Mount Uluguru kidedea tuzo za madereva

KLABU ya mbio za magari ya Mount Uluguru imetwaa taji la klabu bora ya mwaka 2024  na kupewa tuzo maalum katika hafla ya utoaji zawadi iliyofanyika mwishoni mwa juma katika Hoteli ya Golden Tulip, jijini.

Klabu hiyo ya mkoani Morogoro ilishinda tuzo ya ubora baada ya mchuano mkali na klabu ya Arusha baada ya vilabu vyote kufanikiwa kuandaa mashindano bora kwa mwaka 2024.

“Ni zawadi njema sana kwa wapenda mchezo wa mbio za magari mkoani Morogoro. Nina imani tutafanya mashindano bora zaidi katika msimu huu wa mwaka 2025,” alisema mwenyekiti wa klabu ya Mount Uluguru, Gwakisa Mahigi.

Hafla hiyo iliyojulikana rasmi kama Night of The Titans, licha ya kuwapa tuzo madereva, wasoma ramani na klabu bora kwa mwaka 2024, pia iliwaenzi malegendi na wote waliochangia katika kuendeleza mchezo wa mbio a magari nchini.

Aliasgar Fazal ambaye ambaye ameshiriki mbio za magari kama dereva na kiongozi wa klabu ya Dar es Salaam Motorsports na Kishor Shapriya aliyeshinda ubingwa wa mbio za magari mara tatu akileta Subaru Impreza ya kwanza nchini, ni baadhi ya ‘malegendi’ walioenziwa katika hafla hiyo.

Tuzo hizo za washiriki waliofanya vyema kwa mwaka 2024 zilihusisha nchi nne za Afrika Mashariki na kati kwa sababu wanufaika wa tuzo wanatoka nchi za Tanzania, Kenya, Uganda na Zambia.

Mshindi wa jumla wa mwaka kwa upande  wa madereva ni Manveer Birdi wa Dar es Salaam ambaye alijizolea pointi 101 na kufuatiwa na Gurpal Sandhu wa Arusha aliyepata pointi 73  wakati Randeep Birdi wa Dar es Salaam, alimaliza katika nafasi ya tatu akiwa na pointi 69.

Aliyepata tuzo ya juu kwa wasoma ramani alikuwa Ravi Chana kutoka Kenya ambaye alitengeeza pointi 81 wakati nafasi ya pili ilichukuliwa na Zubayr Piredina aliyekusanya polinti 73 akifungana na Mzambia Dave Sihoka aliyemaliza katika nafasi ya tatu akiwa  pia na pointi 73.

Bingwa wa daraja NRC 2 ambazo ni maalum kwa magari ya kisasa ni Yassin Nasser(Mtanzania) na msoma ramani wake Ally Katumba kutoka Uganda.