Mpanzu, Chasambi wang’aa Simba ikiichapa Tanzania Prisons

Ladack Chasambi na Elie Mpanzu wamekuwa habari ya mjini leo baada ya kuiongoza Simba kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Tanzania Prisons katika Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.

Wawili hao kila mmoja aliweka kimiani bao moja huku lingine likifungwa na Jean Charles Ahoua na kuiwezesha Simba kupata pointi tatu muhimu ambazo zimeifanya irudi kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ikifikisha pointi 47.

Mabao ya wawili hao ndio yalionekana kushangiliwa zaidi na mashabiki wa Simba kulinganisha na lingine moja la Ahoua.

Hapana shaka bao la Mpanzu lilishangiliwa sana kutokana na kuwa la kwanza kwake tangu ajiunge na timu hiyo lakini bao la Chasambi ambalo lilikuwa la tatu lilifurahiwa kwa vile Simba iliamua kuufanya mchezo wa  kama tuzo maalum kwake kama njia ya kumuweka sawa kisaikolojia kufuatia kitendo cha winga huyo kujifunga katika mchezo wa Simba na Fountain Gate uliomalizika kwa sare ya bao 1-1.

Simba ilijihakikishia ushindi huo mapema kipindi cha kwanza ambacho pia ilipoteza nafasi tatu za wazi kupitia kwa Mohamed Hussein, Lionel Ateba na Chasambi.

Ahoua ndiye alifungua sherehe ya ushindi wa Simba akimalizia pasi ya Shomari Kapombe katika dakika ya 29.

Bao hilo lilikuwa la nane kwa Ahoua kwenye Ligi Kuu msimu huu akiwa nyuma ya Clement Mzize na Lionel Ateba ambao kila mmoja ana mabao tisa.

Dakika ya 43, Mpanzu alifunga bao la pili akimalizia kwa shuti kali pasi ya Lionel Ateba.

Kapombe tena alimpikia Chasambi bao katika dakika za nyongeza za kipindi cha kwanza na kabla filimbi ya kwenda mapumziko haijapulizwa.

Kipindi cha pili kilianza kwa Tanzania Prisons kuwatoa Amade Momade na Selemani Ibrahim ambao nafasi zao waliingia Ezekiel Mwashilindi na Tariq Simba huku Simba ikimtoa Abdulrazack Hamza na kumuingiza Chamou Karabou.

Mabadiliko hayo yalionekana kuiimarisha kidogo Tanzania Prisons ambayo katika kipindi hicho cha pili haikuruhusu bao lakini hata hivyo nayo ilishindwa kufunga bao langoni mwa Simba.

Kwa kutoruhusu bao jana, kipa wa Simba amefikisha mchezo wa 14 kwenye ligi bila nyavu zake kutikiswa (Clean Sheets).

Mabadiliko mengine ya Tanzania Prisons katika mchezo wa jana yalikuwa ni ya kuwatoa Lambert Sabiyanka, Adam Adam na Meshack Abraham ambao nafasi zao zilichukuliwa na Abdulkarim Segeja, Kelvin Sengati na Evance Daifu.

Simba pia iliwatoa Fabrice Ngoma, Mohamed Hussein, Ladack Chasambi na Yusuph Kagoma ambao nafasi zao zilichukuliwa na Debora Mavambo, Steven Mukwala, Valentine Nouma na Edwin Balua