Moto wateketeza bweni la wasichana sekondari Makanya

Same. Moto ambao chanzo chake hakijafahamika, umeteketeza bweni la wasichana katika Shule ya Sekondari Makanya iliyopo Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro.

Moto huo uliozuka leo Februari 14, 2025 saa 12:45 asubuhi, umeunguza magodoro, vitanda na vifaa vya wanafunzi yakiwemo madaftari, masanduku na nguo.

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kilimanjaro, Jeremiah Mkomagi amesema moto huo umezuka wakati wanafunzi wakiwa katika shughuli za usafi wa mazingira kabla ya kujiandaa kuingia darasani.

“Leo Februari 14, 2025 saa 7:26 asubuhi tumepokea taarifa kwa njia ya simu na kujulishwa tukio la moto wa bweni la wanafunzi wa kike, shule ya Makanya iliyopo Kata ya Makanya wilayani Same,” amesema Kamanda Mkomagi.

Baadhi ya vifaa vilivyookolewa kwenye bweni la wasichana la Makanya  lililoteketea kwa moto, Same.

Kamanda Mkomagi hakuna madhara ya kibinadamu yaliyojitokeza.

“Chanzo cha moto huo bado hakijafahamika, madhara yaliyotokea mpaka sasa ni kuteketea kwa magodoro 20, kuungua kwa vitanda 10 vya ‘double decker’ na mali za wanafunzi yakiwemo masanduku, nguo na madaftari,” amesema Kamanda Mkomagi.

Amesema taarifa zaidi ya tukio hilo zitatolewa baadaye.