Polisi wa Msumbiji, Jumatano ya wiki hii walifyatua risasi za moto pamoja na vitoa machozi dhidi ya wafuasi wa kinara wa upinzani Venancio Mondlane, ambapo walikuwa wakijaribu kuandamana kuelekea katikati ya jiji la Maputo, wanaharakati na wandani wa Mondlane wamethibitisha.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
Kwa mujibu wa duru za idara ya polisi, watu 10 walijeruhiwa bila hata hivyo kueleza sababu za kwanini waliamua kuzuia msafara wa mwanasiasa huyo pamoja na wenzake kuingia Maputo.
Picha jongeo zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii, zinamuonesha Mondlane akiwa na wanasiasa wengine wa upinzani juu ya gari lake, wakitawanyika baada ya milio ya risasi, baadhi ya watu wake wa karibu wakidai polisi walidhamiria kumuua.
Kufuatia makabiliano hayo, mpaka sasa haifahamiki ni wapi Mondlane na wanasiasa wenzake wamejificha ingawa watu wao wa karibu wanasema wako salama.

Maandamano haya yalifanyika saa chache kabla ya rais Daniel Chapo, kutiliana saini makubaliano na baadhi ya vyama vya siasa, makubaliano yanayolenga kumaliza miezi ya mivutano ya kisiasa baada ya ushindi wake wenye utata, huku Mondlane mwenyewe akiwekwa kando kwenye mkataba huu.
Tangu kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa urais uliofanyika mwezi Octoba mwaka jana na mgombea wa chama tawala Frelimo kutangazwa mshindi, taifa hilo limeshuhudia vurugu za wafuasi wa upinzani wanaoendelea kusisitiza kuwa uchaguzi huo haukuwa huru, haki wala kuaminika.