Mount Meru kamili upimaji saratani ya matiti, yapokea mashine ya kisasa

Arusha. Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru mkoani Arusha imepokea mashine mpya ya kisasa ya mammografia itakayosaidia katika utambuzi wa mapema wa magonjwa ya matiti, hususan saratani ya matiti.

Mashine hiyo inayojulikana kama ‘Mammography Breast Cancer Screening System’, imetolewa na Serikali na kukabidhiwa kitengo cha mionzi cha hospitali hiyo leo Machi 7, 2025.

Ujio wa mashine hiyo unatarajiwa kuboresha huduma za uchunguzi wa magonjwa ya matiti kwa wanawake wa Arusha na maeneo jirani.

Akizungumza wakati wa hafla ya kupokea mashine hiyo, mtaalamu wa radiolojia katika Hospitali ya Mount Meru, Dk Edward Joseph ameishukuru Serikali kwa kuiwezesha hospitali hiyo kuwa na kifaa hicho cha kisasa.

Amesisitiza kuwa mashine hiyo itawapunguzia wanawake wanaohisiwa kuwa na tatizo la saratani adha ya kusafiri zaidi ya kilomita 120 hadi Hospitali ya KCMC iliyopo Kilimanjaro ili kupata huduma hiyo.

Dk Joseph ameongeza kuwa mashine ya Mammografia, inayotumia X-Ray ya kiwango cha chini, ina uwezo wa kuchunguza tishu za matiti na kugundua mabadiliko hata kabla ya dalili kuanza kuonekana au kutambulika kwa uchunguzi wa kawaida wa mwili.

“Utambuzi wa mapema ni hatua muhimu kwa mafanikio ya matibabu na kuongeza uwezekano wa mgonjwa kupona na mashine, hii ndio itasaidia sana hilo katika kuokoa maisha ya wanawake,” amesema Dk Joseph.

Takwimu zinaonyesha kuwa wanawake 42,000 hugundulika kuwa na saratani ya matiti kila mwaka nchini, huku asilimia 38 pekee ya wagonjwa ndio wanaopata matibabu na kupona.

Dk Joseph amewahimiza wanawake, hususan wenye umri wa zaidi ya miaka 40, kujitokeza na kufanya uchunguzi wa mara kwa mara wa afya zao ili kugundua mapema tatizo likijitokeza.

“Katika kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake, tumepokea mashine hii ambayo awali haikuwepo Arusha kabisa, hivyo wanawake wanapaswa kutumia fursa hii kuhakikisha wanapima afya zao mara kwa mara ili kupunguza vifo vinavyotokana na saratani ya matiti, sio wasubiri hadi dalili zijitokeze au ugonjwa kusambaa kwani huwa vigumu kupona kwa haraka,” amesema.

Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk Alex Ernest amesema Hospitali ya Mount Meru, pia, iko katika hatua za mwisho za kuanzisha kliniki ya matibabu ya saratani.

Kliniki hiyo itawezesha wagonjwa wa Arusha kupata dawa za saratani bila kulazimika kusafiri hadi Dar es Salaam.

“Mbali na kuboresha huduma za uchunguzi wa saratani, tunatarajia kuanzisha kliniki maalumu ya dawa za saratani hapa hospitalini, ili kusaidia wagonjwa wanaohitaji matibabu,” alisema Dk Ernest.