Mpanzu ameanza balaa kaeni kwa kutulia

KIUNGO mshambuliaji wa Simba Ellie Mpanzu, ameanza kujipata baada ya juzi kutupia bao la kwanza katika Ligi Kuu Baara, wakati Wekundu wakipata ushindi wa mabao 3-0 nyumbani dhidi ya Tanzania Prisons.

Mpanzu aliyeingia Simba kupitia dirisha dogo la usajili lililofungwa mwezi uliopita, alifunga bao hilo baada ya kupokea pasi tamu ya beki wa kulia wa timu hiyo, mkongwe Shomary Kapombe na kumaliza ukame wa kutumika kwa dakika 400 ndani ya kikosi hicho, akiwa pia na asisti moja.

ALIVYOANZA SIMBA

Mpanzu alianza kuitumikia Simba, Desemba 21, mwaka jana, timu hiyo ikiwa ugenini dhidi ya Kagera Sugar na Wekundu hao waliibuka na ushindi wa mabao 5-2.

Katika mechi hiyo, Mpanzu alipewa dakika 57 na kocha Fadlu Davids, akianza kwenye kikosi cha kwanza akionyesha kiwango safi kabla ya kutolewa kumpisha Joshua Mutale.

Fadlu alianza kumpa dakika chache kiungo huyo, ikiwa ni hesabu zake za kumrudishia ubora taratibu kutokana na Mpanzu kukosa kucheza mzunguko wa kwanza wa ligi.

Kabla ya kutua Simba alikuwa na hesabu za kwenda kucheza Ulaya, Baada ya kukwama wekundu walimchukua mwishoni mwa mzunguko wa kwanza.

Hata hivyo, Fadlu alikuwa anaendelea kuridhishwa na ubora wa Mpanzu na taratibu akaanza kumuongezea muda mpaka mechi hizi mbili za mwisho dhidi ya Fountain Gate na Prisons akamaliza dakika 90.

AIPANGUA SIMBA

Kabla ya ujio wa Mpanzu Fadlu alionekana kama anahesabu za kumtumia kiungo Aweso Aweso hata Edwin Balua ambao walikuwa wakipishana kucheza ndani ya kikosi hicho.

Baada ya ujio wa Mpanzu wawili hao wakapotezwa kabisa na nafasi ikachukuliwa na Mkongomani huyo ambaye tangu alipoanza kucheza dhidi ya Kagera hakuwahi kukaa nje, huku akicheza mfululizo mechi sita za ligi na zile za Kombe la Shirikisho Afrika.

KACHANGAMSHA MBELE

Tangu Mpanzu aanze kuichezea Simba, unaona namna safu ya ushambuliaji ya wekundu hao wa Msimbazi ilivyoongeza kutokana na nguvu na kasi ya kiungo huyo.

Simba kule mbele imekuwa ikiwatumia viungo Mpanzu, Jean Charles Ahoua na kinda Ladack Chasambi, ambapo viungo hao watatu wamekuwa wakikimbiza kwa kasi kwenda lango la wapinzani wakiendeleza ubora wao kwa kumpa huduma nzuri mshambuliaji Lionel Ateba.

ANAPIGA MIGUU YOTE

Ubora mwingine hatari kwa Mpanzu ni kwamba huyu ni kiungo anayeweza kupiga kwa miguu yote, ambapo ndani ya mechi hizo sita za ligi amekuwa akionyesha ubora wa kupiga mashuti makali ambayo mengi yamekuwa yakipoteza malengo kidogo kuwa mabao, kitu ambacho kabla kilikuwa hakifanyiki kwa kiwango cha kutosha na juzi bao lake likatokana na shuti kali lililojaa pembeni chini.

DAKIKA 400 BAO MOJA

Juzi bao ambalo Mpanzu alilofunga kwenye mechi yake ya sita, alilipata akiwa ameshafikisha dakika 400 kwenye mechi za ligi na Wekundu hao, baada ya kulitafuta kwa muda mrefu akiwa pia ametengeneza (asisti) moja kwenye ligi na moja ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF).

MGENI WA 52 BARA

Mpanzu anakuwa staa wa 52 kwa kigeni kufunga bao katika Ligi Kuu msimu huu, bao lake likiwa la 129 kati ya 130 yaliyofungwa hadi sasa katika mechi 142 iliyozalisha jumla ya mabao 313, yakiwamo tisa ya kujifunga. Mabao mengine 174 yamefungwa na wazawa 87 akiwamo Ladack Chasambi ambaye naye alifunga bao la kwanza msimu huu kwenye ushindi huo wa 3-0 dhidi ya maafande wa Prisons.

MSIKIE FADLU

Kocha wa kikosi hicho Fadlu Davids anasema ni jambo zuri kwa mchezaji huyo kuanza kufunga na sasa anaamini mabao zaidi yatakuja kutokana na ile hali ya kujiamini kurejea.

Anasema Mpanzu amekuwa na nguvu kubwa kwenye safu ya ushambuliaji kutokana na kasi yake pamoja na kutengeneza nafasi.

Pia anasimulia namna wachezaji walivyoumizwa na matokeo ya mchezo uliopita akisema wenyewe ndio waliokuwa wanahamasishana juu ya ushindi kwenye mchezo wa juzi wala yeye hakuongea sana.

“Nafurahia namna wachezaji wanavyoishi kwa kuitafutia ushindi timu, wakihamasishana wenyewe kwa wenyewe ndio maana imekuwa rahisi kuona wanatengenezeana nafasi ili Simba ishinde.

“Mpanzu ameongeza kitu kikubwa hasa eneo la mbele ambako kumekuwa na ongezeko la utengenezaji wa nafasi na ufungaji wa mabao,” anasema.