubwa kutoka kwangu, na mimi nipo tayari kutoa kila nilicho nacho ili kuleta furaha kwao,” anasema Mpanzu ambaye alijiunga na Simba katika dirisha dogo akitokea AS Vita ya DR Congo, alikubaliana na changamoto za kuzoea mazingira ya Ligi Kuu Bara, hivyo anaendelea kujiimarisha kila wakati.
Anasema ushindani wa ligi unamfundisha kuwa siyo kila wakati matokeo yatakuwa kama anavyotarajia. Hata hivyo, anasisitiza kuwa ushindi dhidi ya Yanga utakuwa ni hatua muhimu katika kutimiza malengo ya timu na kuendelea kujiimarisha kwenye mbio za ubingwa.
Wakati anapokuwa uwanjani, Mpanzu amekuwa akionyesha umahiri kama winga mwenye kasi na uwezo wa kufanya mashambulizi. Anaweza kucheza kama winga wa kushoto au kulia, lakini pia anaweza kuhamia katikati ya uwanja na kucheza kama namba 10, akichukua jukumu la kuanzisha mashambulizi ya timu.
Vilevile pia uwezo wa kukaa na mpira mguuni na kupenya kwenye ngome ya wapinzani, vitu ambavyo vimemfanya kuwa mchezaji muhimu katika kikosi cha kocha Fadlu Davids. Mpanzu pia anajua kwamba ni lazima ailindie safu ya kiungo na kushambulia kwa umakini ili kuhakikisha timu inapata matokeo bora.
“Ni muhimu kuwa na ushirikiano mzuri kama timu na nashukuru kwa kiasi kikubwa wachezaji wenzangu wanajua namna gani tunaweza kushirikiana.”
LIGI YA BONGO
Mpanzu pia alizungumzia kuhusu ushindani mkubwa ambao unaonekana katika Ligi Kuu Bara msimu huu, ambapo kila timu inapigania malengo na haijali kama inacheza dhidi ya timu kubwa za Simba na Yanga.
Anasema: “Ligi ya Tanzania ina ushindani mkubwa sana. Kuna wachezaji wengi wazuri kutoka ndani na nje ya nchi, na kila timu inataka kushinda. Ushindani huu unafanya kila mechi kuwa ngumu na unahitaji jitihada za ziada. Lengo letu kubwa ni kuhakikisha kuwa tunadumisha ubora wetu.”
KUHUSU UBINGWA
Mchezaji huyo amezungumzia ubingwa wa Ligi Kuu Bara akisema mpango wake ni kuhakikisha anachangia kikamilifu katika kuhakikisha kuwa Simba inapata ushindi dhidi ya Yanga na katika michezo mingine ya ligi ili watimize lengo la kunyakua ubingwa.
Anasema, anajua ushindi katika Dabi ya Kariakoo utawapa nguvu na kuongeza morali katika safari ya kutimiza lengo hilo.
“Tunaweka akili zetu kwenye mechi hii, lakini pia tunajua kuwa baada ya hapo kuna michezo mingine itakayotufanya tuendelee kupigana kwa bidii,” anasema.
AMTAJA MAYELE
Kama mchezaji kutoka DR Congo, Mpanzu anazungumzia pia kuhusu wachezaji wengine kutoka nchi yake waliocheza Tanzania, na anamtaja Fiston Mayele kuwa mmoja wa mastaa ambao amewahi kuvutiwa nao.
Mayele alionyesha kiwango bora akiwa Yanga na alikuwa na mchango muhimu kwenye timu hiyo, na Mpanzu anaeleza kuwa,
“Mayele ni mchezaji mzuri sana na alikuwa akicheza kwa kiwango cha juu wakati akiwa Yanga. Alifikia hatua ya kuitwa kwenye timu ya taifa ya DR Congo hiyo inadhihirisha uwezo wake mkubwa. Ni mtu ambaye napenda kumfuatilia sana kwa sababu alikuwa na mchango mkubwa kwenye timu ya Yanga.”