Mourinho azua balaa jingine Uturuki, hatihati kupigwa rungu

Istanbul, Uturuki. Kocha wa Fenerbahce, Jose Mourinho amejikuta tena kwenye mzozo mwingine baada ya kuzua tafrani kubwa katika mechi ya robo fainali ya Kombe la Uturuki kati ya timu yake dhidi Galatasaray, mchezo uliomalizika kwa Fenerbahce kulala kwa mabao 2-1. 

Katika mchezo huo uliochezwa kwenye uwanja wa Şükrü Saracoğlu ambao ni uwanja wa nyumbani wa Fenerbahce, Mourinho alionekana akimshika pua kocha wa Galatasaray, Okan Buruk, kitendo kilichosababisha vurugu kubwa kati ya wachezaji na benchi la ufundi wa timu zote mbili.

Buruk alidondoka chini huku akishika uso wake, hali iliyoibua hisia kali kwa upande wa Galatasaray na kusababisha vurugu zilizopelekea wachezaji watatu kuonyeshwa kadi nyekundu. 

Wachezaji waliopewa kadi nyekundu kutokana na tukio hilo ni Mert Yandas wa Fenerbahce, pamoja na Kerem Demirbay na Baris Yilmaz wa Galatasaray.

Licha ya kwamba Mourinho hakupata adhabu uwanjani, huenda akakumbana na adhabu kali kutokana na picha za video zinazoonyesha alivyohusika moja kwa moja katika kuchochea vurugu hizo. 

Mourinho, ambaye alijiunga na Fenerbahce msimu huu amekuwa na kashfa mbaya pale anapokutana na Galatasaray kwani mwezi Februari, alifunguliwa mashtaka dhidi ya klabu hiyo baada ya madai ya kibaguzi yaliyoelekezwa kwao.

Matukio haya yanamfanya Mourinho kuendelea kuwa mmoja wa makocha wa soka wenye historia ya visa vya utata. Mwaka 2011, akiwa kocha wa Real Madrid, alizua mkasa alipomchoma jichoni kwa kidole Tito Vilanova, aliyekuwa kocha msaidizi wa Barcelona. Tukio hilo lilizua hasira kubwa kwa mashabiki wa soka na alifungiwa mechi mbili, ingawa baadaye adhabu hiyo ilifutwa. 

Mourinho, ambaye amepata mafanikio makubwa katika klabu mbalimbali za Ulaya ikiwemo Chelsea, Real Madrid, Manchester United na Roma na anakabiliwa na shinikizo kubwa kwa matokeo ya timu yake pamoja na vitendo vyake nje ya uwanja. 

Kwa sasa macho yote yameelekezwa kwenye Shirikisho la Soka Uturuki (TFF) kuona iwapo litamchukulia hatua kocha huyo, au ikiwa ataponea kama ilivyotokea mara kadhaa katika historia yake ya ukocha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *