Moto wateketeza wawili ndani ya nyumba

Kibaha. Watu wawili wamefariki dunia huku wengine watatu wakinusurika baada ya moto kuteketeza nyumba walimokuwa wamelala.

Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo Jumapili machi 2, 2025 katika Mtaa wa Mailimoja A Halmashauri ya Mji wa Kibaha Mkoa wa Pwani.

Kwa mujibu wa mmiliki wa nyumba hiyo iliyokuwa inatumiwa na wapangaji, Edwin Byamungu waliofariki dunia hawajui majina yao.

“Nimepigiwa simu usiku juu ya tukio hili, nikaja nikakuta wananchi wanasaidia kuzima wakishirikiana na Jeshi la Zimamoto lakini wapangaji wawili, mwanamke na mwanamume waliokuwa wamelala chumba kimoja wamefariki,” amesema Byamungu.

Amesema awali chumba hicho kilikuwa kinamilikiwa na mtu anayetambulika kama Husna aliyekuwa anajihusisha na shughuli za ujasiriamali na ndiye aliyekuwa anamjua, hivyo waliofariki hawatambui.

Amesema wakati wanaendelea kuzima moto huo Jeshi la Polisi lilifika na kuchukua mabaki ya marehemu hao na kupeleka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani Tumbi.

Baadhi ya wapangaji wamesema walishitushwa na moto huo usiku wa manane na walianza kufanya jitihada za kuuzima, lakini hata hivyo hawakuumudu.

“Hatujui chanzo cha moto huo hadi sasa ingawa ulianzia kwenye chumba cha hao wenzetu waliofariki,” amesema Jonathan Antony.

Kwa upande wake Komba Mustapha amesema alishitushwa na kelele za watu waliokuwa wakisikika kuomba msaada na alipofungua akakuta watu wanazima moto huo.

“Nilirejea saa sita usiku natokea kazini nikaingia nikalala, baadaye nilishitushwa na kelele za watu nilipoenda nje nikawakuta watu wanaendelea kuuzima moto huo,”amesema Mustapha.

Mwenyekiti wa mtaa huo, Athumani Lusambi amesema alifika eneo la tukio baada yakupigiwa simu.

“Tulifanya mawasiliano na watu wa zimamoto lakini mali zote za wapangaji zimeteketea,” amesema.

Diwani wa Mailimoja, Ramadhani Lutambi amesema kuwa tukio hilo limewapa mshituko mkubwa na kuwaacha kwenye wakati mgumu.

Juhudi za kumtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salum Mkorcase ili kuzungumzia tukio hili zinaendelea kufanyika baada ya simu yake kuita mara kadhaa bila kupokewa.